Uhuru Kenyatta na maafisa wa IEBC waondolewe

Siwezi kuacha asilani masuala ya uchaguzi wa Kenya yanipite bila kutoa maoni yoyote yale. Chaguzi zote za nyuma pia nilitoa maoni na ushauri kupitia vyombo vya habari. Tunakumbuka kuwa siku ya Ijumaa Septemba 1, 2017 ilikuwa ni shangwe Afrika nzima. Ni siku ambayo Kenya na Afrika iliishtua dunia ya wastaarabu na wapenda haki, amani na demokrasia.

Vyombo vya habari vikubwa duniani vilirusha habari ya dharura au habari ya hivi punde (breaking news) kutoka Kenya. Ilikuwa siku ya ushindi mkubwa na wa kihistoria kwa Kenya na Afrika. Hata Uhuru Kenyatta ambaye ushindi wake ulibatilishwa aliheshimu maamuzi ya mahakama japo hakukubaliana nayo. Na akaahidi yuko tayari kwenda kupiga debe upya.

Sambamba na hilo, dunia nzima iliwapongeza majaji wa Kenya wakiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga kwa kuonesha ukomavu na ujasiri wa kutenda na kutoa haki. Binafsi nilifurahi mno kwa maamuzi ya majaji. Si kwamba napendelea yeyote kati ya wagombea wanane waliojitokeza, kama ambavyo akina Edward Lowassa walivyofanya. Na naelewa hakuna tatizo kumpenda mgombea yeyote, lakini utashi wangu unapenda ushindi wa kidemokrasia na wa haki kwa yeyote, awe Mohammed Abduba Dida au Dkt Ekuru Aukot.

Ilipofika Jumamosi ya Septemba 2, 2017, kwa kutumia ulimi uleule na kinywa kilekile, Uhuru Kenyatta aliporomosha matusi mazito kwa majaji na kuahidi kuifumua upya na kuirekebisha mahakama endapo atashinda uchaguzi wa marudio; tofauti kabisa na aliposema anaheshimu maamuzi ya majaji. Akawaita majaji wakora! Akaapa, ninanukuu “…watano au wasita…” eti hawezi kuamua nani awe rais kwa niaba ya Wakenya milioni 40.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba majaji hawakuamua nani awe rais. Na wala hawakusema Uhuru alichakachua matokeo. Ni tume (IEBC) iliyochakachua matokeo ya urais. Kwahiyo majaji wakaamua uchaguzi urudiwe kwa kuwa haipendezi hata kwa Uhuru mwenyewe kupata kura haramu kwa mitambo ya kompyuta. Inabidi apate kura halali miongoni mwa Wakenya milioni 40.

Dosari za Wazi za IEBC na Makosa ya Uhuru Kenyatta

Kuna watu wanauliza kwanini uchaguzi wa urais umepatikana na dosari wakati waangalizi wa kitaifa na kimataifa walisema ulikuwa huru, wa haki na wa uwazi? Nifafanue kwa ufupi kuwa kazi ya waangalizi ni kufuatilia uhalali wa mchakato wa uchaguzi kabla na wakati wa kupiga kura. Hawahusiki kabisa kuhesabu kura. Wapiga kura wakimaliza zoezi la kupiga kura unakuwa ndio mwisho wa kazi ya waangalizi. Kuhesabu kura ni kazi ya maafisa wa tume, mawakala wa vyama vya siasa na/au wagombea binafsi.

Badala ya kuhesabu kura kwa kutumia kompyuta na fomu 34a na 34b kwa pamoja, IEBC ikaamua kupeperusha tu matokeo kwa kompyuta pasipo kuambatisha fomu husika. Haikuzingatia matakwa ya kikatiba, kisheria na kikanuni. Lakini kumbe baadhi ya maafisa wa IEBC walianza kuchakachua hesabu. Kisheria mshindi wa uchaguzi hana budi kutokana na utashi na uwingi wa wapiga kura, na si kutokana na utashi wa  wanaohesabu kura.

