HABARI

Nguzo ya tatu ya mitaji ya mafanikio ni vipaji

Kila mtu aliyezaliwa hapa duniani anacho kitu pekee alichojaaliwa nacho. Si umbile lake, elimu yake, umaarufu wake, usomi wake, cheo chake katika jamii, au utajiri wake wa vitu na fedha; la hasha, ni kipaji chake. Uwezo wa kiasili ndani ya mtu katika maumbile, nafsi na roho yake huitwa kipaji. Kinatoka ndani yake. Vipaji ni tunu au zawadi toka kwa Mungu ambayo hakuna anayeweza kutunyang’anya au kutuibia mpaka tutakapokufa.

Fedha na magari vyaweza kuibiwa, nyumba inaweza kuanguka, kubomoka, kubomolewa au kuungua, lakini vipaji hubakia kuwa nasi daima. Ni kama nyuki wanavyotengeneza asali tamu na ya ubora wa viwango vya hali ya juu, lakini hawafundishwi na yeyote wala kusomea popote. Hawana stashahada wala shahada! Ni uwezo wa asili ulio ndani yao. Ndivyo vipaji vyetu vilivyo, ni kama uwezo wa nyuki ulivyo katika kuzalisha asali tamu.

Vipaji vinatofautiana baina ya watu kama ambavyo viungo vya mwili viko tofauti na kila kiungo kina kazi yake tofauti. Macho yana kazi tofuati kabisa na pua. Mikono ina kazi tofauti kabisa na masikio. Moyo una kazi tofauti na kongosho. Meno yana kazi tofuati na vidole, nk.; lakini viungo vyote hufanya kazi tofuati kwa ajili ya faida ya viungo vyote na mwili wote.

Jamii ni kama mwili, una watu tofauti wenye uwezo au vipaji tofauti kama ambavyo mwili una viungo tofauti vyenye uwezo tofuati. Watu, kama viungo vya jamii tunapaswa kutumia vipaji vyetu tofauti kwa faida ya watu wote na jamii nzima. Hilo ndilo kusudi la Mungu la kutujaalia vipaji au uwezo tofauti kwa ajili ya kutufaidisha wenyewe, kufaidiana na kuifaidisha jamii.

Kipaji ni mtaji na nyota muhimu inayotupa fursa ya kung’ara na kustawi kimaisha. Mathalani, zama hizi kipaji cha kusakata kandanda ni fursa na utajiri mkubwa endapo vijana wetu watuzitumia fursa zilizopo na sisi kuwapa fursa. Tusiwanyime fursa kama ambavyo Zanzibar imekosa fursa ya kung’arisha vijana wetu kusakata kandanda kimatiafa kupitia CAF barani Afrika na ulimwenguni kote kupitia FIFA. Vipaji vinatupa nafasi ya kugundua malengo muhimu katika maisha yetu na kutuwezesha kuyatimiza.

Nimesema kila mtu aliletwa hapa duniani kwa kusudi maalum na la kipekee. Ili kutekeleza kusudi hilo, Mungu katujaalia vipaji vya uimbaji, uigizaji, ufundi, uchoraji, uchongaji, ususi, uchezaji muziki, uchekeshaji, uchezaji michezo mbalimbali, ujasiriamali, utabibu, ualimu, uongozi katika jamii, ugunduzi, nk. Ni vipaji ambavyo tunazaliwa navyo kwa ajili ya faida ya mwenye kipaji na jamii nzima.

Nimebahatika kuzunguka nchi nzima na kuona vijana wanavyotengeneza simu kwa uhodari lakini hatuna shule au chuo chochote cha kufundisha kutengeneza simu. Ni vipaji vya ufundi wa vifaa vya elektroniki ndani ya vijana. Wanajitahidi sana kuvionesha vipaji vyao, lakini kwa bahati mbaya tunathamini sana vyeti badala ya ubunifu na vipaji. Tunapaswa kuvitambua, kuvienzi, kuviendeleza na kuwatunukia vijana hawa. Vitabu tunavyosoma, teknolojia tunayoiona, sanaa tunayoishuhudia, nk.; vilivumbuliwa na wenye vipaji maalum, wengine hata bila ya kwenda shule maalum au rasmi.

Najua kuna watu wanalalamikiwa au kulaumiwa kuwa hawana ubunifu. Lakini kila mtu ana upekee katika jamii kupitia kipaji chake. Hakuna mtu yeyote yule mwenye afya njema asiye na kipaji. Kuna mtu nyumbani kwetu Mwakaleli anapiga sana marimba na kuimba. Kila afikapo na kuanza kupiga na kuimba, watu huacha kazi zao na kujumuika naye kujimwayamwaya. Anapaswa kupewa fursa na kuanza kufaidika na kipaji chake huku akiendelea kutuburudisha kwa kipaji chake cha kuparaza marimba.

