SMZ kuwafuta kazi watumishi wote watakaowabagua wananchi

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema haitosita kumfukuza kazi mara moja mtumishi yeyote wa serikali atakayebainika anatoa huduma kwa misingi ya ubaguzi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  wakati alipokuwa akizindua rasmi jengo jipya la Ofisi ya Baraza la Mji la Chake Chake Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za sherehe za Maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Alisema serikali itaendelea kuwahudumia wananchi wake kwa misingi ya usawa bila ya kujali itikadi za kisiasa na kwamba kufanya hivyo kutaiwezesha Zanzibar kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Aidha Balozi Seif alisema Serikali imefanya mageuzi makubwa katika mfumo uitwayo Ugatuzi na kuhamisha majukumu yake katika Serikali za Mitaa kwa lengo la kuimarisha utoaji bora wa huduma mbali mbali kwa wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi Jengo Jipya la Baraza la Maji Chake chake Pemba ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alieleza kwamba wananchi wanapaswa kutambua kuwa kitendo hicho cha kuwapelekea huduma karibu yao  zina lengo la kuimarisha  Utawala wa Demokrasia  hapa Nchini.

Hivyo aliwakumbusha wananchi kwamba Madiwani waliowachagua  wanawajibika kwao wananchi, na pale watakapoona huduma wanazopaswa kupewa haziendi vyema wana haki ya kuwawajibisha, kuwahoji sambamba na kutaka maelezo yatakayowaridhisha huku wakielewa kwamba hiyo ndio maana ya kuimarisha demokrasia.

Akitoa Taarifa za ujenzi wa jengo hilo la Baraza la Mji wa Chake Chake, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Ndugu Khamis Mussa Omar  alisema ujenzi huo ni sehemu ya Mradi Mkuu wa Huduma za Jamii  Zanzibar { ZUSP }.

Ndugu Mussa alisema changamoto ya ujenzi huo ilitokana na ubovu wa Nguzo za asili ambazo Mkandarasi wa Mradi huo alilazimika kujenga upya nguzo hizo na kuongezeka kwa gharama za ujenzi huo zilizofikia asilimia 36.4%.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.