Miezi 10 bila Ben Saanane

Miezi 10 sasa tangu Ben Saanane apotee. Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG) tumeshirikiana na vyombo vya dola, taasisi na mashirika ya kiraia katika juhudi za kumtafuta. Tumetoa ushirikiano wote kwa jeshi la polisi na mamlaka zingine za nchi. Katika vikao vyetu na vyombo vya dola, tulieleza mashaka yetu na tukahitaji wayafanyie kazi ili kuyasahihisha.

Walituhakikishia kuwa wangeshughulika na kila njia ambayo ingeweza kuleta taarifa ya Ben alipo. Lakini miezi 10 sasa, mashaka yapo pale pale. Vyombo vya dola vimeshindwa kusahihisha hata mashaka madogo tu, kwa mfano mtu aliyempigia simu ya vitisho Ben.

Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TRA) walitoa mawasiliano ya Ben ikiwa ni pamoja na watu waliokua wakimtisha. Polisi wakaahidi kufuatilia na kubaini watu hao. Sasa ni miezi 10 polisi WAMESHINDWA kuwakamata watu hao. Wameshindwa hata kuwabaini tu kwamba ni akina nani wakati wamepewa mawasiliano yote na TCRA.

Hiki ni kielelezo kwamba vyombo vyetu vya ndani vimeshindwa kumtafuta Ben. Mara ya mwisho tumeenda makao makuu ya polisi, taarifa tuliyopewa ni kwamba bado wanaendelea na uchunguzi. Miezi 10 ya uchunguzi wameshindwa hata kujua waliokua wanamtisha Ben wakati namba wamepewa na TCRA? Uchunguzi gani huu?

Siingilii kazi za polisi, lakini inawezekanaje uchunguzi wa mtu anayekashifu serikali unatumia siku moja ameshakamatwa, lakini mtu aliyemtishia Ben maisha unatumia miezi 10 na bado wameshindwa kumpata?

Na hili ni moja dogo. Yapo mengi makubwa kuhusu Ben ambayo polisi waliahidi kuyachunguza. Lakini kama hili dogo limewashinda, hayo mengine itakuaje?

Tunalipenda jeshi letu la polisi, tunaliheshimu, lakini tunadhani wamefikia kiwango chao cha mwisho cha uchunguzi. Hawawezi tena. Tunawasiliana na wenzetu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ili kuomba serikali iruhusu wachunguzi wa kimataifa.

Tuliomba waangalizi kutoka Umoja wa Mataifa ataifa na wakaonesha hamu ya kusaidia, lakini serikali ikatuambia tusubiri kwanza polisi wamalize uchunguzi wao, kama wakishindwa ndipo tufikirie wachunguzi kutoka nje. Serikali ilituhakikishia tuendelee kuwa na IMANI na jeshi la polisi.

Ni kweli tuna imani na polisi lakini tunadhani uwezo wao ni mdogo kuchunguza suala la Ben. Tutawaomba waweze kutangaza kwamba wameshindwa, ili tupate uhalali wa kuomba wachunguzi wa kimataifa. #BringBackBenAlive!


Imeandikwa na Malisa Godlisten katika mtandao wa Facebook tarehe 12 Septemba 2017.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.