Wafungwa wa gereza la kilimani Zanzibar kunufaika na mafunzo ya ushoni

Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib, amesema mabadiliko mengi ya kimaendeleo yaliyopatikana baada ya Mapinduzi yanatokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akiweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha mafunzo ya ushoni makao makuu ya Vyuo vya Mafunzo Kilimani mjini Zanzibar, Waziri huyo amesema serikali ina azma ya kuendeleza Mapinduzi hayo kwa kuingiza mapato kwa njia mbaimbali ili kuinua uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja.

Alisema baada ya mapinduzi, serikali imeamua kujikita zaidi katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake kwa kukuza uchumi wa taifa ili waweze kufaidika na matunda hayo.

Mhe. Salama alisema kazi ya ushoni ina maslahi mazuri kama zilivyo shughuli nyengine, hivyo wanafunzi hawana budi kuchangamkia fursa ya kuwepo chuoni hapo kwa ajili ya kujifunza.

Aidha alisema taaluma ya ushoni ina nafasi kubwa ya kuwapatia vijana ajira na hivyo kujipatia kipato kitakachowasaidia kuendesha maisha yao.

Aidha alitaka jengo hilo litakapokamilika liwe na utaratibu wa kufanyiwa ukarabati kila baada ya muda  ili kuliimarisha na kuwa kivutio kwa wateja.

Risala iliyosomwa na ASP Jaffar Abdullah, imeeleza kuwa jengo hilo likianza kazi litashona sare za wanafunzi na maofisa wa vyuo vya mafunzo, pamoja na taasisi mbalimbali.

Hata hivyo, wameitaka serikali kuwaingizia fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ambao awali ulikadiriwa kugharimu shilingi 67,000,000, lakini chuo hicho kimetumia shilingi 21,000,000 kutoka mfukoni mwake.

Naye Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar Ali Abdullah Ali, alisema jengo hilo litakapokamilika litaweza kuchukua zaidi ya wafanyakazi 40 kwa wakati mmoja.

Pia alisifu juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kuhakikisha vyuo hivyo vinawekewa mazingira bora ili viweze kuleta tija na kudumisha amani na utulivu uliopo.

“Chuo hicho kitaipunguzia serikali gharama za kushonesha nguo nje, na fedha zitakazookolewa  zitatumika katika shughuli nyengine za kiuchumi,” alisema.

Ufunguzi wa chuo hicho ni miongoni mwa shamrashamra za kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

About Zanzibar Daima 1606 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.