Anayemuamini Profesa Lipumba anajidharau

ANAITWA Ibrahim Haruna Lipumba. Ni mwanasiasa. Kupitia kazi hii adhimu ya siasa, anajulikana vema kuwa mmoja wa wagombea maarufu wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu siasa za vyama vingi ziliporudishwa katika jamhuri mwaka 1992.

Amegombea nafasi hiyo mara nne – 1995, 2000, 2005 na 2010. Na mara zote akiwa ameteuliwa na Chama cha Wananchi kinachojulikana pia kwa jina la Civic United Front (CUF).

Jina lake linatangulizwa na neno “profesa” ikiwa na maana “akistahili” kuitwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba. Neno profesa, linalobeba herufi saba, linawasilisha wasifu wa mtu mwenye kiwango cha juu mwisho kielimu.

Profesa ni neno linalotumika kumtambulisha mtu aliyebobea katika masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya mwanadamu.

Huyu Ibrahim Haruna Lipumba ni profesa wa masuala ya uchumi, fani ambayo umuhimu wake unajieleza bayana. Uchumi ni suala lenye mfungamano hasa na maisha ya kila siku ya mwananchi. Inasemwa na wajuzi kuwa uchumi ndio sekta kiongozi katika kumjenga mwanadamu.

Na Jabir Idrissa

Profesa Lipumba ni msomi. Kazi zake zikipigiwa mfano kwa namna zilivyoashiria kuelezea tatizo fulani linalogusa utaratibu wa kumpatia mwanadamu maendeleo. Anajadili tatizo na hatimaye kutoa ufumbuzi.

Isitoshe, profesa Lipumba anatajika mpaka viunga vya kiutendaji vya Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na asasi za kilimwengu zinazohusu jukumu la kutoa utaalamu wa ushauri katika uendeshaji sera za kifedha na uchumi kwa ujumla wake.

Asasi kama Benki ya Dunia au World Bank (WB) na Shirika la Kimataifa la Fedha liitwalo kwa Kiingereza the International Monetary Fund (IMF) anafahamika kwa kazi za kisomi. Ndio kusema kuwa mtu atendae kazi mpaka zikavuta akili za wanataasisi hizo, huwa anatambuliwa kama mtaalamu au gwiji muhimu wa eneo fulani.

Kutokana na ukweli huo, Profesa Lipumba, nataka kuamini, hakuhangaika kupenya kuwa mwanasiasa, kama ni kweli alitamani mwenyewe kuwa.

Hwenda hadhi hiyo ya usomi wa kiwango cha juu ndiyo ilipenya ndani kabisa mwa fikra za viongozi wakuu wa CUF hata kukubali rai ya “rafiki wema” waliopenda akubaliwe kuwa mgombea urais wakati wa uchaguzi mkuu wa 1995.

Simulizi zinasema hao rafiki wema walipeleka rai yao baada ya kupata khabari kuwa uongozi wa CUF unahangaika kupata au haujapata mtu wa kumpa kijiti ili kuwakilisha chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais nchini akipambanishwa na wanasiasa magwiji.

Hadhi na yanayotokea

Inawezekana viongozi wa CUF wanajuta. Kwa viongozi hao waliokuwa pia waasisi wa chama na hasa fukuto la siasa za mageuzi, na yumkini hata wale niliowaita “rafiki wema” kuwa katika majuto kipindi hiki, ni tafsiri halisi ya ninachothubutu kuita “kupotea kwa hadhi ya kisomi ya profesa Lipumba.” Ukitia tamati kunisoma, amua kunibishia kuwa angali msomi mkubwa na mtaalamu mbobezi wa uchumi.

Angalia anavotajika kwa mwaka sasa. Baada ya kukosa urais Oktoba 1995, akichukua nafasi ya tatu nyuma ya Benjamin Mkapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Augustine Mrema wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alivikwa uenyekiti CUF.

Alifanikiwa kukisaidia chama kuimarika. Kilienea nchini na kuvuna ufuasi mkubwa. Kufikia Oktoba 2010, CUF kilikuwa na nguvu kubwa. Kikichukuliwa kama chama tishio zaidi kwa CCM.

Leo, CUF ilipo, imeongeza idadi ya wabunge wa majimbo. Haijapata kutokea katika historia yake kuwa na wabunge wengi Bara. Mazoea ni wawili tu. Awali Kigamboni na Bukoba. Ikaja Kilwa na Kigamboni. Ikaja Kilwa na Lindi mjini. Basi.

