Baraza la Wawakilishi Zanzibar kendelea tena Februari 7,2018

Mkutano wa tisa wa Baraza la tisa la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza  Jumatano 7/2/2018 huko Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Akizungumza na Waandishi wa habari katika ukumbi mdogo wa Baraza hilo, Katibu wa Baraza hilo, Raya Issa Msellem alisema kuwa katika mkutano huo jumla ya maswali 74 yanatarajiwa kuulizwa na wajumbe na kujibiwa na Mawaziri wa Serikali ya Zanzibar.

Msellem alisema kuwa mbali na maswali hayo pia kutasomwa  miswada ya sheria iliyowasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Disemba mwaka jana 2017 na itasomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa katika mkutano huo.

Miswada hiyo ni pamoja na Mswada wa Sheria Nam 2 ya mwaka 1995 ya kusimamia mwenendo wa biashara na kumlinda mtumiaji ya Zanzibar  na kutunga Sheria mpya ya ushindani halali wa biashara na kumlinda mtumiaji, kuweka masharti bora zaidi pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mswada mwengine ni mswada wa sheria ya kufuta sheria ya mwenendo wa jinai Nam.7 ya mwaka 2004 na kutunga sheria mpya ya mwenendo wa jinai na kuweka utaratibu bora  upelelezi wa makosa ya jinai na usikilizaji wa kesi za jinai na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Aidha Msellem alisema kuwa sambamba na hayo pia kutakuwa na ripoti za kamati za kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa mwaka 2017/2018, na taarifa ya wabunge watano (5) wanaoliwakilisha Baraza hilo katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano.

Ripoti nyengine ni ripoti ya serikali kuhusu maombi ya wananchi wa Kisakasaka Zanzibar kuhusu namna wanavyoweza kufaidika kutokana na machinjio ya wanyama yaliyopo maeneo yao.

Kikao hicho cha tisa cha Baraza la tisa la Wawakilishi Zanzibar kinatarajiwa kua cha wiki mbili kuanzia asubuhi ya kesho Jumatano.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.