Prof. Mbarawa amepotoka nafasi ya Wazanzibari taasisi za Muungano

Nimeisikiliza video inayosambaa katika mitandao ya kijamii iliyojumuisha kwa pamoja hoja zilizotokea Bungeni za Mhe. Saada Salum Mkuya, mbunge wa kuchaguliwa Jimbo la Welezo – Unguja, na waziri wa zamani wa fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT); na majibu ya Mhe. Makame Mbarawa, mbunge wa kuteuliwa na rais na waziri katika serikali ya JMT. Kinachodhihirika ni muendelezo wa khulka ya kuhuzunisha ya Wazanzibari kujisahau na kuhujumiana wenyewe kwa wenyewe, badala ya kushikamana na kutetea maslahi ya Zanzibar, ambayo kimsingi ndiyo yaliyowapeleka Bungeni.

Kifalsafa, ukiwasikiliza waheshimiwa hawa, utagunduwa mgongano wa kimtazamo kuhusiana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar baina yao na mgongano huu ndio unaoakisi kambi mbili kuu za kimtazamo kuhusiana na Muungano huo.

Kambi moja inautazama Muungano kama mashirikiano ya Washirika Wawili wanaostahiki haki, hadhi na fursa sawa. Kambi ya pili inautazama Muungano huu kama mzazi wa Nchi Moja tu na kwamba wale Washirika walikoma pale tu nchi zao zilipoungana na ambazo hakuna haja ya kupigiwa jicho tena.

Na huu ndio umekuwa msuguano wa kudumu juu ya NAFASI za WASHIRIKA wa Muungano huu.

Hoja za Mhe. Saada zinaonekana kusimamia mtazamo wa uwepo wa Washirika Wawili wa Muungano wanaostahiki hadhi, haki na fursa sawa na ambao inabidi watazamwe hivyo katika kila eneo . Prof. Mbarawa yeye anaonekana wazi kusimamia mtazamo wa Tanzania Moja na kuwa hivi tulivyo sasa ni utaratibu wa mpito tu kuelekea huko Tanzania Moja Khasa na Serikali Moja, na kuwa hakuna haja ya kutazama pande mbili ILA la muhimu ni kutazama SIFA na UWEZO wa mtu tu.

Mgongano ulipo

Tujadili kwa ufupi. Kwanza kwa wafuatiliaji wa Muungano huu wanajua fika kuwa, kwa upande wa Zanzibar, mtazamo wa Prof. Mbarawa ni fikra za utopia na porojo endelevu zinazodumishwa kwa lengo la kuisukuma Zanzibar kuelekea kule kwenye Nchi Moja na Serikali Moja.

Profesa Makame Mbarawa, waziri wa mawasiliano wa Tanzania

Lakini pamoja na hayo tuuchukue huu mtazamo wa Prof. Mbarawa na tuugeze na uhalisia wa mambo, kisha tujiulize: hivi kwa mtazamo huo huo, je hii leo yeye mwenyewe Prof. Mbarawa angelikuwa mbunge? Maana yeye ni mbunge wa kuteuliwa kupitia nafasi 10 za uteuzi wa rais. Hivi katika watu takriban milioni 55, Rais John Magufuli amekosa watu 10 wenye UWEZO na SIFA za kisiasa, mpaka amteuwe mtu ambaye hiyo SIFA na UWEZO wa kisiasa ulimshinda jimboni kwake ambako alikataliwa!?

Ni wazi kuwa Rais Magufuli alitizama uhalisia kuwa katika uteuzi ule, hawezi kukwepa kuteua Wazanzibari, na kupitia kapu hili ndio na yeye, Prof. Mbarawa, akapenya. Hata huo uwaziri, kama hoja ni SIFA na UWEZO tu, hivi yeye leo angelikuwa waziri? Maana kwa takriban watu milioni 55 walioko Tanzania Bara, kweli kakosekana mtu mwenye SIFA na UWEZO wa kukamata wizara hiyo – ambayo yenyewe kimsingi si ya Muungano – mpaka aletwe mtu kutoka Zanzibar?

