Nguzo ya sita ya mitaji ya mafanikio ni teknolojia

Huku niliko eneo la bonde la Mwakaleli, sihitaji kwenda mjini kutafuta kazi za ushauri elekezi (consultancies) ninazofanya. Huwa nawasiliana na taasisi mbalimbali zilizopo nchini na hata za nje ya nchi kuomba kazi, hususan za kuchambua na kuandika masuala anuai ya kijamii. Namaliza kila kitu na kuwasilisha juu-kwa-juu kupitia teknolojia ya mawasiliano. Ndivyo ilivyo kwa nyanja zingine za kazi mbalimbali za kibinadamu. Inatumika teknolojia.

Teknolojia yoyote ile, kwa ajili ya kazi yoyote ile, ina kazi kuu nne: kurahisisha kazi, kuleta tija au kuongeza uzalishaji (productivity), kuongeza ubora (quality improvement) na kuhakikisha usalama wa huduma na/au bidhaa tunazozalisha. Basi! Bado naamini tunapaswa kuendelea zaidi na pengine kugundua teknolojia za aina nyingi. Na kwa kusema hivyo, hakuna anayebisha kuwa teknolojia ni mojawapo ya nguzo msingi za mitaji ya mafanikio katika maisha yetu. Hongera kwa wagunduzi, na zaidi sana atukuzwe Mungu atupae vipaji vya ugunduzi ndani yetu.

Historia na Mchango wa Teknolojia Kimaendeleo

Inasadikika zama za kale (ya kale sana!) watu walikula nyama mbichi, viazi vibichi, kunde mbichi na mboga za majani mbichi. Baadaye wakagundua teknolojia ya kuwasha moto kwa kugonganisha mawe au kupekecha vipande vya miti kwa kutumia fimbo nyembamba hadi moto unawaka. Tokea hapo vimekuja viberiti, makaa, mafuta, gesi hadi umeme kwa ajili ya nishati ya kupikia, kuongeza joto, kuyeyusha chuma, kuendeshea mitambo, nk.

Ninapoandika makala haya natumia teknolojia ya mawasiliano. Niko kwenye kompyuta (mpakato), siandiki kwa kutumia kalamu ya wino na mkono, bali natumia puku (mouse) na kicharazio (keyboard) cha kompyuta huku maandishi yakijitokeza kwenye kioo cha kompyuta (monitor/screen). Baada ya kumaliza tu kuandika nitatuma mara moja kwenda gazeti la Mwelekeo kupitia anuani ya baruapepe yao (email address). Kutuma na kumfikia mhariri wa gazeti la Mwelekeo ni ndani ya dakika moja.

Zamani ningetakiwa kwanza niandike barua kwa mkono, kisha ninunue bahasha na stempu. Ningekwenda kutuma Tukuyu kwa njia ya posta umbali wa kilomita 35 tokea Mwakaleli ninakoishi. Ingenichukua takribani siku nzima kwenda na kurudi, yaani saa 24 ambazo ni sawa na dakika 1440. Badala ya kutumia dakika 1440 kwa kutuma tu makala, siku hizi natumia dakika 1 tu! Aidha, kuna rafiki yangu aliyekuwa kambi ya jeshi JKT Mlale mkoani Ruvuma ambako ujumbe wa kifo cha kaka yake kilichotokea Tanga ulichukua miezi 6 kumfikia, na akafika kwao kwa kusafiri juma zima. Alikuta kaburi limedidimia na kuota msitu wa nyasi!

Enzi za ukoloni babu yangu mkubwa katika ukoo wa Mwakatobe, hayati Lebhi Mwakaaje, inasemekana aliwahi kufanya uchuuzi wa viungo (spices) kati ya Suma (wilayani Rungwe) na Zanzibar. Mahali alipokuwa akifikia hadi sasa huitwa “Mwakiji” baada ya wenyeji kutamka jina lake hivyo, badala ya Mwakaaje. Kwenda na kurudi ilikuwa inamchukua miezi miwili. Siku hizi baada ya kuwepo usafiri wa ndege uwanja wa kimataifa wa Songwe na boti za kisasa kati ya Dar es Salaam na Zanzibar, inachukua saa 4 kwenda Zanzibar na kurudi mkoani Mbeya, badala ya kutumia miezi mwili.

Kabla na wakati wa mwanzo wa ukoloni, safari ya kutoka Dodoma kwenda Tanga ilikuwa inachukua juma zima kupitia Dar es Salaam, Unguja, Pemba kisha mnavuka bahari kwenda Tanga. Njia fupi ya sasa kupitia Chalinze na Segera haikuwepo. Vivyo hivyo, kupiga simu tulikuwa tunakwenda makao makuu ya wilaya au mkoa kupanga foleni kwenye simu za kukoroga. Kama ndugu zako wako vijijini, ujumbe wako utapelekwa makao makuu ya wilaya waliko na kuchukua takribani mwezi mzima kuwafikia. Sasa tunawasiliana kwa simu za mkononi mahali popote, muda huohuo, bila kujali umbali. Hakika tumetoka mbali na sasa teknolojia imeifanya dunia kama kijiji!