Hata hivyo, watu wengi tunashindwa kabisa kuvitambua, kuviendeleza na kuvitunza vipaji vyetu. Unaweza ukawa unatafuta mtaji wa kuanzia maisha au kuzunguka kila kona kutafuta ajira, kumbe unatembea na ajira au mtaji wako ambao labda ni sauti yako nzuri kwa kuimba. Ni muhimu sana kutambua kipaji chako ambacho ni mtaji wa kukupa ajira. Ukitambua kipaji chako na kukitumia ipasavyo utakuja kuwa mtu muhimu sana katika jamii.

Vijana wanaosakata kandanda, hasa nchini China na katika nchi za Ulaya, wana mishahara minono na mikubwa kupindukia ambayo hulipwa ndani ya juma moja. Hawasubiri mwisho wa mwezi. Kuna baadhi yao hulipwa takribani shilingi milioni 600 kwa juma! Ni kweli wengi hawajasoma lakini vipaji vyao vya kusakata kabumbu vimekuwa mtaji unaowafanya wawe matajiri kuliko wasomi na kuweza kuwaajiri wasomi.

Wengi tuliosoma na kuwa na shahada na utaalamu wa kutukuka, hatuufikii utajiri wa Nasib Abdul almaarufu Diamond Platinumz. Kipaji chake cha kuimba kimemfanya awe tajiri mkubwa na mwenye miradi ya maana. Aidha, nadhani wanaoongoza kwa utajiri duniani si wafanyabiashara, bali wale wanaotumia vipaji vyao kujiendeleza kama ambavyo Bill Gates hakusoma sana, lakini kipaji chake cha ufundi wa kompyuta na vifaa vya elektroniki, kimemfanya awe tajiri namba moja duniani kote.

Angalia mazingira unayoishi na watu wanaokuzunguka. Kama wanapenda kipaji chako na kukuunga mkono endelea kuishi hapohapo, lakini kama hakuna anayejali kipaji chako nenda sehemu unayokubalika. Kama unaishi sehemu ambayo hawathamini muziki wa ala na nyimbo zako za asili, tafuta mahali pengine na kuendeleza kipaji chako huko. Maisha ni kipaji chako na unaweza kuishi na kustawi nacho popote pale.

Ili kudumisha kipaji chako, nashauri kifanyie mazoezi na tunza mwili wako. Mazoezi huimarisha na hukomaza kipaji chako. Kuna haja kubwa ya kukifanya kipaji chako kionekane na/au king’are ili watu wakuone na kuutambua uwezo wako na kisha kukutambua wewe baada ya kwanza kujitambua wewe mwenyewe. Kipaji chako kikubebe na kukuinua badala ya kuwategemea wanadamu wanaoweza kukuingiza katika utumwa na kukunyonya. Kipaji chako awe ndiye mwajiri wako mkuu – boss wako!

Je, unapenda ufugaji? Fuga na jiendeleze. Je, unapenda kilimo? Lima na jiendeleze. Je, unasukumwa kufundisha katika fani fulani unayoipenda? Jifunze ualimu uwe mwalimu wetu. Je, una ufundi wowote? Ongeza maarifa na vifaa. Je, unaguswa kuitumikia jamii? Jitume na uwe na huruma, ukarimu, kujali wengine na moyo wa utumishi kwa wengine, maana hiyo ni misingi ya utu. Mojawapo ya hayo, ni kipaji chako ulichojaaliwa nacho.

Aidha, uwezo wako wa kuongea vizuri, kuimba vizuri, kuchekesha wengine, kupiga vizuri ala za muziki, kuumudu mchezo wowote ule ikiwemo kusakata kandanda, kusuka, kufinyanga vitu, kushona, kupamba sehemu mbalimbali, kupika vizuri, kutengeneza vitu mbalimbali, kuandika mambo mbalimbali, kuchonga vitu mbalimbali, kuchora picha mbalimbali, nk.; ni kipaji, kipawa, ajira na mtaji wako wa kukufanikisha kimaisha. Uwezo huo upalilie, uendeleze, uimarishe, utunze na jitunze ili uufaidi na kuwafaidisha wengine.

TANBIHI: Makala hii ya Gwappo Mwakatobe ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mwelekeo la tarehe 1 Agosti 2017

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.