HABARI

Jinsi tawala za kifamilia zinavyouwa demokrasia Afrika

Zipo sababu nyingi zilizomfanya Robert Mugabe ashinikizwe na jeshi na kisha chama chake kujiuzulu. Lakini sababu kubwa na ambayo chama chake ZANU-PF na hata Bunge, kiliiweka mbele ni suala la kuimiliki Zimbabwe kama mojawapo ya mali zake za kifamilia. Bunge lilisema lingemwondoa Rais Mugabe kwasababu mkewe Grace Mugabe amenyang’anya (usurp) madaraka ya urais wakati yeye si rais huku mumewe Mugabe akimwacha afanye kazi za serikali wakati si Rais wa Zimbabwe aliyechaguliwa.

Kufukuzwa kwa Emmerson Dambudzo Mnangagwa na hata Joyce Mujuru kabla yake kulishinikizwa na Grace ambaye alitaka kuurithi urais wa mumewe kwa udi na uvumba. Grace alidiriki kusema Emmerson Mnangagwa ni nyoka ambaye hana budi kupondwa kichwa. Sasa naamini katambua bayana kwamba vyeo vya umma kwa nchi za kidemokrasia si vya urithi wala si vya kifamilia. Na kwa namna fulani kapondwa kichwa yeye.

Familia ya Eyadema wa Togo

Gnassigbe Eyadema

Utawala wa familia ya Gnassingbé Eyadema nchini Togo ndio mkongwe kabisa Afrika kwa zaidi ya miaka 50. Kwa sasa kuna maandamano makubwa sana ya kuitaka familia ya Eyadema iondoke madarakani chini ya mtoto Faure aliyemrithi baba yake Gnassingbé alipofariki 2005.

Kama ilivyokuwa Zimbabwe iliyokuwa ikimlinda na kumtetea Mugabe, serikali ya Togo nayo inamlinda Faure kwa nguvu zote huku ikisaidiwa na jeshi. Baada tu ya kuingia madarakani, Faure Eyadema alimteua kaka yake wa kambo, Kpatcha, kuwa Waziri wa Ulinzi, japo walianza kugombania madaraka wao kwa wao na kisha Kpatcha kutiwa ndani.

Familia ya Bongo wa Gabon

Ali Bongo Odimba

Nchini Gabon, ni utawala wa familia ya Omar Bongo aliyetawala kwa miaka 42 kabla ya kufariki mwaka 2009. Akarithi mtoto wake Ali Bongo Ondimba ambaye anatawala hadi sasa huku akilaumiwa sana anavyovuruga chaguzi.

Ali Bongo Ondimba anamiliki vitega uchumi 39 nchini Ufaransa na magari mengi ya kifahari aina ya Ferrari na Mercedes. Familia ya Bongo imeigeuza Gabon mali yake. Nakumbuka hata mchezaji wa Barcelona, Lionel Messi, alilaumiwa sana kumtembelea dikteta Ali Bongo mwaka 2015.

Familia ya Nguema wa Guinea ya Ikweta

Theodoro Obiang Nguema Mbasogo

Nchini Guinea ya Ikweta, inatawala familia ya Rais Theodoro Obiang Nguema Mbasogo aliyeko madarakani kwa muda mrefu kuliko wote Afrika. Ni rais katili sana na aliyempindua mjomba wake, Rais Francisco Macias Nguema, na kumuua.

Mtoto wake mpenda anasa, Teodorin Obiang Nguema Mbasogo, ni makamu wake na anatarajia kumrithi baba yake. Nchi ya Ufaransa tayari imemhukumu Teodorin kwa ufisadi mkubwa.

Museveni wa Uganda

Yoweri Kaguta Museveni

Nchini Uganda, Yoweri Kaguta Museveni ametoka hali ya kupigania ukombozi wa Uganda hadi kupigania uongozi wa kifamilia.

Sasa anapambana kuondoa ukomo wa umri ambapo wabunge wamehongwa shilingi za Uganda milioni 29 kila mmoja ili kurahisisha kuondoa ukomo wa umri.

Wachache wamerudisha lakini wengi wameweka kibindoni na kuna uwezekano mkubwa hoja ya kuondoa ukomo wa umri kupita.

