Profesa atatulia akitimiza anachotakiwa

MSOMAJI wa MwanaHALISI, na hasa safu hii, amenijia. Kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, akitumia Na. +255623248721, anasema, “… kwa kuwa CUF walitoa mwanya, yeye ameutumia kujirudisha kwenye kiti… sasa wamsikilize tu maana ameshika mpini.”

Huyu msomaji anajibu nilichokiandika katika toleo la gazeti hili, Na. 404, nilipojadili kinachoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), na hasa mgogoro aliousababisha Profesa Ibrahim Lipumba, aliyejirudisha uongozini na kushikilia kiti cha mwenyekiti ilhali alijiuzulu mwenyewe kwa tamko la hadharani.

Msomaji hakufafanua mwanya ambao CUF waliuacha ambao Profesa Lipumba aliutumia kutaka kurudi kwenye kiti miezi kumi baada ya kujiuzulu kwa hiari yake akisema nafsi yake inamsuta kuendelea kukiongoza chama hicho.

Hata hivyo, namsoma msomaji kuwa anazungumzia kile kinachotajwa na wengi kuwa eti chama, baada ya tamko la profesa kujiuzulu ambalo alilitoa tarehe 5 Agosti 2015, kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Peacock, Mnazimmoja, Dar es Salaam, hakikuitisha mkutano ili kujadili uamuzi huo.

Tangu awali, mtizamo wangu uliniaminisha kusema kwa akili ya kawaida, kilichopaswa kufanywa wala sio kujadili kujiuzulu kwa mwenyekiti. Msingi ni kuwa hakuomba kujiuzulu, alijiuzulu. Alijiuzulu kwa tamko la maneno, na akafanya hivyo kwa barua rasmi aliyokiandikia chama kupitia Katibu Mkuu.

Tena kwa kweli, Profesa Lipumba alijiuzulu huku akipuuza mashauri na nasaha za watu mbalimbali katika chama – makundi ya wanawake, wazee na vijana – waliomfikia na kumsihi aahirishe uamuzi wake angalau kwa wakati ule.

Katika pitapita zangu hivi karibuni, nilikutana na mmoja wa viongozi wa Kiislam inayomiliki shule ya msingi na sekondari, akinieleza kuwa alikuwa mmoja wa viongozi wa kidini “waliomsihi sana” profesa asijiuzulu.

Alinambia aliongoza kundi la maulamaa wenzake na vijana wa Kiislam wanaokiamini chama hicho, na kumsihi kuakhirisha kujiuzulu ili angalau asubiri uchaguzi wa rais, wabunge, wawakilishi na madiwani upite. Huko mbele angefikiriwa kuchukua hatua hiyo.

“Niliongoza wenzangu tukaenda Buguruni. Tulipokutana naye, nikamweleza tumefika kumuomba asijiuzulu kwa sasa… baada ya muda kidogo wa kuanza kutoa maelezo, nilijikuta nalia machozi kwa huzuni. Fikiria mtu mzima na familia yangu ninalia hadharani nikimsihi.

“Nilipopata nguvu nikamwambia, Profesa, hivi unavoniona ndivyo walivyo wenzangu hawa niliofuatana nao kuja kukuona hapa, na hata jamii kwa upana wake kabisa imeguswa na kushtushwa na habari hizi. Sasa tunakunasihi sana subiri kwanza uchaguzi upite.”

Hii ni ile siku ambayo profesa alihanikiza uwanja mzima kwenye ofisi kuu za CUF Buguruni, baada ya kusikika taarifa za nia yake hiyo. Siku hiyo ya tarehe 4 Agosti 2015, gazeti la Uhuru linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasimu mkubwa wa kisiasa wa CUF, lilikuwa limechapisha habari iliyopewa uzito mkubwa kuwa Lipumba amejiuzulu uenyekiti CUF.

Katika habari hiyo, kulikuwa na kauli ya Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad kuwa hakuwa na taarifa hizo, na kwamba kwa nafasi yake ya kuwa dhamana wa mbele wa chama hicho, anahisabu Profesa angali mwenyekiti CUF.

Profesa Lipumba akionesha kusikia kilio cha viongozi wenzake, ambao pia walimsihi asitishe nia yake hiyo mpaka chama kimalize shughuli za uchaguzi mkuu, wanachama wenzake na wapenzi wa chama, aliondoka Buguruni na kurejea nyumbani kwake.

Kumbe aliwaridhia wote wale kwa shingo upande. Moyoni mwake na kama alivyosema hadharani, dhamira yake inamsuta kubakia kiongozi, alipoamka tu siku iliyofuata, tarehe 5 Agosti, alifukuzia hotelini Peacock, na kutangaza kuwa amejiuzulu.

Ni muhimu ieleweke hapa, profesa huyu wa uchumi, hakutangaza nia. Hakusema anaomba chama kimruhusu ajiuzulu. Alisema “nimeamua kujiuzulu nafasi ya mwenyekiti wa CUF na nitabakia mwanachama ambaye nimelipia kadi yangu….”

Hivi baada ya hapo, uongozi ufanye nini? Ndipo ukaitisha haraka kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT). Baraza likateua wanachama watatu wa kushika majukumu ya mwenyekiti aliyekiacha kiti.

Baraza hilo ambalo ilielezwa kuwa lilikasimiwa mamlaka ya Mkutano Mkuu wa Chama, lilimteua wakili maarufu nchini, Twaha Taslima, kuongoza iliyoitwa Kamati ya Uongozi ya Taifa. Wajumbe wenzake ni Aboubakar Khamis Bakary, mwakilishi wa Mgogoni, Pemba, na Severine Mwijage, mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Kagera.

