Kama vile Dk. King, hata kifo kisingemuua Lissu

Nimefuatilia kwa makini mazungumzo yanayoendelea katika mitandao ya kijamii, magazeti ya nchini pamoja na vyombo vyenginevyo vyenye kutoa taarifa tangu siku ya tarehe 7 Septemba mwaka huu, baada ya Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Tundu Antipas Lissu, kupigwa risasi nje ya nyumba yake mjini Dodoma.

Kitendo hicho cha Lissu kupigwa risasi mchana kweupe, ndicho kilichoibua hisia kali za Watanzania. Hata kwa ambao kabla ya tukio hilo hawakuwa hata wakimtaja Lissu, baada ya kitendo hicho ndio wamekuwa wafuatiliaji wakubwa wa kutaka kujua Lissu ni nani, anafanya nini na kwa nini yakamkuta hayo yaliyomkuta.

Kwa wingi wa risasi zilizomiminwa katika shambulio hilo na kwa jumla ya risasi tano zilizothibitishwa kuzama mwilini mwa Lissu kwa mujibu madaktari wa Tanzania, kwa mtu mwepesi mwepesi aliye na wingi wa hofu na uchache wa ujasiri, hakukuwa na sababu ya kubakia hata kwa kutapia roho, bali angekufa kwa ule mlio wa risasi moja tu baada ya kufyatuliwa kutoka bunduki za hao wanaoitwa ‘Watu wasiojulikana’.

Na Ali Mohammed

Lakini kwa Lissu haikuwa hivyo. Alijihami kwa kufuata maelekezo ya dereva wake na hatimaye akatoka mzima ingawa si salama.

Sitaki niungane na watu wengine wanaotoa hukumu juu ya tukio hilo, lakini kwa hali inavyokwenda nchini tangu Lissu apigwe risasi mpaka leo, hakuna siku ipitayo kama Lissu hajatajwa. Wengi wao humtaja Lissu kutumia nafasi yake katika ulingo wa mapambano ya siasa.

Umaarufu wa Lissu baada ya kushambuliwa

Wengine hutumia kumtaja kupitia taaluma na ubobezi wake katika fani yake ya sheria na wengine humtaja na kumuita ni mtetezi wa haki za wanyonge wakihusisha mifano mbali mbali baada ya kusoma maandiko mbali mbali yanayoelezea kwamba kumbe mbali na yote hayo, Lissu pia ni mtetezi wa raia wote wa Tanzania kwa kupitia sekta ya madini.

Yote haya yamekuja mara tu baada ya Lissu kumiminiwa risasi. Kwamba baada ya tukio hilo, sio kwamba watu walisikitika kidogo na baadaye yakesha, lakini walisikitika na kisha wakataka kujuwa kwa nini Lissu apigwe risasi. Licha ya upelelezi wa kipolisi tunaoaminishwa kuwa unaendelea hadi leo bila ya taarifa za kina za matokeo na maendeleo ya upelelezi huo, lakini raia nao wanatumia nafasi zao kutaka kumjua Lissu kutoka utandu hadi ukoko. Hapo ndipo mambo mengi yanayomuhusu Lissu yakaenea kwa kasi kubwa sana katika jamii ya Tanzania.

Miongoni mwa hayo, ni kile kitabu chake kitabu kiitwacho ‘A Golden Opportunity? Justice & Respect in Mining’ cha mwaka 2008, alichoandika kwa ushirikiano na Mark Curtis. Kitabu hichi kinaonesha jinsi Tundu Lissu aliye mahututi kitandani hospitalini huko Nairobi, akiuguzwa na kutibiwa majeraha ya risasi za bunduki ya SMG, anavyoinuka na kusimama barabara na kupambana kitaalamu kupigania wananchi wa Tanzania juu ya suala zima la madini.

Huyo ndiye Lissu aliyejitoa muhanga, licha ya vitisho alivyovipata mara kadhaa kutoka kwa watu wasiojulikana na wanaojulikana si kwa maslahi binafsi yake binafsi, bali ni kwa kutetea haki za wananchi wanyonge wa kawaida, sambamba changamoto kedekede alizoipa serikali pamoja na wawekezaji wa madini kuacha ukatili, dhuluma na unyanyasaji dhidi ya wakaazi wanaozunguka au waishio katika maeneo zilipo rasilimali hizo za madini.