Mchango wa teknolojia ni mkubwa mno katika maisha yetu. Kazi nyingi (si zote) tufanyazo hatutumii viungo vyetu kama mikono na miguu. Tunatibiwa, tunasafiri, tunajenga, tunawasiliana, tunashona, tunaelimishwa, tunafanya biashara, tunapima muda, tunajilinda, nk.; kwa urahisi zaidi kwa kutumia teknolojia. Teknolojia imeleta madadiliko mengi na makubwa katika nyanja mbalimbali za maisha yetu. Mashine na vifaa vya kila aina na sampuli hutumika kuzalisha huduma na bidhaa kwa urahisi, kwa wingi, kwa uhakika, kwa haraka, kwa ubora, kwa faida kubwa na kwa muda mfupi.

Teknolojia ni nini hasa? Ni neno la Kiswahili tulilotohoa kutoka neno la Kiingereza la “Technology.” Technology nalo ni maneno ya Kigiriki ya “Techne” likimaanisha ufundi au ujuzi, na “logos” lenye maana ya elimu au maarifa. Kwahiyo kwa ufupi, teknolojia ni maarifa ya kisayansi ya kufanyia kazi kwa kutumia nyenzo au vifaa kwa urahisi, kwa tija na kwa ufanisi.

Sasa tunaishi katika kizazi cha ukuaji wa teknolojia kwa kasi ya ajabu. Mtu ambaye alifariki kabla ya kugunduliwa simu za mkononi, tuseme kwetu sisi kuanzia miaka ya 1990 na kurudi nyuma; endapo atafufuka ghafla hawezi kuamini tunavyowasiliana na watu wa mbali kwa vipande vidogo kama vipande vya sabuni.  Ataona kama hirizi vile au uchawi wa aina fulani.

Hata hivyo, kuna malalamiko kwamba teknolojia inatulemaza na kuchukua ajira au kazi ambazo watu tungepaswa kufanya kwa mikono yetu. Wengine wanasema teknolojia ya mawasiliano haijafanya dunia kuwa kama kijiji, eti kwasababu inatufanya tusiongee sisi kwa sisi kwa kuwa kila mtu anatingwa na simu yake ya mkononi. Tunaonywa kuwa endapo kila kitu tutatumia teknolojia kama maroboti, basi watu tutabaki kama midoli na kukosa ajira.

Wengine wanahofia kwamba hata mpira utakuwa unachezwa na midoli kwenye kompyuta! Pamoja na hayo, bado mtu atabakia kuwa bora kuliko teknolojia kwa kuwa ndiye anayegundua na kuendesha. Kompyuta au simu haiwezi kuwa na akili zaidi ya mtu aliyeitengeneza. Na kwa kusema hivyo, kamwe tusiache kuifanyisha kazi na mazoezi miili yetu ili afya na akili zetu  ziendelee kuimarika. Tuitumie teknolojia kutuendeleza na si kutulemaza.

Hitimisho

Pamoja na kuwa na nguzo zingine za mitaji ya kutufanikisha kimaisha tulizozijadili huko nyuma, yaani afya njema, fikra pevu, vipaji, rasilimali asilia na maarifa na elimu; tunahitaji sana teknolojia kwa ajili ya kuongeza tija, ubora na uwingi wa huduma na bidhaa zetu. Tulipokuwa tunaanza kuvutia wawekezaji toka nje, hususan kwenye sekta ya madini, tulitoa sababu za kutokuwa na teknolojia ya kuchimbia na kuchenjulia makinikia.

Hata hivyo, teknolojia hii ipo, inauzwa na tunao uwezo wa kununua na kuchenjua madini yetu wenyewe. Tusitafute wawekezaji na misaada toka nje, bali tutafute teknolojia ya kuzichakata, kuzisindika na kuziongezea thamani rasilimali zetu asilia. Huko China, Japan, Korea Kusini, Malaysia, Singapore, Afrika Kusini, Brazil, na nchi zingine zilizoendelea na/au zinazoendelea; hawatafuti wawekezaji na misaada, bali hutafuta kwanza teknolojia ya kuendeleza wao wenyewe nchi zao. Tusiombe kitoweo cha samaki bali tutafute teknolojia ya kuvua samaki wenyewe.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwandumi Gwappo A. Mwakatobe, mchambuzi huru wa masuala ya kitaifa na kimataifa anayeishi Mwakaleli, Mbeya. Anapatikana kwa anuani ya baruapepe: gwandumi@hotmail.com au gwappomwakatobe@gmail.com

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.