Zanzibar Heroes iliufanya 2017 kuwa Mwaka wa Mashujaa

Ulikuwa usiku wa maajabu, usiku wa furaha, usiku wa historia na usiku wa aina yake. Usiku wa Mashujaa. Nalazimika kuuita majina tofauti usiku wa tarehe 23 Disemba 2017 kwa kile kilichotokea pale katika jengo maarufu la Baraza la Wawakilishi la zamani kwa kile alichokifanya Dk. Ali Mohammed Shein kwa vijana wa Zanzibar Heroes. Nauita hivi kwa sababu kila Mzanzibari mpenda michezo na asiyependa michezo alifurahishwa usiku ule.

Hata hivyo, jambo moja lazima nilieleze na nieleweke. Kwamba usiku huo haukutokea tu burebure, bali ulikuja kutokana na sababu maalum tena yenye uzito wa hali ya juu. Kwa nchi za wenzetu waliokuwa hawana kizuizi cha dini, bila shaka kungechongwa masanamu yakapakwa rangi ya dhahabu na kuwekwa sehemu maalum kila anayepita ayaone. Lakini kwa kuwa kwetu sisi hilo ni ‘kharam’ tena ‘mutalak’, basi angalau tuliweza kukifanya kile kidogo kisichochupa sana mipaka ya mafundisho ya dini yetu.

Na Ali Mohamed

Usiku huu uliwezekana kwa kuwa wachezaji wetu, ndugu zetu, wenetu na marafiki zetu wa Zanzibar Heroes walitanguliza kufanya maajabu nchini Kenya katika mashindano ya CECAFA 2017 sio tu kwa kuvifunga vigogo vya Afrika Mashariki na Kati lakini pia kwa kiwango kikubwa cha soka walichokionesha mashujaa wetu hao kiasi cha kuwafanya vigogo hao wataharuki na wasiamini hadi hii leo.

Wafuatiliaji wote wa soka sio tu nchini Zanzibar, bali pia hata Tanganyika, Afrika na ulimwengu mzima wanakubaliana juu ya kitu kimoja – kwamba Zanzibar Heroes walichokifanya ni cha maajabu na kwacho wameifanya dunia nzima sasa ielekeze macho ya heshima katika taifa letu dogo la Zanzibar.

Ndani ya Zanzibar kwenyewe, Zanzibar Heroes walichukuliwa kuwa ni washindi halisi wa michuano ile hata kama hawakurudi na kombe. Kupitia kwao, waliufanya usiku wa tarehe 23 Disemba kuwa alama ya Umoja wa Wazanzibari, ambapo makundi yote mawili ya kisiasa visiwani mwetu – yaani lile rafiki kwa Dk. Shein na lile lenye uhasama naye – yalifurahishwa na kilichotendwa naye kwenye usiku huo.

Heshima ambayo Dk. Shein amewapa Mashujaa wa Zanzibar haiwalazimishi wasiomkubali kuacha kuendelea na uhasama wao au kuondoa tofauti zao zozote naye, lakini naamini wamekiridhia na kukipongeza kile alichokifanya, hata kama bado wataendelea kutokuwa na mapenzi naye kwani kile kitu hasa kinachowahasimisha baina yao bado hakijawa sawa.

Tangu pale Dk. Shein amalize kutaja zawadi yake ya tatu kuwazadia Zanzibar Heroes, kila kona, kijiwe, kipembe, baraza na maskani hapa Zanzibar yalikuwa ni maneno ya pongezi kwenda moja kwa moja kwa kiongozi huyo au pongezi kwa Zanzibar Heroes kwa kuzawadiwa.

Mwanzoni kabla ya kukamilishwa kutajwa zawadi hizo, wengi hawakuamini kwamba hizo walizopatiwa ndizo zingekuwa zawadi zao, kwa sababu katika historia ya Zanzibar hakuna kipindi serikali kama serikali kufanya jambo hilo kwa wanamichezo hata pale walipofanya jambo zuri zaidi ya hili la Zanzibar Heroes.

Ikumbukwe kwamba mwaka 1995, wakati wa utawala wa Dk. Salmini Amour Juma (Komandoo), wachezaji wa Zanzibar Heroes ya wakati ule ambao ni wazazi wa hawa wa sasa, walifika hatua ya fainali ya mashindano ya CECAFA na wakachukuwa kombe, lakini serikali kama serikali haikuwa na kubwa walilolifanya zaidi ya mfanyabiashara Mohammed Raza kuwazawadia vespa mashuhuri kwa wakati huo chapa cha Select.

