Si nchi istahiliyo kuongozwa kihuni

NILIPOMSIKIA Mohamed Aboud Mohamed, mwanasiasa ndani ya CCM anayeitwa waziri katika serikali anayoiongoza Dk. Ali Mohamed Shein, akitaka Jeshi la Polisi Tanzania kuwa makini na baadhi ya viongozi wa siasa wanaotumia mwamvuli wa siasa au dini kinyume na taratibu kutaka kuharibu amani na utulivu, kwa kweli nilijua kitakachofuata.

Huyu waziri katika serikali iliyojiweka madarakani, alifanya ziara kwenye vyombo vya ulinzi na usalama mjini Zanzibar. Ziara yenyewe ilinijenga imani kuwa inapalilia jambo kubwa na zito, na litadhihirika muda si mrefu.

Mohamed Aboud ambaye wanaompamba wanamuita Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, akiwa ofisi za makao makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar, akasema kwa kuwa nchi imetulia sasa, mambo yanakwenda vizuri, na vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake vizuri, wadhibitiwe watu wachache wenye nia mbaya na nchi na dhamira mbovu kwa maslahi yao binafsi wanaokusudia kuharibu amani na utulivu kwa ujanja wanaoufanya.

Na Jabir Idrissa

Kwa hivyo, anataka jeshi hilo kutilia maanani hali hiyo kwa kuizungumza mara kwa mara ili kuwahi kudhibiti tatizo kabla halijawa kubwa. Akasema jambo la msingi ni lazima watu hao wajulikane na wapelekwe kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichukuwe mkondo wake.

Nikarudi nyuma kidogo. Wiki mbili hivi, baada tu ya wahalifu kumshambulia kwa nia ya kutaka kumtoa roho Tundu Anthipas Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais wa Wanasheria Tanganyika, mwanasiasa asiyefanana kwa mengi na Mohamed Aboud naye alisema makubwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi au The Civic United Front (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad akionesha hisia kali dhidi ya shambulio lililolengwa kumuua Lissu kwa risasi za moto, alimtaka Rais John Magufuli kuitisha kikao cha dharura kujadili hali mbaya ya usalama katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maalim Seif alisema tukio alilotendewa Lissu limemshtua na kumfadhaisha na kufikia hatua ya kuamini usalama wa raia na mali zao umo kwenye mtihani mkubwa; na kuwa ipo haja kwake Rais kuitisha kikao cha dharura kitakachojumuisha viongozi wa kisiasa na wa kidini kujadili mustakbali wa taifa kipindi hiki.

Hawa wawili ni wanasiasa. Maalim Seif ni mwanasiasa wa enzi na aliyebobea. Amesomea hasa sayansi ya siasa na kuikhitimu kwa daraja la juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu miaka ya mwanzo ya 1970. Mohamed Aboud naye mwanasiasa, ila mchanga au wa kuja. Baada ya kufanya biashara kwa muda fulani, aliamua kuingia katika siasa ilipokaribia miaka ya 1990.

Maneno yake ni ya fitna. Yale ya Maalim Seif yanasihi kiongozi mkuu katika jamhuri si tu kutafakari, bali kuchukua hatua ya dharura. Huyu gwiji ameona kushambuliwa mbunge na wakili maarufu nchini, kunaashiria kuvunjwa kwa misingi ya amani na utawala wa kidemokrasia nchini. Hoja nzito kiuongozi na kimaono.

Hujaelewa sio? Angalia tukio la kushambuliwa Lissu lilivyoiteka dunia, achilia mbali Tanzania. Hujaona namna vyama vya mawakili Marekani (ALA), Afrika Kusini (SAL), Kenya (KLS), Zanzibar (ZLS), Uganda (ULS), Uingereza na Wales vilivyoibana serikali ya Rais Magufuli kutaka uchunguzi makini ufanywe kubaini wahusika wa kutaka kumuua Lissu na wakipatikana washitakiwe na ushahidi imara kutolewa mahakamani? Na katika muktadha huohuo, wametaka Marekani kama taifa na Umoja wa Ulaya (EU).

Maalim Seif, kama walivyopata picha mawakili wa mataifa hayo, amegundua kuwa utawala umeingia doa na uzito wake unampita hata kiongozi mwenyewe. Panahitajika mjadala mpana kuidhibiti hali iliyokwishavurugika. Anayaona matukio mabaya yanayozidi kuiharibu sifa ya jamhuri, ya kuitwa kisiwa cha amani na utulivu.