Je, kifo kingelizika jina la Lissu?

Kihistoria, duniani Lissu si mtu wa kwanza kuanzisha mapambano kuitetea na kuisimamia jamii yake katika kupata haki fulani au kulinda kitu fulani. Yako mataifa kadhaa yalikuwa na watu mfano wa Lissu. Kinyume chake pia, Lissu hatakuwa wa mwisho kwa Tanzania kujitolea kufanya hivyo. Watakuja wengi mfano wa Lissu na zaidi ya Lissu watakaosimama kuitetea Tanzania ndani na hadi nje yake.

Kama ninavyoamini mimi na wengine kwamba Lissu amejitoa kuitetea jamii ya Tanzani, pia duniani wapo wengi wamepita kuzitetea jamii zao. Wapo waliofanikiwa kuzipata haki walizokuwa wakizipigania wakiwa katika hali ya uzima bila hata kovu moja, licha ya madhila mengi waliyoyapata kutoka kwa wapinga haki hizo. Lakini pia wapo waliozipata haki hizo wakiwa walemavu, wagonjwa na waliodhoofika kutokana na madhila kama hayo ya kupigwa risasi na mateso mengineyo.

Na pia wako waliozikosa haki hizo kwa kuuwawa kikatili na wapinga haki waliokuwa wakipambana nao, lakini pamoja na kuuwawa kwao, bado harakati zao ziliendelea hadi kupatikana haki hizo walizokuwa wakizidai. Wengine hadi leo bado wanaendelea kupambana na kudai haki hizo huko huko makaburini walipo, mfano wa hao ni Dkt. Martin Luther King Jr. Huyu ni mfano wa wanaharakati waliokufa ambao hadi hii leo bado wako hai kupigania haki za jamii zao.

Sitaki nieleweke labda wamekufa kimazingara kama vile tuaminivyo kwamba watu hufa kwa kutolewa kikoa lakini wanatumika uchawini Bumbwini, Kwanyanya na Ukutini – Chambani Pemba. La hasha! Ninachokusudia ni kuwa ingawa bwana huyu na wengine mfano wake walipigwa risasi na kuuawa wakiwa katika mapambano ya kuzitetea jamii zao, fikra zao bado kila uchao zinaonekana kama zimetolewa leo, na jamii inatumia fikra zao kama ndio dira ya kuongozea mambo na nchi zao.

Ikumbukwe kwamba mwaka 2008 wakati wa kampeni za kugombania urais wa Marekani, taifa lililo kubwa zaidi duniani lakini likiwa pia na kiwango cha juu cha ubaguzi wa rangi dhidi ya weusi, waliingia katika historia mpya ya uongozi wa nchi hiyo ikiwa ni kwa kumuingiza rais mweusi madarakani, Barack Hussein Onyango Obama. Mtoto huyo wa raia wa Kenya alifanikiwa kwa kutumia kumbukumbu za harakati zile zile za Hayati Dk. King, ambapo hata katika baadhi ya majimbo ambayo Obama alihisi yana kiwango cha juu cha ubaguzi, alitumia msamiati wa ‘I have a Dream……..’ (Nina ndoto……), msamiati ambao ulitumiwa na Dk. King katika hutuba yake maarufu ya tarehe 28 Agosti 1963, miaka mitano kabla ya kupigwa risasi kadhaa katika taya na uti wa mgongo.

Basi kwa mfano huo wa wanaharakati waliouwawa kwa kutetea maslahi na haki za raia wa nchi zao, hususan Dk. Martin Luther King Jr, yatosha kuamini kwamba hata zile risasi zilizomiminwa kutoka kwenye bunduki aina ya SMG mbele ya ‘kadamnasi’, mchana kweupe, na baadaye moja kwa moja zikaingia katika tumbo, mguu, kiuno na bega la Lissu, sambamba na Watanzania wanyvyomzungumza baada ya tukio lile kuanzia siku ile hadi leo, nashawashika kuamini kwamba hata kama risasi zile zingempeleka kwenye umauti, bado Lissu angaeendelea kuzungumzwa, kutajwa, kupendwa na hata kuheshimiwa na Watanzania wanaoheshimu na kufahamu maana na malengo ya harakati za kusimamia na kuetea haki na maslahi ya raia. Kwa hivyo, hata kifo kisingelilizika jina la Lissu.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.