Zanzibar ingekuwa Zanzibar, Heroes wangefika mbali

Shamrashamra za mafanikio baada ya timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, kushika nafasi ya pili katika mashindano ya Kombe la CECAFA 2017, zimeibua hisia kubwa na furaha miongoni mwa Wazanzibari.

Hisia hizi zikazidi kushika nguvu na hamasa, baada ya timu nyengine ya Zanzibar, Zanzibar Sand Heroes, kuibuka kidedea na kubeba kikombe katika michuano ya soka la ufukweni, Copa Dar es Salaam Beach Soccer 2017, yaliyofanyika kwenye mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania na kuzishirikisha pia timu za Malawi, Uganda na mwenyeji wao, Tanzania.

Kabla ya ushindi wa Sand Heroes na baada ya ule wa Zanzibar Heroes, timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Zanzibar nayo ilishinda kwenye michuano ya Vyuo Vikuu vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, TUSA 2017, na kuchukuwa kombe kama wenzao wengine.

Pamoja na furaha hii ya michezo, yapo masuala muhimu mawili yamejitokeza katika kipindi hiki, na makala hii inayachambuwa mambo hayo na maana yake halisi kwa maisha ya kila siku ya taifa la Zanzibar na watu wake.

Hisia za Umoja na Mshikamano

Kwanza kabisa na kilicho wazi zaidi, ni hisia za umoja na mshikamano wa Wazanzibari katika jambo lolote lenye maslahi ya kitaifa kwa nchi yao. Hili la mpira nalo limeibuwa hisia za kujiamini, kuweza, umahiri, na uwepo wa vipaji vya kutosha kupeperusha bendera ya Zanzibar katika utambulisho wa michezo na hususan soka kimataifa kwa ufanisi zaidi.

Sehemu ya umma uliojitokeza mitaani Zanzibar kuwaunga mkono Zanzibar Heroes wakati wa Fainali za CECAFA2017

Kupitia ushindi huo,  Wazanzibari kwa ujumla wao wameendelea kutoa wito kimaneno na kivitendo kuwa wanao uwezo kuiwakilisha nchi katika michuano megineyo kama vile Kombe la Mataifa ya Afrika kupitia CAF na Kombe la Dunia kupitia FIFA, na hivyo kulaumu kuminywa kwa fursa hiyo kwao.

Kihistoria yapo mambo mengi sana ambayo yaliweka bayana umoja wa Uazanzibari katika mambo yenye maslahi kitaifa kama vile mjadala wa masuala ya mafuta na gesi, na suala la katiba mpya. Katika hili la michezo kauli mbiu maarufu kwa rika zote ni #SongaZanzibarSonga na hakuna mwanya wa kidudu mtu kujipenyeza.

Siasa za Utaifa na Utambulisho

Jambo la pili, ni hisia za kisiasa za Wazanzibari kuhusu nchi yao kuhusiana na mazingira ya kisiasa ya ndani ya Zanzibar na yale yanayohusu mahusiano yake na Tanzania Bara (Tanganyika) ndani ya Muungano uliopo.

Ambapo kuna wengine wanalaumu sana kuhusisha siasa na michezo, uhalisia unawasuta, kwani michezo – kama eneo jengine lolote la kijamii – haiwezi kujitenga na siasa. Kama ilivyo kwenye uchumi, kwa mfano, michezo pia ni eneo linalohusu ugawanyaji wa fursa na rasilimali na uendelezaji wa watu na, hivyo, nalo husimamiwa kwa sera na utawala. Kwa hivyo ni siasa. NUKTA.

Kiuhalisia, hata mgawanyo wa kimamlaka wa nchi yetu unalizingatia suala la michezo kama ni sehemu nyeti ya siasa za nchi. Kimsingi suala la michezo si katika mambo ya Muungano, lipo chini ya mamlaka ya Zanzibar pekee. Hapo ndipo wengi hawaelewi na hawataweza kuelewa kwa nini Zanzibar isipewe nafasi kushiriki katika michuano ya CAF na FIFA kwa kigezo kuwa Zanzibar si nchi.