Kiuhalisia, tujiulize zaidi: hivi yeye ni mahiri na mzoefu wa kuyaelewa mazingira ya kijiografia tu ya Tanzania Bara (achilia mbali utaalamu), kuliko mtu aliyezaliwa na kukulia Tanzania Bara? Si ajabu hayo maeneo anayofanyia kazi, kayajua baada ya kuupata huo uwaziri.

Na vivyo hivyo kwa Mhe. Saada, naye hapo alipokuwa waziri wa fedha – nayo kimsingi haikuwa wizara ya Muungano – hakuwa waziri kwa sababu Tanzania Bara yote hakuna mtu mwenye SIFA na UWEZO wa kufanya kazi hiyo. Ukweli ni kuwa msingi na kigezo cha kwanza kikubwa kinachowapa wao na Wazanzibari wengine fursa hizi ni Uzanzibari wao, baadaye ndio huja hayo mazingatio ya SIFA na UWEZO.

Dharau ya wanaoitwa viongozi

Ni jambo la kusikitisha leo kumsikia kiongozi akiwadharau, kuwakebehi na kuwabeza hadharani watu wa vijijini Pemba na waliopo Darajani, Mjini Unguja; wakati kiuhalisia hawa ndio ngazi aliyopandia na kumfikisha huko alikofika. Hichi kibri na jeuri si malipo yanayowastahikia abadan. Na huu ndio aina ya uongozi uliofikisha hapa Muungano huu, wa kudhani kuwa viongozi ndio waelewa na wananchi ni mambumbumbu.

Saada Salum Mkuya, mbunge wa Welezo – Unguja na waziri wa zamani wa fedha wa Tanzania.

Hawa wa vijijini Pemba na vijiweni Darajani ndio wenye hatimiliki ya Muungano, ilitegemewa kama ni manufaa basi yaende kwao na kama ni matatizo yatawasibu wao. Badala yake Muungano umekuwa milki ya viongozi na kila ukitaka kujipenyeza na kudumu kwenye uongozi, basi jipendekeze kwa kujifanya muumini wa Muungano wa aina hii ya Prof. Mbarawa; na ukiutetea uwe mkali kama uliyetoneshwa jipu; na uwe tayari hata kubeza na kudharau watu wako. Kiukweli, watu wa aina hii hawana mapenzi ya kweli na Muungano, bali Muungano kwao ni mtaji na jahazi tu la kuwavuusha kutimiza maslahi yao binafsi.

Tujiulize zaidi: kama hoja ni SIFA na UWEZO, kwa nini Katiba imesema Rais wa JMT akitoka upande mmoja wa Muungano, basi Makamo wa Rais atoke upande wa pili? Si tungetazama SIFA na UWEZO tu? Rais akitoka Chato, Makamo anaweza akatoka Kibondo. Kusingekuwa na haja ya kutazamwa ulipotokea. (Na hilo sharti na kuzitambua nchi mbili hizi lipo pia katika muundo wa Taasisi kadhaa za Muungano, kama vile Tume ya Uchaguzi, Tume ya Haki za Binadamu n.k. – ambapo inaelezwa kuwa mwenyekiti akitoka upande mmoja wa Muungano, makamo atoke upande wa pili). Kama kwenye Uongozi wa juu hilo limetambuliwa, kwa nini iwe nongwa kwenye mgao wa ajira tu?

Upotokaji wa Prof. Mbarawa

Prof. Mbarawa haeleweki aliposema Watanzania waliopo nje (nadhani alikusudia nje ya Bunge) wanataka aina hiyo ya Muungano na kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itatoa ushirikiano kwa yoyote anayewekwa Zanzibar kufanya kazi katika Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar, bila kujali ametokea upande gani wa Muungano.