Maalim Seif, tofauti na Mohamed Aboud ambaye anaendekeza fitna ya kisiasa kwa kuwa yu miongoni mwa walaji nchi kwa ushindi uliotokana na kupindua maamuzi ya haki ya wananchi waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba 2015, anajua kasi ya uharibifu wa amani isipoangaliwa, taifa laweza kusambaratika.

Maalim Seif ndiye anayeshika uongozi wa kupigania kurudishwa kwa haki ya wananchi iliyonyongwa kutokana na tamko haramu la Jecha Salim Jecha la tarehe 28 Oktoba 2015 ambalo alilitoa mafichoni, nje na mbali kabisa na majukumu yake kama mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Jecha, kada mashuhuri CCM, katika siku hiyo, alikimbia makamishna wenzake waliokuwa na kazi muhimu ya kuuchunga mustakbali wa Zanzibar, na kutumika kutimiza matakwa ya mabwana zake CCM waliokuwa wameangushwa chini na wananchi kupitia sanduku la kura. CCM walikuwa wameshindwa kura halali.

Sasa wakati kosa hilo halijasahihishwa itakiwavyo, na Zanzibar yenye historia refu na iliyo hazina maishani, ikiwa na utulivu wa juujuu kwa vile umma mkubwa unaamini umedhulumiwa na haki yao ingali imeshikwa na hao madhalimu, anatokea Mohamed Aboud na maneno ya kutaka Polisi ikaze kamba katika kuwabana wananchi wanaotaka haki yao ya kikatiba.

Ni kwa sababu anajua vifua vya viongozi wa CCM na shingo zao vinazidi kuandamwa na dhambi ya dhuluma, anaingia, akibeba utumwa wa wakubwa zake wanaoumia naye pamoja, anashinikiza Polisi waumize wadaihaki.

Wanachokitaka kwa maneno aliyoyatoa na yakanukuliwa na vyombo vya habari vingi, ni Polisi kukamata viongozi wa CUF, chama kilichojijenga kuwa nguzo madhubuti ya kubeba matakwa ya Wazanzibari walio wengi Unguja na Pemba, na walioko ughaibuni, mpaka yatakapothibitishwa yameingia kwenye mikono salama.

Mohamed Aboud katu kwa maneno yake yale hakulenga kuiambia Polisi iwashike wapuuzi wanaobeba silaha za moto na za jadi na kupita mitaani wakishambulia wananchi katika maeneo ngome ya upinzani. Asilani abadani.

Mwanasiasa wa kuja huyu ambaye ndo katika wale wasiowakilisha hasa maslahi ya Wazanzibari wa asili ya Pemba, ingawa mwenyewe anatokea, anakula raha, anashiba yeye na familia yake, bali anahofia nguvu ya kudai haki ya wananchi inaongezeka na kama vile inahatarisha maslahi yao binafsi.

Yeye kama kweli anastahili kutambuliwa ni waziri msaidizi mkuu wa makamo wa pili wa rais, mbona hajasikika akiiambia Polisi tangu ikiwa chini ya Hamdani Omar kwamba iwadhibiti askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanaohujumu wananchi kila wakati mitaani usiku na mchana? Hajapata kusema na hawezi kusema hayo.

Sasa usiku wa siku ya pili baada ya maneno yake kwa Polisi, hao wanaoitwa askari wa vikosi vya SMZ ambao wananchi wamewapachika jina la “mazombi” waliingia mitaani kama kawaida yao, na kushambulia wananchi kwenye barza zao kuanzia magharibi. Udhalimu ulioje unaotendwa na kupaliliwa na viongozi wa CCM?

Naam, ni udhalimu tu. Unapoona askari wamebeba bunduki za moto na marungu ya miti na mapande ya nondo, na kushambulia raia huku serikali ikichekelea – hakika inachekelea kwa sababu siku zote wahalifu hao wamebaki kuwa ni watu wasiodhibitiwa kama vile watu wasiojulikana – ujue utawala umekuwa asi na kwa kujua haukubaliki kwa wananchi, hauna isipokuwa kutumia staili ya ufashisti kuendeleza madaraka.

Leo matukio ya mashambulizi dhidi ya raia yanayozidi kushuhudiwa, yameshalaza watu kadhaa hospitali, baadhi wakiwa wamevunjwa miguu na mikono. Hapo damu imemwagwa kipuuzi tu. Ni ili kufurahisha wakubwa. Sasa utasemaje nchi inaongozwa kwa sheria na wanaoongoza wanahishimu katiba na sheria? Zanzibar ni nchi ya watu wema, sio madhalimu, na kwa hivyo haiwezi kudumu kuendelea kuongozwa kihuni na wahuni. Hapana.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.