Ndio maana wakati wa michuano hii ya CECAFA na hata Copa, Wazanzibari wengi walikejeli jina walilotumia majirani zao katika michuano hii kama “Tanzania” na kutaka wajiite kwa jina lao la asili kabla ya Muungano, yaani ‘Tanganyika’, ili kutenganisha utambulisho wa washiriki. Hili niliachie hapa sijakusudia kulizungumzia kwa undani.

Kumbukumbu ya Siasa za Uchaguzi 

“Nawapongeza Zanzibar Heroes kwa kututoa kimasomaso na kutinga fainali. Nawatakia kila la kheri katika mechi ya fainali waibuke na kombe na watupe raha ambayo Watanzania tumeikosa kwa muda mrefu” – Rais Mstaafu Kikwete.

Katika hili la siasa, pia ziliibuka hisia kali kuhusu dhulma iliyopitikana Oktoba 2015 ya kufujwa kwa matokeo halali ya uchaguzi na chama tawala kujiweka madarakani kwa nguvu za jeshi. Pamoja na hayo kuendelea kuwadhulumu wananchi na kuwanyanyasa. Kwa vile wengi wetu hatuwezi kusahau wala kudogosha udikteta huu, wapo waliotoa kauli za wazi kulaani dhulma hii ambayo bado inaendelea kutekelezwa dhidi ya Wazanzibari.

Timu ya Zanzibar Heroes ikipokewa kishujaa nyumbani baada ya kuwa washindi wa pili CECAFA 2017.

Hata hivyo, yamejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kututaka ‘tusichanganye siasa na michezo’. Hayo yamejitokeza kupitia michango mbalimbali katika vyombo vya mawasiliano ya kijamaa kwa nyakati tofauti.

Kwa mfano, kufuatia Zanzibar Heroes kufuzu kutinga fainali za michuano ya CECAFA 2017, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, alituma ujumbe kupitia Twitter kuwapongeza Zanzibar, akiandika: “Nawapongeza Zanzibar Heroes kwa kututoa kimasomaso na kutinga fainali. Nawatakia kila la kheri katika mechi ya fainali waibuke na kombe na watupe raha ambayo Watanzania tumeikosa kwa muda mrefu”.

Tatizo halikuwa kauli bali mtoa kauli na hapakukosekana majibu.

Moja katika watoa maoni wa awali kabisa kwenye salamu hizo za Rais Mstaafu Kikwete, alikuwa Mkurugenzi wa Nje wa CUF, Ismail Jussa, ambaye aliuliza “Wakupe raha wakati wewe uliwapa karaha kwa kuifisidi Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuyapindua maamuzi ya Wazanzibari na kuyavuruga Maridhiano yao?”

Na wengi wengine wakamkumbusha Kikwete juu ya yale aliyowatendea au aliyowacha yatendeke dhidi ya Wazanzibari wakati wa utawala wake. Miongoni mwayo ni kitendo cha kuwasweka ndani viongozi wa Uamsho na nafasi yake kama Amiri Jeshi Mkuu kuvuruga na kupindua maamuzi ya wananchi wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kwa hili hatuwezi kutenganisha siasa na michezo, maana hisia zetu kuhusu utu wetu, uhuru na uwepo wetu kama jamii huru na maisha yetu ni muhimu zaidi kuliko michezo. Kwa wale waliofisidi ustawi wa jamii yetu ni lazima waambiwe makavu uso kwa macho. Na hapa wamefanya vyema waliotoa maoni.

Michuano ya Siasa za Ndani ya Zanzibar

Kwa upande wa siasa za ndani ya Zanzibar, lile kundi ninaloliita hapa “wafadhiliwa waliowekwa madarakani baada ya Mapinduzi ya Oktoba 2015” nao walijitia kulibeba haraka hili la Zanzibar Heroes na kulitumia kama turufu kuonesha kwamba mahusiano yao na jamii sio mabaya ili wapunguzuwe mbinyo na wahisani na waachiee hadi 2020.

Yaani licha ya kuwa kukuibia na kukupora, lakini haya anayoyafanya anastahiki kusifiwa! Sisi tulio pembeni tutajiuliza kama kweli wewe akili zako zipo timamu. Huo ni  ulimbukeni, upogo wa mawazo, utindio wa ubongo, na ndio huo ubwege.

