Nguzo ya nne ya mitaji ya mafanikio ni rasilimali asilia

Hii ndio hali halisi ya waendesha Gari za Ngombe wanavowatumia Wayama hawa kwa kujipatia Riziki zao.

Hadi sasa, kwa msomaji anayefuatilia mfululizo wa uchambuzi wangu wa nguzo za mitaji halisi ya kutufanikisha katika maisha, atakuwa amegundua kuwa kumbe ni kweli kwamba fedha si mtaji, bali ni matokeo au mapato yatokanayo na mitaji mingine. Vitu vyenye thamani kubwa kuliko vyote si fedha, bali afya njema, fikra, vipaji ndani ya watu, na sasa rasilimali asilia.

Wanaoujua uchumi wa dunia hukiri kuwa akiba nzuri na njema si fedha zilizoko benki au mfukoni mwako. Yale ni makaratasi tu au namba, bali ukiweka akiba ya madini kama dhahabu, almasi na vito vingine vya thamani, na ukamiliki ardhi, una akiba isiyoyumba, isiyooza wala kuathiriwa na chochote, hata ukitokea mfumuko wa bei za vitu vyote. Thamani ya ardhi, madini na rasilimali zingine asilia, ndio utajiri wa uhakika duniani kote. Hivyo basi, katika makala haya nitazijadili rasilimali asilia zikiwa mojawapo ya nguzo za mitaji ya kustawisha maisha yetu.

Rasilimali asilia (natural resources) ni urithi mkubwa tulionao hapa duniani. Rasilimali (resources) ni vitu vyote vinavyotumika vinapohitajika. Hapa neno asilia (natural) ni kitu chochote cha asili, kinachopatikana katika mazingira yetu pasipo kutengenezwa, kuumbwa au kusindikwa na watu. Rasilimali asilia (natural resources) ni vitu vya asili kama vile hewa, maji, ardhi, vyanzo vya nishati (mfano mwanga wa jua, gesi asilia, makaa, mafuta ghafi, nk), mimea, wanyama, madini, anga, nguvu za uvutano (magnetic forces), nk.

Rasilimali asilia hutumika kukidhi mahitaji ya viumbe hai tukiwemo watu, maana nasi ni rasilimali watu (human resources). Dunia yetu ni sayari pekee iliyojaa rasilimali asilia kwa wingi kila upande wa mazingira yetu. Uhai na maisha yetu hutegemea moja kwa moja uwepo wa rasilimali asilia. Viumbe hai hatuwezi kuishi bila hewa, maji na mimea. Hatuwezi kujenga nyumba, kupata makazi na chakula pasipo ardhi. Hatuwezi kuendesha mitambo, magari, ndege na vyombo vingine vya moto pasipo mafuta, upepo na madini ya chuma. Pasipo jua hatuwezi kuwa na mimea, umemejua na mwanga.

Tayari nimejadili katika makala yaliyopita nguzo za mitaji ya mafanikio ya afya njema ya miili, fikra na vipaji. Lakini nguzo hizi haziwezi kufanya kazi pasipo rasilimali asilia. Kwa sasa dunia inakaribia kuwa na watu wapatao bilioni nane. Kadri watu tunavyoongezeka ndivyo mahitaji ya rasilimali asilia huzidi kuongezeka. Mahitaji ya watu yamekuwa mengi na shughuli zimezidi kuongezeka na kusababisha upungufu kwa baadhi ya rasilimali asilia. Niainishe kidogo baadhi ya rasilimali asilia muhimu kama ifuatavyo:

  • Hewa

Kama tujuavyo, hewa safi ni muhimu sana kwa ajili ya uhai wetu duniani. Na bahati iliyoje kwamba hewa hupatikana bure kwa ajili yetu, mimea na wanyama. Endapo hewa ingekuwa inauzwa kama tunavyouziwa mafuta, umeme, vyakula, nk.; naamini wengi tungepukutika! Kutokana na umuhimu huo wa hewa safi kuna haja ya kuongeza juhudi za kudhibiti uchafuzi wa hewa.

  • Maji

Japo dunia kwa sehemu kubwa imefunikwa na maji lakini mengi hayajahifadhiwa na kusambazwa vya kutosha ili kukidhi mahitaji ya nyumbani, viwandani na umwagiliaji. Tumewahi kujadili huko nyuma kuwa maji ni rasilimali asilia yenye upekee kwa kuwa haina mbadala.

