Kongamano la kimataifa la kiswahili kufanyika Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kimataifa la lugha ya Kiswahili linalotarajiwa kuanza Disemba 19 visiwani humu.

Kauli hiyo imebinishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza),Mohamed Seif Khatib wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Mnazi Mmoja Mjini Unguja.

Alisema kuwa katika kongamano hilo ambalo linatarajiwa kuwa la siku mbili, jumla ya mada 100 zinatarajiwa kuwasilishwa na wenyeji pamoja na wageni zikiwemo makala maalum zinazohusiana na masuala ya Kiswahili.

“Katika hizo mada 100 ndani yake muna makala ambazo wananchi na wataalam mbali mbali wataziwasilisha ambazo zitakuwa na mchango mkubwa katika kuikuza lugha ya kishwahili kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo”alisema Khatib.

Khatib alisema kuwa zaidi ya washiriki 100 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo wakiwemo wataalamu wa masuala ya Kiswahili wa ndani na nje ya nchi, taasisi za kiraia, wataalamu na wanafunzi kutoka vyuo vikuu pamoja na wanachi mbali mbali.

“Miongoni mwa nchi ambazo hadi wakati huu tayari zimeonesha nia ya kushiriki kongamano hilo ni pamoja na Tanzania bara, Kenya, Misri, Burundi, Ghana, Namibia, Marekani, Ujerumani, Uganda lakini pia kuna na nchi nyengine mbali mbali ambazo nazo tunatarajia kuwa zitashiriki”alisema Khatib.

Alisema kuwa lengo la kungamano hilo ni kuona lugha ya kiswahili inazidi kuimarika siku hadi siku pamoja na vipawa vya waandishi wa vitabu, vijarida na mambo mengine vinazidi kuendelea hasa kwa kutumia matumizi sahihi ya misamiati ya lugha ya Kiswahili.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar, Mwanahija Ali Juma amewataka wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa ya kongamano hilo kwa kushiriki ili nao waweze kuongeza utaalamu zaidi katika misamiati ya lugha yao.

Alisema kuwa kwa kuwa kongamano hilo litawashirikisha watu kutoka mataifa mbali mbali ni wazi kuwa hiyo ni fursa pekee ya kuweza kubadilishana mawazo pamoja na uzoefu katika utumiaji sahihi wa lugha ya Kiswahili.

“Ni muda mrefu Wazanzibari tumekuwa nyuma katika kuchangamkia fursa pindi zikitokea, hivyo niwaombe sana ndugu zangu hii fursa ya kongamano si ya kutupita hata kidogo hasa kwa kuwa ina umuhimu mkubwa pamoja na kuwepo na watu muhimu ndani ya kongamano hilo”alisema Juma.

Juma alisema kuwa pamoja na fursa hizo lakini pia wananchi wa Zanzibar wanaweza kunufaika katika kujua mbinu mbali mbali za kiufundi hasa kwa kutumia njia za kisasa za mitandao ya kijamii ambapo Zanzibar bado ipo nyumba katika matumizi ukilinganisha na nchi mbali mbali.

hata hivyo Makamo Mwenyekiti wa Bakiza, Maulid Omar Haji alisisitiza kuwa Kiswahili ni moja ya bidhaa adimu duniani hivyo ni vyema kwa waswahili wa Zanzibar kuitunza na kuithamini bidhaa hiyo ambayo ni miongoni mwa rasilimali ziliopo.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.