Ingawa kitu kimoja kilikuwa wazi. Kundi hili lilijitokeza baada ya kuona kiwango cha hamasa kilivyopanda kupitia uhamasishaji wa mitandao ya kijamii. Katika kujikurupuwa kwao, wakaitisha onesho la umma kwa televisheni kubwa ya uwanjani illi watu wawaangalie vipenzi vyao Zanzibar Heroes wakicheza fainali. Na bila kusahau, Dk. Ali Mohamed Shein akawazawadia wachezaji zawadi na kuwaandalia hafla ya taarabu pale waliporejea nyumbani.

Mapokezi ya Mashujaa wa Zanzibar

Na tena wapo waliojitokeza wakasema ‘katika hili tunawapongeza, wamejitahidi’ lakini pia wale waliokumbushia uovu wa watawala hawa walijibiwa vile vile “msichanganye siasa na michezo”.

Kwa watu wenye kutafakari, kulisifia kundi la “wafadhiliwa waliowekwa madarakani baada ya Mapinduzi ya Oktoba 2015” kwa usanii huu, ni sawa na wewe kuvamiwa na jambazi nyumbani kwako na kukuibia mali yako na kukudhalilisha, kisha jambazi huyo unayemjua akawa anagawa vijisenti kutoka katika ile mali aliyokuibia, nawe ukadiriki kusema “tusichanganye ujambazi na roho nzuri ya huyu mtu!”

Yaani licha ya kuwa kukuibia na kukupora, lakini haya anayoyafanya anastahiki kusifiwa! Sisi tulio pembeni tutajiuliza kama kweli wewe akili zako zipo timamu. Huo ni  ulimbukeni, upogo wa mawazo, utindio wa ubongo, na ndio huo ubwege.

Picha hii inaakisi uhalisia wa yaliyotokea. Pamoja na Wazanzibari kutenzwa nguvu kwa kuwekewa watu ambao hawakuwachaguwa. Pamojam na watu hao wakavunja utaratibu wa utawala wa serikali ya Umoja wa Kitaifa waliojiwekea Wazanzibari wenyewe kupitia maamuzi ya wananchi kwa kura ya maoni. Pamoja na watu hao kujiweka madarakani na kufisidi rasilimali za Wazanzibari kinyume na haki. Pamoja na watu hao kuendelea kuwanyanyasa na kuwadhulumu watu kwa kutumia vikosi vyao vya vurugu vilivyopagazwa majina ya mazombi.

Pamoja na yote hayo, kisha wanatumia mwanya wa furaha ya Wazanzibari kujisogeza karibu na umma ili waonekane wametenda vyema. Sidhani kuwa kamwe Wazanzibari wanaweza Kamwe kujingikiwa kiasi hicho. Kamwe Wazanzibari hawawezi kuwa wasaliti kwa madhila na dhulma zilizowafika wenzao mpaka wengine kufikia kupoteza roho zao kwa vipigo vya askari mamluki wa “wafadhiliwa waliowekwa madarakani baada ya Mapinduzi ya Oktoba 2015” .

Kamwe hawawezi kusahau walivyotenzwa nguvu na kupindua maamuzi ya wengi Oktoba 2015, maana ukweli ni kuwa Zanzibar ni jamii ya umma uliotenzwa nguvu, hisia zenye kusononeka, vipaji vilivyokandamizwa, nafsi zisizo huru, na utu uliokanwa.

Laiti Wazanzibari wangekuwa watu huru, laiti wangekuwa na serikali waliyoichagua kwa ridhaa yao, laiti wangekuwa na utawala unaowajibika na kuheshimu haki za raia, unaoheshimu utu wao na kuwaunganisha kwa kusimamia matakwa yao kama jamii huru, laiti Zanzibar ingelikuwa kweli Zanzibar, basi Zanzibar Heroes wangefika mbali.

Tanbihi: Makala hii imeandikwa na Khamis Issa, mtaalamu wa fani ya siasa za kimataifa na utawala anayeishi kwa sasa barani Ulaya.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.