Katika anga za kimataifa nimewahi kusema, najinukuu: “What counts in authoritarian regimes is not who cast votes, but who count votes.” Nikimaanisha kuwa kinachojalisha katika tawala za kiimla si wanaopiga kura, bali wanaozihesabu. Hao ndio humweka mshindi wamtakaye wao!

Nchi nyingi (si zote) za kidikteta Afrika, na hata nje ya Afrika, watawala dhalimu hujigamba eti mshindi hapatikani kwa vijikaratasi vya kura. Labda niweke wazi hapa, kura si karatasi tu, bali ni sauti ya maamuzi ya mpiga kura. Kuidharau sauti hii kupitia karatasi ya kura ni kuinajisi demokrasia na ni kuyanajisi maamuzi ya kidemokrasia. Ndicho walichokifanya IEBC.

Kabla hata kampeni za uchaguzi wa marudio hazijaanza rasmi, tayari IEBC imeanza kwa dosari kubwa. Kimakosa imetangaza marudio ya uchaguzi yawe Oktoba 17, 2017 kwa wagombea wawili tu, Raila Amalo Odinga na Uhuru Muigai Kenyatta, badala ya wagombea wote wanane. Baada ya kugundua dosari kadhaa (irregularities and illegalities), majaji waliamua uchaguzi wa urais urudiwe kwa kuwa ulikuwa batili (null and void).

Majaji hawakusema wagombea wawili warudie uchaguzi, la hasha! Walisema utaratibu wa kuhesabu kura za urais ulikiukwa kinyume na katiba na kwahiyo ni batili na usiofaa. Wagombea urais walikuwa wanane, IEBC wanapaswa wasikilize tena na tena hukumu ndiposa watangaze tarehe mpya ya uchaguzi kwa wagombea wote. Mimi si Mkenya, ni Mtanzania, lakini ninayewapenda jirani zetu na kuwakumbusha sheria, kanuni na taratibu walizojiwekea wenyewe. Ninawaombea Mungu awaongoze na kuwalinda!

Kama nilivyotangulia kusema hapo juu, Uhuru Muigai Kenyatta kaichukia vibaya sana mahakama ya juu kufuta upuuzi wa tume, anaitetea tume iliyochakachua matokeo ya urais. Naelewa kuchanganyikiwa kwake, lakini mwenye hekima na ambaye ni rais angependekeza, japo kwa kuzuga, irekebishwe tume, si mahakama. Je, mbona 2013 hakuirekebisha mahakama iliyomthibitisha? Je, anadhihirisha aliungana na tume kuvuruga hesabu?

Kwa elimu yao majaji, hadhi yao, umri wao (na kuwa na familia), na uaminifu wao katika kutenda na kutoa haki, ni kuwadhalilisha na kuwafedhehesha kwa kuwaita wakora (crooks). Wakora ni majambazi, wahuni, walaghai na vibaka wa mitaani. Ni wahalifu! Kama anaona wanasheria ni vibaka, je atairekebisha mahakama kwa kuwaweka nani mbadala? Wafanyabiashara? Munguki? Kabila lake? Mbona si fani yao?!

Ikumbukwe kuwa tangu uhuru, Kenya imetawaliwa na marais wanne toka makabila mawili tu, watatu wakikuyu na mmoja mkalenjin. Muungano wa Jubilee sehemu kubwa ni wakikuyu na wakalenjin. Labda Kenyatta anataka hata mahakama iwe makabila mawili tu: Kikuyu na Kalenjin. Ubaguzi wa kikabila unawatesa sana Wakenya, hatutaki mahakama iwe ya kikabila.

Aidha, nisisitize kuwa mahakama ndio itakuwa mshindi katika uchaguzi wa marudio, si mgombea mmoja. Nasema hivyo kwa kuwa mahakama imeushinda udhalimu. Mgombea atakayepata kura nyingi auweke wakfu (dedicate) ushindi wake kwa mahakama na majaji waliotenda na kutoa haki.

