Zanzibar yakabidhiwa vifaa maalum vya kugundua watumiaji wa dawa za kulevya

Wagonjwa wanaotumia dawa aina ya ‘Methadone’ kama tiba baada ya kuathirika na dawa za kulevya na wanaoutumia aina nyengine ya dawa  kwa njia za siri wamepatiwa muarubaini baada ya kupatikana vifaa maalum vya kumgundua mtumiaji huyo kwa kupimwa mkojo .

Vifaa hivyo vinavyojulikana kwa jina la ‘DOAKIT’ vimetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na madawa ya kulevya na uhalifu (UNODC).

Mratibu wa Mradi wa Taifa wa kupambana na HIV/AIDS kwa wafungwa, Immaculate Nyoni ambae ni afisa wa UNODC Tanzania amemkabidhi vifaa hivyo Mratibu wa huduma za ukimwi kwa watu wa makundi maalum Zanzibar, Dk Shaaban Hassan katika hafla iliyofanyika Kliniki ya Methadone iliopo Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo- chekundu Mjini hapa.

Nyoni alisema UNODC itaendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapatia tiba sahihi wagonjwa walioathirika na dawa za kulevya ili kuona kunapatikana wanajamii wazuri.

Alisema katika uungaji mkono wao huo wameanzia kwa kuleta vifaa hivyo vya DOAKIT 1500 ambavyo vinaweza kutumika kwa kipindi cha miezi mitatu kwa mujibu wa idadi ya wagonjwa wanaotumia Methadone waliosajiliwa katika kliniki hiyo.

Daktari dhamana wa Hospitali hiyo ya Kidogochekundu, Dk Khamis Othman alilishukuru shirika la UNODC kwa kuwapatia msaada huo ambao kwa kipindi cha mwaka mmoja walikuwa na upungufu mkubwa na kupelekea baadhi ya wagonjwa kutumia aina nyengine ya dawa bila kujulikana.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za kutumia tiba ya Methadone mgonjwa hatakiwi kutumia aina nyengine ya dawa za kulevya na akifanya hivyo hupata madhara makubwa kwa kuongeza kiwango cha dawa mwilini.

Alisema DOAKIT ni vifaa vyenye uwezo wa kugundua aina sita ya dawa za kulevya kwa kuchunguza mkojo wa mtumiaji na vinaweza kutumika katika maeneo mbali mbali kuwachunguza watumiaji wa dawa hizo.

Dk Othman aliesema kuwa Kliniki ya Methadone ya Kidongochekundu ilianzishwa mwaka 2015 na imesajili wagonjwa 434 ambao wanapatiwa  tiba kamili na imekuwa mkombozi wa vijana wengi waliokubali kujiunga.

Alisema kazi ya Methadone ni kusaidia kuondosha hamu ya kutumia Heroine na dawa nyengine za kulevya hatimae mtumiaji huacha kidogo kidogo kutumia dawa hizo.

Hata hivyo amekiri kuwa bado wanakabiliwa na changamoto kubwa akisema kuwa baadhi ya wagonjwa wanaotumia Methadone hukosekana baadhi ya siku kufika kituni kwao kutokana na kufuata dawa  za kulevya kwa siri.

Msaada wa vifaa hivyo uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na madawa ya kulevya na uhalifu (UNODC) vimegharimu shilling milion 17 za kitanzania.

About Zanzibar Daima 1699 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.