Riziki Shahari: Mamlaka ya Bunge kikatiba siyaoni

UKIJUA historia ya ujanani kwake alivyokuwa akisoma hadi alipohitimu elimu ya kidato cha tano katika Shule ya Wasichana ya Korogwe mwaka 1980, ndio utaelewa ni kwa nini leo Riziki Shahari Mngwali ametokea kuwa mwanamke mkakamavu asiyeyumba kimsimamo.

Nimebaini kuwa hivyo ndivyo alivyo Bi Riziki, mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na mbunge wa Viti Maalum.

Mama huyu, mzaliwa wa mwaka 1960, ni kiongozi shupavu aliyejijengea heshima kubwa tangu akiwa katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) lililodumu kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2013 mpaka 2014.

Bi Riziki ni mwingi wa maelezo yenye maneno mazito ambayo huachi kufikiri mara mbili ukiyasikia. Wala hana muhali akijisikia kusema.

Akiipata nafasi ya kusema jambo analolijua na kuliamini, husema hasa. Hafichi kitu na hana sababu ya kudanganya. Huwa anajitoa na kusema ukweli mtupu kinagaubaga.

Katika mahojiano mahsusi na MwanaHALISI yaliyofanyika Jumatano wiki iliyopita kwenye ofisi ya wabunge wa CUF jijini Dar es Salaam, mbunge huyo anasema ukakamavu wake ni wa asili tangu akiwa shule.

Anakumbuka visa mkasa vitatu vilivyomsukuma kuingia kwenye siasa. Mosi, anasema wakati akisoma kidato cha tano na sita katika shule ya wasichana Korogwe ya mkoani Tanga, walifundishwa somo la siasa iliyoelekeza namna ya kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pia jioni walipata mafunzo ya siasa ya lazima kutoka CCM yaliyojumuisha hata wale wanafunzi ambao hawakupangwa kusoma somo la siasa.

“Sikuona umuhimu wa kurudia kufundishwa kitu kimoja mara mbili. Nilihoji kuhusu hili na wakati wa mahafali ya kidato cha sita tukalazimishwa kufanyiwa sherehe pamoja na waliosoma mafunzo kuhusu CCM ambao hawakuwa wahitimu.

“Tulipohoji, tukanyimwa kadi ya uanachama ya CCM,” anasema Riziki.

Kadi hiyo anasema ndiyo iliyotumika kama kiambatanisho cha kujiunga na chuo kikuu na hata mafunzo ya kijeshi jambo amabalo anasema lilikuwa linawanyima haki ya kupata elimu kwa sababu tu ya kukosa kadi.

Kisa cha pili, anasema, ni wakati akituma maombi ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, katika fomu za maombi ilitakiwa pia maelezo ya wajumbe wa CCM wa mtaa alioishi kuhusu ushiriki wake katika kujenga chama.

“Basi mama yangu akachukua zile karatasi na kuzipeleka kwa wajumbe. Wale wajumbe wakata niende mwenyewe. Mama akawambia kwa kuwa wananifahamu fika wangeweza tu kunijazia bila ya mimi kuwepo; wakagoma kujaza, nikashindwa kutuma maombi, badala yake nikaomba nafasi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nikapata,” anaeleza Riziki.

Je, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakukuhitajika maelezo ya wajumbe wa shina wa CCM? Anasema, “Chuo Kikuu Dar es Salaam sikupata shida, wao walitaka tu kadi ya CCM ambayo nilikuwa nayo.”

Kisa cha tatu ni kilichomhusisha kada wa CCM. Alikuwa kiongozi ila hana uhakika ni ngazi ipi lakini anahisi alitoka wilayani. Anamkumbuka kuwa na kiburi. Alifika shuleni kwao Korogwe na kuitisha mkutano na kuanza kuwatisha.

Anasema kiongozi huyo aliwatisha kwamba angewaweka ndani kama wangehoji chochote kuhusu utawala au serikali na akawapa mfano namna alivyomweka ndani kijana mmoja baada ya kuhoji kwa nini walilazimishwa kusema “zidumu fikra za Mwalimu Nyerere.”

