George Weah ataja vipaumbele sita katika uongozi wake Liberia

Rais mteule wa Liberia George Weah, ameainisha vipaumbele vyake sita katika muhula wake wa urais wa miaka sita akitoa wito kwa nchi hiyo kuanza kuuza mazao yake nje ya nchi na kukarabati miundo mbinu chakavu ya nchi hiyo.

George Weah aliyasema hayo jana katika mahojiano yake ya kwanza kuwahi kufanya tangu kushinda kiti cha urais wiki iliyopita.

Weah alipata uungaji mkono mkubwa wa vijana na hivyo kumuwezesha kushinda kiti cha urais kwa kuibuka na zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Liberia.

Amesema kuwa anataka kuiona nchi hiyo ikiboresha sekta ya kilimo ili kuwawezesha wananchi kuzalisha chakula chao wenyewe.

Aidha amesema kuwa Liberia ina uwezo wa kuuza mazao yake nje ya nchi iwapo kilimo kitaboreshwa. Ametolea mfano wa Ghana na nchi nyingine jirani zinazouza mazao yao nje ya nchi.

Zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wa Liberia wanategemea kilimo.

Itakumbukwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya Waliberia wanategemea kilimo kwa ajili ya kujikimu kimaisha huku kampuni kubwa ya Sime Darby yenye makao yake nchini Malaysia ikiwekeza pakubwa huko Liberia katika ulimaji wa zao la mafuta ya mchikichi.

Weah pia ametoa kipaumbele kwa suala la kukarabati miundo mbinu chakavu ya nchi hiyo akisema kuwa barabara ni suhula muhimu kwa ajili ya mawasiliano huku akiwatolea wito Waliberia wanaoishi nje ya nchi kurejea nyumbani ili kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maendeleo ya nchi hiyo.

Chanzo: Parstoday Kiswahili

About Zanzibar Daima 1606 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.