Nadhani haelewi hisia za Wazanzibari katika hili na pia yupo mbali mno na malalamiko ya SMZ katika hili. Pengine hajapata fursa ya kuzisoma taarifa kadhaa kuhusu kero za Muungano, hususan kwa upande wa Zanzibar. Hiyo SMZ anayoisemea sijui ni ipi, lakini kwa SMZ hii tunayoijua sisi, hilo hawalikubali. Na ipo mifano ya SMZ, sio tu ya kutokutoa ushirikiano kwa wateule katika nafasi za Muungano wasio Wazanzibari, bali iliwatimua kabisa.

Mfano mmoja ni pale Mkuu wa Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar, alipoletwa mtu kutoka Tanzania Bara wakati wa enzi za uongozi wa Dk. Salmin Amour Juma na kukataliwa kuhudumu nafasi hiyo kwa Zanzibar. Baada ya tukio hilo,utaratibu huo ulisita, ingawaje sio kwa asilimia 100. Nadhani Mhe. Saada alizungumza kwa kuyaelewa mazingira ya siasa za Zanzibar, ambazo pengine Mhe. Mbarawa yuko mbali nazo.

Hili la ajira kila leo ni malalamiko juu ya Zanzibar kunyimwa au kupunjwa katika kupata ajira kwenye Taasisi za Muungano na hata nafasi za kiuongozi katika Mihimili ya Dola ya JMT na pia nafasi za kibalozi. Katika hizo balozi za Tanzania huko nje, mbali na Zanzibar kuambulia nafasi chache za ubalozi, tena katika nchi zisizo na umuhimu mkubwa kimaslahi, lakini yapo malalamiko kuwa wafanyakazi kutoka Zanzibar ni wa kutafuta.

Ukweli ni kuwa, kwa Wazanzibari hata huo Urais wa JMT walitaka uwe kwa zamu baina ya Zanzibar na Tanganyika. Katika ajira, wanataka uwepo uwiano, japo si sawa kwa sawa, baina ya Zanzibar na Tanganyika. Hata huo uwaziri kuna malalamiko jinsi Zanzibar inavyowekwa upande katika teuzi hizi. Wakati wa kuanza kwa Muungano mwaka 1964, pamoja na kuwa Mambo ya Muungano yalikuwa machache, 11 tu, ila Wazanzibari takriban wanane walipewa uwaziri. (Ukumbuke siku hizo Baraza la Mawaziri lilikuwa dogo, sio kama la leo). Leo hii mambo ya Muungano ni 22 lakini Mawaziri Wazanzibari ni wawili-watatu. Labda tumeimarisha kutizama Uwezo na Sifa tu bila kujali Washirika wa Muungano kama anavyopalilia Prof. Mbarawa.

Nina hakika Prof. Mbarawa anaposhiriki vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hutetea maslahi ya Tanzania kwa nguvu zote bila kujali kuwa SISI, wana wa Afrika Mashariki ni wamoja, na hivyo tutizame SIFA na UWEZO tu. Lakini huyu huyu linapokuja suala la kuitetea Zanzibar anakuwa na ukali wa ajabu, kama alivyoonekana katika mjadala huu.

Tuwe wakweli, mathalan zitokee nafasi 100 za ajira katika taasisi yoyote ya Muungano, halafu kigezo iwe ni SIFA na UWEZO tu, hata Wazanzibari wawe na uwezo na sifa kiasi gani, ndani ya maombi kutoka upande wenye watu milioni 55, atapita mtu kutoka upande wenye watu milioni moja!?

Amma kweli, maji hufuata mkondo. Na mkondo wa mto huu ni kuhakikisha kuwa Zanzibar inapotea kabisa na badala yake tujione kuwa ni Watanzania tu; wakati uhalisia ni kuwa hizi ni Nchi Mbili tofauti ambazo zimeungana, na ambazo zinastahiki haki na hadhi sawa.

Katika Muungano wowote, nchi huingia kwenye Muungano ili ifaidike na Muungano; ila inapofika wakati wachezaji unaopeleka uwanjani wakawa wameshupaa kujifunga magoli wenyewe, hapo ujue kuna tatizo la wachezaji kusaliti timu yao kwa maslahi yao binafsi.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.