Hapana shaka, uongozi uliona hiyo ndiyo hatua muafaka inayozingatia katiba ya chama. Haionekani hii inayosemwa na wanaomtii profesa kuwa kulipaswa kuitishwa mkutano mkuu ili kuridhia. Kwa CUF, katika kipindi kile, dharura ilikuwa kushughulikia mipango ya uchaguzi mkuu wa taifa, na wala sio kushughulika na mtu aliyejiuzulu mwenyewe.

Hata akili ya kawaida, inakubali kuwa kwa vile alichokifanya profesa ni kujiuzulu, na sio kuomba kujiuzulu, la muhimu ni kujaza nafasi yake. Si tumeona namna alivyoshawishiwa asijiuzulu akapuuza; anayesema ilikuwa kushughulikia uamuzi wake kwa maana ya kuitisha mkutano mkuu wa kuridhia, anataka kuonesha anavyodharau akili za viongozi wote aliowaacha profesa.

Baraza Kuu lina nguvu za kutosha kufanya maamuzi. Na kwa kuwa ndio chombo cha kuweza kukutana kwa dharura kuliko mkutano mkuu unaohitaji maandalizi na raslimali fedha, na kwa wakati ule chama kikikabiliwa na kibarua cha kushiriki uchaguzi wa taifa, uamuzi wa kuteua kamati ya kushika majukumu ya mwenyekiti, ni muafaka.

Si kweli kuwa palikuwa na mwanya wa profesa kurudi kitini. Ni aibu na fedheha kujirudisha uongozini baada ya kukaa nje kwa miezi kumi. Uamuzi aliouchukua haujapata kutokea penginepo popote.

Katika kuonesha msimamo imara kuhusu uamuzi wa chama kuteua kamati ya uongozi, tarehe 17 Juni 2016, mwenyekiti wa kamati, wakili Taslima, alitoa tamko kuhusu hatua ya profesa kulazimisha kurudi kwenye kiti kwa kuwa eti “hakujibiwa barua yake ya kufuta au kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu.”

Kwamba kulikuwa na sharti la kikatiba kuwa ajibiwe barua ya kujiuzulu, halipo kwenye katiba ya chama. Alijiuzulu anajibiwa nini hapo? Kuwa Mheshimiwa Profesa Lipumba umekubaliwa kujiuzulu?” Hilo halipo kwenye chama hicho, ndivyo uongozi unavyoshikilia.

Wakili Taslima alihoji: “Hivi madai ya kutojibiwa barua yake ya tarehe 5 Agosti aliyompelekea Katibu Mkuu, ndiyo msingi wa hoja yake ya kurudi katika nafasi ya uwenyekiti, hajui kwamba Mkutano Mkuu wa Taifa haukuhitajika kufanyika kwa ajili ya jambo hili?

Hivi wale wajumbe walioteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuunda Kamati ya Uongozi wanaenda wapi sasa baada ya yeye kuamua kujirudishia uongozi?

Hivi yeye Lipumba na Baraza Kuu nani mkubwa kimamlaka mpaka afikie hatua ya kutoheshimu uamuzi wa Baraza Kuu?

Profesa Lipumba hasa kwa uamuzi wake wa kujirudishia uenyekiti ametumia kipengele kipi cha Katiba ya chama hasa baada ya kuvitaja vipengele kadhaa vya Katiba katika Ibara ya 117?

Maswali haya tumeshindwa kuyajibu kwa ufasaha. Chama kinamuomba asijaribu kukiyumbisha chama kipindi hiki; Watanzania wanahitaji kuwekwa pamoja na kupewa matumaini ya namna gani matatizo yao yanaweza kutatuliwa.”

Ni kwa sababu hiyo, hata profesa Lipumba anapohangaika kutafuta suluhu haeleweki. Na sababu kubwa ni kwamba ameendelea kuchukua hatua za kukidhoofisha kuliko kukiimarisha chama. Ni tofauti na madai yake “ninakipenda chama hiki na tungemaliza mgogoro nje ya mahakama.”

Ukweli profesa anaogopa kesi mahakamani, zikiwemo zile alizotuma mawakili wazifungue. Anajua ataanguka. Si hivyo, angetulia akisubiri maamuzi. Hatulii maana anachotakiwa kukikamilisha kwa maslahi binafsi – kumtokomeza Maalim Seif – hajakifikia.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Jabir Idrissa na ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHALISI la tarehe 28 Agosti 2017.

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

1 Comment

  1. Mheshimiwa Lipumba alijiuzulu mwernyewe pale chama kilipo mchagua Mheshimiwa Lewasa kupigania urais wa Tanzania ilihali Tanzania nzima ilikuwa tayari kumchagua Lipumba kwa tiketi ya CUF kuwa rais wa Tanzania na kwa bahati mbaya sana Maalim Seif hakuliona hilo na kwa bahati mbaya zaid Lewasa akashindwa vibaya sana kwa kuwa hakuwa na sifa za manufaa kwa Tanzania.Hapo lilipo tokea hilo Mheshimiwa Lipumba akaliona kosa hilo, CUF italiona kosa lake na kujirekibisha,na yeye akaona heri auonde uamuzi wake kujiuzulu uana kiti wake wa CUF kabla hauja jadiliwa na kaqmati kuu. Jee hilo ni kosa? Yaliyo pita si ndwele ya gange yajayo.Jee Tanzania haina watu wazee kama vile Mheshimiwa Mzee Moyo wawezao kumkabili Maalim Seif na Mheshimiwa Lipumba wakaacha hasama zao kwa minajili ya kuiokoa CUF na jamii ya wafuasi wake?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.