HABARI

Kwani upinzani wa kisiasa ni adui wa maendeleo?

ZIMEKUWEPO  hisia miongoni mwa nchi za Kiafrika kuwa upinzani wa kisiasa ni kama njia ya kuzorotesha maendeleo! Hisia hizo zinatolewa na serikali zinazokuwa zimeingia madarakani kwa njia ya kudai demokrasia na baada ya kuukalia usukani zikatamani kuiziba njia hiyo ili isije kutumiwa na wengine, pamoja na serikali zilizodumu madarakani muda wote bila kuonesha maendeleo chanya.

Mfano, tumeshuhudia serikali ambazo zimelazimika kushika usukani kwa kupitia misituni, kwa maana ya kuendesha vita katika jitihada za kuzing’oa serikali zinazokuwa madarakani huku zikiweka vikwazo vya kuondoka madarakani kidemokrasia.

Cha kushangaza ni kwamba serikali hizo zinazokuwa zimepita misituni kutokana na njia za kidemokrasia kuwekwa vigingi, badala ya kuzisafisha njia za kidemokrasia ili ziweze kupitika kiurahisi nazo zinazidi kuweka vigingi kana kwamba njia za misituni ndizo pekee  zilizobarikiwa!

Ikumbukwe kwamba harakati zote za kutaka kuchukua madaraka, hususan katika nchi za Kiafrika, ziwe za kiupinzani wa kawaida au hata zile za kupitia misituni, zinaongozwa na neno demokrasia. Kwamba serikali zinazokuwa madarakani zinapuuza sana demokrasia.

Kwahiyo zinakuwepo ahadi lukuki za kujenga na kuimarisha  demokrasia ya kweli pale wapinzani wakiingia madarakani. Lakini kimaajabu, ikishatokea wapinzani wakaingia madarakani ahadi zinabadilika, demokrasia inazidi kuminywa kuliko hata mwanzo.

Kisingizio kikubwa ni cha maendeleo. Kwamba wapinzani wakiingia madarakani watazorotesha au kukwamisha kabisa maendeleo yaliyokwisha kupatikana na yanayoendelea kutafutwa! Ambapo kwa lugha nyingine inajitafsiri kuwa upinzani ni adui wa maendeleo.

Mifano ni mingi. NRM ya Uganda kwa kutumia jeshi lake la NRA ilipigana vita vya msituni kwa zaidi ya miaka mitatu kwa madai ya kuitafuta demokrasia na baadaye maendeleo ya nchi. Lakini baada ya kuchukua madaraka neno demokrasia halitakiwi kusikika tena nchini Uganda, isipokuwa demokrasia nchini humo ni NRM. Zaidi ya hapo ni uchochezi na vurugu!

Inadaiwa nje NRM maendeleo ya nchi hiyo yatavurugika, kitu kinachoonesha kwamba upinzani dhidi ya NRM ni sawa na upinzani dhidi ya maendeleo! Vivyohivyo nchini Burundi, Rwanda na hata DRC.

Ila namshukuru na kumpongeza sana rais msitaafu wa Kenya aliyepewa uprofesa wa siasa, Daniel Toroitich arap Moi, kwa kukubali bila mizengwe kuikabidhi nchi kwa upinzani baada ya yeye kusitaafu. Bilashaka yeye aliamini kwamba maendeleo ya Kenya yangeweza kuendelezwa na wapinzani kuanzia pale alipoyafikisha yeye, ilmradi nao walikuwa ni Wakenya wazalendo.

Kitu pekee cha kutia simanzi ni pale mrithi wake, Mwai Kibaki, aliposhindwa kuwaamini wapinzani wake kuwa nao wangeweza kuyaendeleza maendeleo hayo pale alipokuwa anawania kipindi cha pili cha uongozi wa nchi hiyo na kuifanya Kenya izame kwenye gharika la damu!

Lengo la makala haya ni kuangalia upinzani na maendeleo. Ni kweli upinzani ni adui wa maendeleo kama inavyofanywa ieleweke na walio madarakani katika nchi nyingi za Kiafrika?