Leo inao Kilwa Kusini, Kilwa Kaskazini, Mchinga, Tandahimba, Mtwara Mjini, Temeke, Kinondoni na Kaliua. Kina madiwani wengi haijatokea. CUF leo inashika halmashauri kadhaa.

Mafanikio haya yamempita profesa Lipumba. Yalimpitaje? Alijiuzulu kwa hiari tarehe 5 Agosti 2015, miezi miwili kabla ya upigajikura. Tena, alijiuzulu hata baada ya kunasihiwa na uongozi pamoja na wazee wa CUF. Alipoamua, akatokomea. Punde akaonekana kwa picha alizopiga Rwanda ‘akila bata.’

CUF imepata mafanikio kwa ushirikiano na vyama vitatu katika umoja wa vyama vya upinzani vilivyoamua kushirikiana – Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Ni National League for Democracy (NLD), NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Profesa Lipumba labda hakupenda mafanikio ya CUF asiyoyachangia. Si aliyakimbia alipotelekeza chama? Alas, baada ya miezi kumi anarudi na akitaka kukalia kiti kilekile alichokiachia kwa jeuri na pupa.

Akijua chama kilishapata mbadala wa nafasi yake, akajitoma kwenye mkutano mkuu wa dharura wa kuchagua mwenyekiti. Hakualikwa rasmi, bali anasema “baadhi ya wanachama wameniita.”

Aliingia ukumbini Ubongo Plaza akilindwa na maofisa wa polisi waliobeba silaha. Amesahau Polisi walimbeba juujuu na kumvunja mkono uwanjani Mbagala Zakhem akikisakia chama kura mwaka 2005.

Ni Polisi haohao walimpiga na kumdhalilisha kwa kumsukuma kikatili alipokuwa Mtoni kwa Azizi Ali, njiani kwenda kuzuia wanachama waliokusanyika Mbagala Januari 2015. Leo wanamhifadhi asidhuriwe na wanachama wa CUF.

Wamemsindikiza kukalia ofisi kuu za Buguruni. Hatua hiyo ilifanikiwa baada ya walinzi wake kushambulia walinzi wa chama waliokuwa getini. Wakampiga mlinzi aliyeshika silaha. Wakavunja milango na kuingia ofisini.

Mpaka sasa profesa anaendesha harakati za “kuimarisha” chama hapo, huku akimlaumu Katibu Mkuu Maalim Seif kuwa ni mtoro kazini. Lakini anajua makao makuu ya chama ni Mtendeni, mjini Zanzibar. Anajua Maalim Seif yuko kule bukheri khamsa ishirini anafanyakazi.

Profesa Lipumba akatangaza kumsimamisha katibu mkuu. Akamteua Magdalena Sakaya, aliyekuwa naibu katibu mkuu Bara, kumkaimu Maalim Seif. Profesa anajua hana mamlaka ya kufanya hivyo maana hana vyombo halali vya kikatiba vya kumwezesha kubadilisha chochote.

Anajua kwa sababu ya ukorofi wake dhidi ya chama, aliitwa akikabiliwa na mashitaka, na aliposusa kikao, akavuliwa uanachama. Hii ni 26 Septemba, siku mbili tangu alipoingia kwa nguvu Buguruni akisaidiawa na Polisi. Anajua alikatia rufaa uamuzi huo kwenye mkutano mkuu.

Hivi unamuamini Profesa Lipumba leo? Unadhani ndiye yuleyule aliyejenga CUF hadi kuitwa “ngunguri” na Polisi namba moja, Omar Mahita? CUF ile iliyobuni kaulimbiu ya “Jino kwa jino?”

Kwa hivyo unaamini khasa Profesa Lipumba anaimarisha chama? Wakati ule hapakuwa na kesi CUF. Leo muimarishaji wa chama anaona fakhari wana-CUF kushitakiana katika kesi 14. Bado ungali unaamini yungali msomi mbobezi wa uchumi?

Umesoma lini makala zake za uchambuzi wa hali ya uchumi Tanzania na Afrika au nchi zinazoendelea? Alikuwa hashindi wiki anazo angalau mbili. Leo kaputi. Atapata wapi nafasi wakati anasikiliza vitoto vilivyoishia darasa la saba. Bado ni profesa yule? Mjinga mie naona amebadilika sana. Unayemuamini najua unajidharau bure!

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la MwanaHalisi la tarehe 14 Julai 2017.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.