Kijana huyo alisema kwa mujibu wa Kiswahili fasaha, si sahihi kusema “zidumu fikra za Mwalimu Nyerere” wakati mwalimu alikuwa bado hai. Kauli hiyo ingefaa kutumika kama mwalimu angekuwa amekufa. Akaswekwa ndani.

“Hivi visa vitatu vilitosha kunifanya kuuchukia utawala wa CCM kwa kuwa niliona haukutoa uhuru. Ulikuwa kandamizi… nilitamani siku moja niingie kwenye siasa nitetee haki hata kama nisingekuwa kiongozi katika siasa,” anasema Riziki.

Kwa sasa Riziki ni mbunge, nafasi aliyoipata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kupitia utaratibu uliowekwa na chama chake. Japo si mara yake ya kwanza kuwania nafasi hiyo. Mwaka 2005 aliomba lakini hakubahatika.

Anasema matarajio yake na anachokiona bungeni ni tofauti. Anavyoamini, uhuru na demokrasia pana ni muhimu ili nchi kufikia maendeleo.

Anasema “niliingia bungeni kwa hamu kweli nikidhani ni chombo kikubwa kinachowakilisha wananchi na kinachofanya maamuzi kwa kujitegemea. Lakini ni tofauti.”

“Nilitarajia sisi wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wasimamizi wa serikali. Yale mamlaka ya kikatiba ya Bunge siyaoni katika bunge hili,” anasema.

Anatoa mfano kuwa wabunge wa upinzani wanapoihoji serikali au kuishauri, mara nyingi wanazuiwa. “Kiti cha spika au wabunge wa CCM wanatumika kuitetea serikali. Sio wajibu wao,” anaeleza Riziki.

Mbali na Bunge kutumika kama wakala wa serikali, Riziki anaona mbunge mmoja mmoja hapewi hadhi inayotakiwa kama mwakilishi wa mamilioni ya wananchi. Badala yake, hata hukumu dhidi yake zinatolewa kama mtu binafsi.

“Lakini bado sijakata tamaa. Vichwa makini vya wapinzani vilivyopo mle ndani (bungeni) vinanitia moyo. Hata wananchi nao wananitia moyo. Wanaelewa kila kitu kinachoendelea bungeni. Si wajinga,” anasema.

Akieleza hali ya demokrasia nchini, anasema “Ni mbaya. Huwezi kuwa na demokrasia bila ya kuruhusu midomo kuzungumza. Kinachofanyika sasa ni hofu, na makatazo ndiyo yametanda. Siasa ni maisha ya kila siku. Hakuna kipindi maalum cha kufanya siasa.”

Anasema utendaji wa serikali si mzuri. Unaweza kuwa na nia na mambo mazuri, lakini haufuati utaratibu, sheria na kanuni ambazo imejiwekea.

Riziki haachi kueleza athari za mgogoro wa uongozi ndani ya CUF, anaoamini uliasisiwa na Profesa Ibrahim Lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, kwa msaada wa vyombo vya serikali, ikiwemo ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Mgogoro huu unatuathiri kiasi chake. Fedha za ruzuku zimezuiliwa kwa sababu ya suala hili. Wabunge na chama tunashindwa kuendesha shughuli za maendeleo katika majimbo ipasavyo. Tunalazimika kuchangishana mfukoni,” analalamika.

Riziki ni mtaalam wa Sayansi ya Siasa, elimu aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ngazi ya Shahada mwaka 1982 hadi 1985. Pia ana Shahada ya Uzamili ya Masuala ya Kimataifa aliyoisomea katika Chuo Kikuu cha Colombia, Marekani.

Elimu ya sekondari alisoma shule ya wasichana Kisutu na elimu ya msingi aliipatia Shule ya Msingi Ilala Bungoni, Dar es Salaam mwaka 1967 hadi 1973.

Mwaka 1985/86 alifundisha Shule ya Sekondari ya Masjid Quba ya jijini Dar es Salaam. Riziki alifundisha masuala ya diplomasia mwaka 1986/2015 katika Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam, na baadhi ya aliowafundisha ni wabunge Nape Nnauye (Mtama), Marry Mwanjelwa (Viti Maalum) na Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini).

TANBIHI: Makala hii iliyoandikwa na Pendo Omary ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi katika toleo lake la tarehe 17 Julai 2017. 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.