Januari mwaka huu, Museveni alimpandisha mwanawe wa kwanza Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba kuwa mshauri maalum wa rais, hatua inayotafsiriwa kuwa ni kumsogeza ikulu kurithi urais. Meja Jenerali Muhoozi kapewa vyeo haraka-haraka. Baadhi ya waganda huona Museveni anamchezea Mungu na yatamkuta ya Mugabe au Mobutu Seseseko.

Familia ya Kabila wa DRC

Joseph Kabila

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), familia ya Kabila ilitoka kupindua nchi kisha baba Laurent Kabila kubadilishana urais na mtoto wake Joseph Kabila anayeng’ang’ania urais hadi sasa pamoja na mihula yake miwili ya kutawala kwa kuchaguliwa kuisha rasmi Desemba 2016. Joseph alianza kutawala baada tu ya baba yake kuuawa mwaka 2001.

Dada yake Jaynet na kaka yake Zoe niwWabunge wanaomiliki utajiri mkubwa sana, yakiwemo mabenki, mashamba, usafiri wa ndege, ujenzi, mahoteli, biashara ya utalii, maduka makubwa na klabu za starehe.

Familia ya Zuma wa Afrika Kusini

Jacob Zuma

Nchini Afrika Kusini, Jacob Zuma amekazana sana kumfanyia kampeni mzazi mwenzake Nkosazana Dlamini-Zuma (ambaye walitalikiana), ili amrithi uongozi wa ANC mwezi ujao na kisha urais wa Afrika Kusini mwaka 2019. Kuna wengine wanasema Jacob Zuma anataka arithi urais Nkosazana Dlamini-Zuma kwa kuwa hataweza kumtia jela baba aliyezaa naye watoto.

Kwa sababu hizo, Rais Jacob Zuma kamtosa kabisa makamu wake, Cyril Ramaphosa, ambaye naye anawania uongozi wa ANC mwezi ujao na kisha urais mwaka 2019. Ni kivumbi kati ya familia ya Jaocb Zuma na Cyril Ramaphosa! Ikumbukwe pia kuwa Jacob Zuma anatuhumiwa kwa ufisadi mwingi akiunganishwa na uswahiba wake na familia ya Gupta.

Unafiki mkubwa

Inasikitisha sana kuwaona waliomlinda Robert Mugabe, akiwemo Emmerson Mnangagwa mwenyewe, na kuivuruga demokrasia ya Zimbabwe, ndio hao hao waliomshinikiza ajiuzulu. Na inatia shaka zaidi chama chake ZANU-PF kilichompitisha kuwa mgombea pekee wa urais mwakani (2018) akiwa na miaka 94, nacho ghafla kikamgeuka. Unafiki ulioje?

Emmerson Mnagangwa

Mashamba waliyoyatwaa kwa wazungu kwa sehemu kubwa waligawana viongozi wa serikali, jeshi na wanachama wa ZANU-PF. Ufisadi mkubwa ulioikumba Zimbabwe unatokana na ulafi na uroho wa viongozi wa kijeshi, chama na serikali chini ya Mugabe na mkewe Grace. Ndio walioporomosha uchumi wa Zimbabwe, lakini leo hii wanaendelea kutawala wenyewe tena.

Je, hapo kuna mabadiliko yoyote yenye tija Zimbabwe? Hakuna hata kidogo! Uchafu hauondolewi na uchafu! Aidha ugonjwa hautibiwi kwa ugonjwa, bali kwa dawa! Ikiwa chanzo cha kipindupindu ni uchafu, hatukitibu kwa uchafu, tutakieneza zaidi. Tusafishe kwanza, tuzoe na kutupa mbali kabisa uchafu wote ambao ni wale wote wanaojiita ZANU-PF na waliomkumbatia Mugabe.

Ndipo sasa tubadili wengine waliopigania demokrasia wakati wote, kama Mchungaji Evans Mawarire, Morgan Richard Tsvangirai, na wengineo. Hayo yangekuwa mabadiliko ya kweli ya mifumo na dawa ya ugonjwa wa Zimbabwe chini ya Mugabe. Tuanzie Zimbabwe kuondoa mifumo ya udikteta Afrika ambayo sasa inageuka kuwa mifumo ya utawala wa kifamilia.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwandumi Gwappo A. Mwakatobe wa Mwakaleli, Mbeya. Anapatikana kwa anwani za baruapepe: gwandumi@hotmail.com au gwappomwakatobe@gmail.com

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.