Naam, safari hii hatutaki tena tume itutoneshe kidonda na machungu ya mauaji ya kikatili ya Chris Musando aliyesimama kidete kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atakayedukua (hack) utaratibu wa kuhesabu kura kwa kuwa ana nywila (password) kwenye kiganja chake. Kama vile kumkomoa kwa usemi wake huo, wauaji walikikata kiganja chake na kuitupa maiti yake vichakani! Mpaka sasa kuko kimya, hatujui kama upelelezi unaendelea au kama kuna yeyote aliyakamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

Uhuru Kenyatta kajikosesha sifa

Kwa kuwatukana majaji na kuahidi kuivunjilia mbali mahakama, Uhuru Kenyatta amejifutia sifa ya kugombea uchaguzi wa marudio. Aidha, kwa tume kufanya makosa mengine kabla hata uchaguzi haujarudiwa, imejiondolea uhalali wa kusimamia uchaguzi wa marudio. Kwahiyo, natoa wito wa kumfuta Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa marudio kwa kukosa sifa za kuwa mgombea, hususan kwa kutishia kuuvunja mhimili wa dola wa kutoa haki uliopo kikatiba na wenye nguvu sawa na serikali na bunge.

Mtu aliyeitukana mahakama, aliyeitukana haki, aliyeutukana utawala na uongozi bora, hapaswi kugombea nafasi yoyote. Mtu aliyewafananisha wanasheria na wakora hafai kuwa rais wa Kenya na nchi yoyote ile ya kidemokrasia. Hawafai Wakenya na Waafrika wote. Amejitia aibu, amewatia aibu Wakenya, amewadhalilisha wanasheria wa Kenya na nje ya Kenya, na katutia aibu sisi Waafrika na Afrika yote.

Matusi kwa mhimili wa mahakama kutoka kwa mtu mwenye hadhi ya rais hakuwezi kuvumilika. Aende kuiendeleza ardhi ya maelfu ya hekta ambayo Baba yake Jomo Kenyatta aliichukua kwa uroho na ubinafsi na kuwaacha Wakenya wengi wakiwa hawana pa kuchungia ng’ombe, kulima na kuishi. La sivyo asubiri rungu la kufutiwa vibali vya kumiliki ardhi toka kwa mtu kama John Pombe Magufuli, endapo atokea Kenya.

Natoa wito kwa majaji wote 7 waliohusika kutoa maamuzi, wamshitaki Uhuru Kenyatta kwa kuwadhalilisha na kuidhalilisha mahakama. Aidha achakuliwe hatua kali za kutishia kuifumua na kuivunjilia mbali mahakama, mhimili unaojitgemea kama ilivyo serikali na bunge. Amevunja katiba aliyoapa kuilinda. Kama ana japo chembe ndogo tu ya uungwana, ajiuzulu urais na ukaimiwe na mwingine hadi rais mwingine apatikane.

Natoa wito kwa wajumbe na maafisa wote wa tume na Mwenyekiti wao Wafula Chebukati wajiuzulu mara moja, au la wafukuzwe kazi endapo hawatajiuzulu wenyewe kwa hiari. Hawafai kuendesha uchaguzi kwa kuanza kuwabagua wagombea kinyume na katiba ya Kenya na tume yenyewe iliyowapitisha. Wasipewe nafasi nyingine ya uharibifu.

Nihitimishe kwa kutoa wito kwa wagombea wote wanane, viongozi wa asasi za kijamii (pamoja na dini), wanasheria (hususan LSK), na viongozi wa vyama vya siasa; wakae kujadili dosari zilizojitokeza na namna bora ya kuziondoa. Wapate mwafaka na maridhiano ya kuendesha uchaguzi wa marudio unaokubalika pande zote kikatiba, kisheria na kikanuni. Kisha wateue wajumbe na maafisa wapya wa tume mpya wanaoaminiwa na wote.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwandumi Gwappo A. Mwakatobe, mchambuzi huru wa masuala ya kitaifa na kimataifa, anayeishi Mwakaleli, Busokelo, Rungwe, Mbeya. Anapatikana kwa anuani ya baruapepe: gwandumi@hotmail.com au gwappomwakatobe@gmail.com

 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.