HABARI

Zanzibar, Kenya zakutana fainali CECAFA

Timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, imeingia katika fainali ya ubingwa wa kanda ya Afrika Mashariki na Kati unaojulikana kama Cecafa Senior Challenge.

 

Zanzibar Heroes iliingia fainali kwa kuifunga Uganda Cranes 2-1 katika mchuano wa nusu fainali ya pili Ijumaa. Kenya ilijikatia tiketi ya fainali kwa kuifunga Burundi 1-0 katika nusu fainali ya kwanza Alhamisi.

Mechi ya fainali itafanyika Jumapili, wakati Burundi na Uganda zitakumbana Jumamosi kutafuta mshindi wa tatu.

Mchezaji Abdul Azizi Makame wa Zanzibar katika dakika ya 25 alifunga goli la kwanza na Derrick Nsibambi wa timu ya Uganda alisawazisha. Mohammed Issa Juma alifanikiwa kuipatia timu yake ya Zanzibar bao la pili la ushindi katika dakika ya 57.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za michuano hiyo hii ni mara ya kwanza timu ya Zanzibar kufikia fainali ya michuano hiyo tangu iliposhinda kombe hilo kwa mara ya mwisho 1995.

Baada ya kufanikiwa kuingia fainali hiyo Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, Khamis Ali Mzee, ametuma ujumbe kuwa: “Sasa FIFA wapende wasipende watatutambua.”

Kwa miaka kadha sasa Zanzibar imekuwa ikitaka ipewe nafasi kushiriki mashindao ya FIFA yenyewe badala ya kujumuishwa katika timu ya pamoja ya Tanzania.

Chanzo: Voice of America Swahili

1 thought on “Zanzibar, Kenya zakutana fainali CECAFA”

  1. …Baada ya kufanikiwa kuingia fainali hiyo Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, Khamis Ali Mzee, ametuma ujumbe kuwa: “Sasa FIFA wapende wasipende watatutambua.”

    Nimeipenda hiyo statement…
    Tunawapa pongezi mabinamu, kila la kheri J2..

    #CYZH

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.