WHO waipatia Wizara ya Afya Zanzibar msaada wa vitendea kazi

Wizara ya Afya Zanzibar imepokea msaada wa vitendea kazi kutoka Shirika la afya ulimwenguni (WHO) ili kuongeza ufanisi katika taasisi za Wizara hiyo.

Msaada huo umelengwa kutumika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja na Kitengo cha Ufuatiliaji mwenendo wa maradhi kilichopo chini ya Wizara ya Afya.

Mwakilishi wa WHO Tanzania Dkt. Mathiew Kamwa alimkabidhi Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo msaada huo na kusema wanathamini juhudi na kazi nzuri inayofanywa na Wizara hiyo na ameahidi kuisaidia zaidi.

Amesema Shirika lake linathamini juhudi kubwa inayofanywa na Wizara ya Afya ya kuwapatia wananchi huduma bora kwa wakati muafaka.

Ameeleza matumaini yake kuwa msaada huo utarahisisha utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo yakiwemo ya ufuatiliaji wa maradhi ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara Zanzibar.

Akipokea msaada huo Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alilishukuru shirika la afya kwa misaada yake inayotoa katika wizara hiyo ambayo inasaidia sana ufanisi wa kazi.

Amemuhakikishia mwakilishi wa WHO kwamba vifaa hivyo vitatumika kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi  yanayoisumbua Zanzibar ikiwemo kipindupindu na kuwapatia wananchi tiba kwa wakati.

Mkurugenzi Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Abdalla amesema WHO na Wizara ya Afya wamejenga ushirikiano wa kufanyakazi kwa pamoja hasa  katika kukabiliana na maradhi ya mripuko.

Baadhi ya vitendea kazi vilivyotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi katika Wizara ya Afya Zanzibar.

Amekumbusha msaada mkubwa wa WHO wakati wa mripuko wa maradhi ya kipindupindu ambapo kutokana na juhudi kubwa za shirika hilo Zanzibar ilifanikiwa kukabiliana na maradhi hayo.

Daktari bingwa wa maradhi ya kuambukiza Dkt. Salma Masauni amesema sehemu ya msaada huo ni maalumu kwa ajili ya Kitengo cha ufuatiliaji mwenendo wa maradhi katika wizara ya Afya ambao ulikuwa unahitajika.

Amesema suala la kufuatilia mwenendo wa maradhi sio kazi nyepesi inahitaji vifaa na nyenzo za kutosha katika kuifanikisha na msaada wa shirika hilo utarahisisha kazi hiyo.

About Zanzibar Daima 1606 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.