Mungu anasema na Wazanzibari

Napata shida kuwaona wananchi wanyonge wakijitoa kwa hamu na shauku ya kuipigania nchi yao. Mapigano hayo yakiwa ya furaha, huzuni au majonzi lakini wakiamini hayo ndio yanaowaunganisha na kuwagawa.

Napata maswali mengi juu ya nani hasa anayepaswa kusimamia uzalendo wa wananchi wanyonge kama wananchi wa nchi yangu niipendayo, nchi ambayo ina kila aina ya ustaarabu unaotokana na asili ya watu wake nq pia utamu na ladha isiyokishwa ya jina lake…Zanzibar!

Natamani kuwaona wale wanaojinasibu na uongozi wa Zanzibar wakijirudi kwa kuitika wito wa umoja na mshikamano ambao Mungu ameuonesha kupitia tasnia ya soka takribani juma zima tangu kuanza kwake.

Napata simanzi na uchungu sana pale ninapowaona wananchi wanyonge wanapokusanya unyonge wao wakaipigania nchi yao, huku wanaopaswa kusimamia unyonge huo kwa kuwaunga mkono wakiwadharau na kuwakebehi, wakiwatumilia kukidhi maslaha yao ya kidunia.

Kwa nini uzalendo wetu unasalitiwa na wanaotutawala? Kwa nini watawala hamugutuki mukatubia kwa matendo yenu na mienendo yenu dhidi yetu? Kwa nini kama kulia na kuhuzunika isiwe kwetu sote, na furaha na vicheko visiwe kwa umoja wetu?Kwa nini tulie na tuhuzunike sisi tu, huku nyinyi mukitufanyia mzaha na kututumia kwa muda mchache kwa dhamira ya kukamilisha malengo yenu?

Kwa nini uzalendo wetu usalitiwe na wachache? Kwa nini kila siku tuwe na furaha ya msimu, huzuni zikawa ndio nguo zetu na matandiko yetu? Kwa nini rasilimali zetu zisitumike kutuunganisha na kutujenga kuwa wazalendo wa kweli,  na badala ya uzalendo wa msimu na kutumiana?

Ingawa nina huzuni, lakini naamini Mungu anasema na watawala wanaowadhulumu wananchi wanyonge kupitia dhana ya uzalendo. Naamini ni sauti na ukuu wa Mungu anaowaonesha wananchi wa Zanzibar kwa mara nyengine tena. Mungu anawaambia watawala nini wanachokihitaji wananchi wanyonge wa Zanzibar.

Mungu anawaambia Wazanzibari: “Nahitaji muishi kwa kupendana katika dhiki na raha!” Mungu anawaambia watawala: “Simamieni uzalendo wa wananchi wenu!” Mungu anawaambia: “Huu ndio ustaarabu wa kileo!” Mungu anawaambia: “Umoja na upendo ndio msingi wa uzalendo wa kweli!”

Mungu anawaambia: “Visiwa vyangu nitavilinda kwa upendo japo vinasalitiwa kwa unafiki na ubinafsi!” Mungu anawaambia: “Nitawaunganisha waja wangu japo watawala wanawatenganisha!” Mungu anawaambia: “Waja wangu hawa wataipenda na kuisimamamia nchi yao niliowatunukia!”

Mungu anawaambia: “Nchi yangu itabaki na jina lake litatukuka hata kama kuna maelfu wasiopenda kushuhudia hivyo!” Mungu anawaambia Wazanzibari wataendelea kuwa Wazanzibari hata kama kuna watu wanataka kuwabadili kua vile watakavyo wao.

Mungu anawaambia iko siku uzalendo wa kweli utapata wa kuusimamia na kutoa tija kwa wananchi wake wanyonge.

Mungu ibariki Zanzibar.
Mungu wabariki Wazanzibari!

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ibrahim Ali.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

1 Comment

  1. It is delicious post, wish you good health so as to manage more best post like that ones,

    Thanks.

    Al-Baghir
    Attorney.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.