Mimi naamini kwamba kitu chochote kisichotaka upinzani, kwa maana ya mabadiliko, hudumaa. Na katika udumavu maendeleo hakuna. Kilichodumaa hakiendelei, maana hakikui.

Tatizo la udumavu katika Afrika limesababishwa kwa kiasi kikubwa na tatizo la kuuhofia upinzani. Tumebaki kukiri tu kuwa sisi ni nchi changa kana kwamba uumbaji wa dunia ulianzia kwa nchi zilizoendelea na sehemu yetu ikaja kuumbwa baadaye!

Lakini tukiyaacha mawazo hayo ya kufikirika na kuamua kuutazama ukweli tutaona kwamba kwa namna ya pekee upinzani ndio umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo katika nchi hizo zinazoitwa za dunia ya kwanza.

Mfano tukichukulia taifa kubwa duniani ambalo kwa miaka mingi limeonekana kuwa mbele kwa karibu kila kitu, Marekani, tutaona kwamba tangu lianzishe upinzani wa kisiasa kwenye miaka ya 1850, limekuwa likipiga  hatua za maendeleo kwenda mbele bila kukwama.

Kila kukitokea aina za mkwamo wananchi wanabadilisha serikali kwa njia za kidemokrasia, wanakiondoa chama kimoja na kukiweka kingine. Kwahiyo kila chama kinachokuwa madarakani kinaelewa kabisa kwamba kikifanya mchezo katika maendeleo ya nchi kinarudishwa kwenye upinzani.

Hilo ndilo linalonifanya niamini kabisa kwamba upinzani upo kuyalinda maendeleo ya nchi tofauti na inavyooneshwa huku kwetu kwamba upinzani unaweza kuyavuruga maendeleo.

Kwahiyo nadhani tusingekuwa watu wa kuomba misaada peke yake katika nchi kama hiyo ya Marekani huku tukiwa tunakiri kwamba nchi hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo, bali pia tungetakiwa kujifunza mbinu ilizozipitia kuyafikia maendeleo hayo.

Maana ni busara kwa mtu mwenye njaa kumpa jembe akalime kuliko kumpa chakula cha masimango kila siku. Kwa mantiki hiyo hatupaswi kuyaangalia tu maendeleo zilizonayo nchi kubwa na kubaki tunayahusudu tu bila kujiuliza maendeleo hayo ziliyapataje na kujaribu kuziiga mbinu hizo.

Kama nilivyoeleza hapo juu, mbinu mojawapo kubwa ya maendeleo ni demokrasia na upinzani wa kisiasa. Hivyo ni vitu ambavyo tunavyo au niseme vimo ndani ya uwezo wetu. Lakini badala ya kuvitumia ili vikachochee uwezo wa kupata maendeleo tunavifanyia “figisu” za kutaka kuvizima visiwepo huku tukiziangalia nchi hizo zinazovitunza vitu hivyo kiumakini jinsi zilivyoendelea na kutuacha sisi udenda ukitutoka!

Mapinduzi ya Ufaransa, 1789 – 99, yaliyouondoa utawala wa kifalme na kuiweka nchi hiyo kwenye utawala wa kidemokrasia ndiyo yaliyoifanya nchi hiyo iwe hivi jinsi ilivyo kwa wakati huu. Pamoja na kuuondoa ufalme mapinduzi hayo yalijenga upinzani nchini humo.

Ikumbukwe nchi hiyo ilifikia wananchi kukosa chakula huku mke wa mfalme akiishangaa hali hiyo na kuuliza kwamba kama wananchi wamekosa mkate kwa nini wasipewe keki?

Hiyo yote kwa sasa inadhibitiwa na upinzani ambapo wananchi wakikosa mkate hawasubiri keki ila wanauondoa utawala uliopo na kuweka mwingine. Upinzani ni rafiki wa maendeleo.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo, anayepatikana kwa anwani ya barua-pepe: prudencekarugendo@yahoo.com na au simu nambari +255784989512

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.