Jambo la pili lilikuwa likinipa wasiwasi juu ya uwepo wa zawadi hizo ni jinsi Dk. Shein alivyolifanyia usiri mkubwa jambo hili la zawadi alizotoa, kwa sababu siku moja nyuma aliulizwa na waandishi waliotaka kujuwa ni zawadi gani angewazawadia vijana wa Zanzibar Heroes, lakini akasema hio ni siri yake na asingemwambia mtu yeyote hadi usiku wa tarehe 23 Disemba ndipo ingejulikana.

Na jinsi Dk. Shein alivyokuwa akihutubia hadhara iliyokuwepo pale, mimi na wenzangu tuliokuwa pamoja kuangalia hafla ile tulikata tamaa na tulikuwa tukinong’onezana na kuambizana kwamba zawadi ya kwanza tayari Dk. Shein amesema ni kule kualikwa Ikulu kupata chakula cha mchana, ya pili ni taarabu maalum kutoka kwa kikundi cha taifa, hii ilitulazimisha kuamini hivyo kwa sababu Dk. Shein alisema kikundi cha taifa ni kikundi cha hadhi sana, huwa hakipigi ila kwa shughuli maalum, hivyo moja kwa moja tukajiaminisha kwamba hio ndio zawadi ya pili yenyewe kutokana na umaalum wa kikundi hicho na ya tatu ni kuwapeleka Pemba ingawa hii haikuwa na ushawishi mkubwa kuamini, sote kwa pamoja tukanong’onezana kwamba idadi ya zawadi tatu zimekamilika, hivyo ikimaliza hapo kila mtu “azinge kitanda akalale”.

Wengine waliamini kwamba ipo zawadi yenye kuonekana ambayo Dk. Shein atatoa, na wakaamini kwamba kwa jinsi Zanzibar ilivyotawaliwa na kila aina ya usafiri, wengi wao waliamini labda ZH wangepewa usafiri, na wengi wao walijikita katika hivi vihonda vya kisasa ‘Click’, ndio ingekuwa Zawadi, lakini baada ya Dk. Shein kutangaza zawadi ya kwanza tu yaani ile ya kuwapatia hundi za shilingi milioni 3 kila mmoja, hakika hakuna aliyeamini, bali tulilazimika kuamini kwa sababu ndio tayari tamko limeshatoka na uthibitisho wa kwamba hilo ni la kweli, ni pale makabidhiano ya hundi hizo yalipoanza kwa kila mmoja kukabidhiwa hundi yake ambapo ni kusema ni zaidi ya milioni 90 ziligaiwa kwa kikosi hicho kilichofanya vyema katika mashindano ya CECAFA kule Kenya, ambapo yameliweka taifa la Zanzibar katika ramani, fursa na mazingira mazuri ya maendeleo ya kimichezo licha ya kuwa nje ya uanachama wa CAF na FIFA.

Haikutosha na kuishia hapo tu, Dk. Shein pia tena akaongeza zawadi pale aliposimama na kutangaza kwamba kila mmoja katika wachezaji na viongozi wao, atapatiwa kiwanja cha kujenga nyumba.

Niseme ukweli kwamba hii ndio zawadi ambayo ilikuwa kilio changu kwa Dk. Shein, hata ukenda sasa hivi katika ukuta wa ‘Facebook’ wa ikulu, ukiangalia kumbukumbu ya vidio ya hafla ya chakula cha mchana, wakati ukuta huo ulipokuwa mubashara na kuruhusu watu kuchangia maoni yao, basi utakuta nimeandika “Dk. Shein vijana wapatiwe viwanja Tunguu”.

Nilitaka hivi ili wawe na kumbukumbu inayoonekana na kusimulika zaidi. Na naam, furaha na vilio vya furaha vilisikika kutoka kwa wachezaji wetu kwa kutoamini kilichotokea, na wengine waliopata nafasi ya kufanya mahojiano ukumbini pale, nje ya ukumbi na vijiweni wanamokutana na marafiki zao, hawakusita kueleza kwamba usiku ule hawakuamini kama ungekuwa na maajabu yale kwao.

Ndio kwa mambo hayo yote niliyoyaeleza, nalazimika kuamini kwamba usiku ule ulikuwa ni usiku wa ajabu, ni usiku wa historia, ni usiku wa furaha, ni usiku wa faraja na ni usiku wa aina yake kutokea katika historia ya Zanzibar kwa mpira wa miguu. Nifike tamati kwa kumpongeza Dk. Shein na niwapongeze wachezaji na viongozi wote wa Zanzibar Heroes. Ahsanteni sana kwa ‘kutunavya uso’.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.