Nchi yetu imebarikiwa sana kwa kuwa na rasilimali maji kwa wingi. Ni mtaji muhimu kwa maendeleo ikiwa tutaitunza, kuihifadhi na kuitumia vizuri. Misri ina mto mmoja tu, lakini inautunza na haijawahi kukumbwa na njaa au kukosa nishati itokanayo na maji. Sisi tuna mito mingi na vyanzo vingi vya maji pamoja na mvua nyingi lakini hatuitumii ipasavyo kwa ajili ya maendeleo yetu.

  • Vyanzo vya nishati

Vyanzo vya nishati ni kama mwanga wa jua, upepo, makaa, mafuta ghafi, gesi asilia, nk. Uhai wetu, mimea na wanyama hutegemea sana nishati ya jua. Upepo tunautumia kujaza matairi ya magari na kuzalisha umeme. Makaa ya mawe yanatumika sana viwanadani na nyumbani. Mafuta, iwe dizeli, petroli, gesi asilia au mafuta mazito, huendesha mitambo na kuturahisishia kufanyia kazi mbalimbali.

Kuna nchi ambazo ni tajiri sana kutokana na rasilimali ya mafuta, hasa nchi za Uarabuni, Amerika Kusini na baadhi ya nchi za Afrika. Miaka ya hivi karibuni Tanzania pia imegundua kiwango kikubwa cha mafuta na gesi asilia hususan ukanda wa mwambao wa Pwani na maeneo ya bonde la ufa. Dunia nzima inasadikika kuwa na akiba ya mafuta na gesi asilia ardhini ya kututosha kwa miaka 60 hadi 100.

  • Ardhi

Ardhi ni rasilimali muhimu sana na wakati huohuo ni mtaji mkubwa kote duniani. Haijawahi kupungua thamani hata siku moja! Kila tunachokula hutokea ardhini. Ukila mboga, kunde, matunda, wanga, nyama, nk.; hutokana na ardhi. Mwili huu hulishwa na vitu vinavyotoka ardhini. Mboga humea kwa kunyonya virutubisho vya kwenye udongo na kisha kuingia na kuijenga miili yetu.

Nyama tunazokula pia hutokana na udongo pale ambapo wanyama hula nyasi, zikajenga nyama zao na kisha kuja kwenye miili yetu tunapokula. Tuna miili ya udongo na kwenye udongo inarudi. Aidha, ardhi ni hifadhi kubwa ya rasilimali zingine kama madini (dhahabu, almasi, chuma, nk.), mafuta, gesi, makaa na maji.

  • Madini

Utajiri wa madini na umuhimu wake tunaujua. Ni hivi karibuni tulisikia makampuni mbalimbali duniani yanavyotajirika kwa uchimbaji wa madini hasa yaliyopo barani Afrika. Tanzania tumebarikiwa kuwa na aina nyingi za madini ambapo hatuwezi kutembea kilomita 5 bila kuwepo kwa aina fulani ya madini.

Kuna haja ya kuungana pamoja kuhakikisha kuwa rasilimali madini inanufaisha vizazi vilivyopo na vijavyo pasipo kuruhusu uporaji unaoendelea sasa. Na kwa kusema hivyo, tuiombee na kuisimamia serikali iweke mbele uzalendo katika mikataba. Pale itakapobidi makampuni yanayotupora yasitishwe kwa kuwa hata tusipochimba sasa madini hayataoza, watakuja kuchimba watoto wa watoto wetu.

  • Mimea

Tuna kila aina ya mimea. Tuna misitu, vichaka, nyasi, nk. Mimea inatupa mboga, mbegu za vyakula mbalimbali, dawa za kila aina na miti ya kujengea nyumba zetu na kutoa samani za kila sampuli. Tusisahau pia kuwa hewa safi tunayovuta ya oksijeni inatokana na mimea. Hewa chafu ya ukaa tunayoitoa humezwa na mimea. Mimea kama mchicha, pilipili, bamia matikiti, miti ya matunda, nk.; ni nguzo muhimu ya mitaji ya mafanikio katika uhai na maisha yetu.

Ukiwa na kipande cha ardhi, ukiwa na msitu, ukiwa na kisima cha maji, una utajiri mkubwa wa kukupatia chochote utakacho. Si rahisi kuibiwa au kushuka thamani. Gari linachakaa na kuharibika, fedha taslimu unaweza kuibiwa au zikashuka thamani, lakini si ardhi. Nawaasa Watanzania wote tutawanyike kwenda kwenye maeneo ya wazi tukashike na kumiliki ardhi, kabla ya sisi na watoto wetu hatujawa wapangaji katika ardhi ya nchi yetu!

TANBIHI: Makala hii iliyoandikwa na Gwappo Mwakatobe ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mwelekeo la tarehe 7 Agosti 2017.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.