HABARI

Hii ndiyo hadhi ya Zanzibar kwa mujibu wa Prof. Kabudi

Kupitia kwa Prof. Palamagambah Kabudi, ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,tumepata fursa, kwa mara nyengine tena, ya kudurusishwa kuhusu HADHI na MAMLAKA ya Rais wa Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri wa Sheria na Katiba wa Tanzania, Palamagambah Kabudi

Kwa ufupi tumeendelea kueleweshwa na kufafanuliwa kuwa yule mtu ambaye Wazanzibari, kupitia KATIBA yao ya ZANZIBAR humchagua kuwa Rais wao, Rais huyo huyo, kwa kupitia KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO (ambayo kimsingi sio iliyomuweka Madarakani) hupewa hadhi ya Uwaziri wa kawaida tu katika Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa Zanzibar anakuwa “Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi”, na kwenye Uchaguzi Wazanzibari walimchagua hivyo; kisha anaunda Serkali yake kwa kuteua Makamu wa Rais wawili na anateua MAWAZIRI na anakuwa Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Na Awadh Ali Said

Katika Serikali yaJamhuri ya Muungano wa Tanzania anakuwa Waziri wa kawaida tu. Kwenye hilo Baraza la Mawaziri, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye anaongoza vikao vya Baraza na ikitokezea hayupo, vikao vinaongozwa na Makamo wa Rais; na ikitokezea wote hawapo, vinaongozwa na Waziri Mkuu. Rais wa Zanzibar hadhi yake ni sawa na hadhi ya Waziri wa kawaida tu ambaye kimsingi huwa amechaguliwa kwa utashi wa mtu mmoja tu, yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kifungu cha 54 (1) cha Katiba ya JMT, 1977:

“Kutakuwa na Baraza La Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote”

Kifungu 54 (2):
“Rais atahudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri na ndiye atakayeongoza mikutano hiyo. Na endapo Rais hayupo basi mikutano itaongozwa na Makamu wa Rais na kama wote wawili Rais na Makamu wa Rais hawapo Waziri Mkuu ndiye ataongoza mikutano hiyo”

Wakati Zanzibar inaungana na Tanganyika mwaka 1964, Mkataba wa Muungano ulieleza wazi kuwa Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na iliendelea hivyo hadi mwaka 1994 ambapo hadhi yake ilishushwa kutoka kuwa Makamu wa Rais hadi Waziri wa kawaida. Mwaka 1992 wakati Tanzania inarejesha Mfumo wa Vyama Vingi iliibuka khofu kuwa endapo Serikali za pande hizi mbili zingekamatwa na Vyama tofauti hali hiyo ingeleta “sokomoko” katika mas’ala ya Muungano. Ikaundwa Kamati ya Jaji Bomani ambayo ilipendekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa Mgombea Mwenza ili kama Mgombea akitokea upande mmoja wa Muungano basi Mgombea Mwenza atokee upande wa pili wa Muungano – na kuwa huyu Mgombea Mwenza ndio atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala ya Rais wa Zanzibar.

Lakini pia utata ukaibuka kuwa Rais wa Znz itakuwa ametolewa kabisa katika Mfumo wa Kiuongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ikaamuliwa aingizwe, ila awe Waziri tu. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likarekebisha Katiba kukidhi mabadiliko hayo. Baadhi ya Wazanzibari walilipinga mno hili.

Mnamo mwaka 1995, Wazanzibari 50 wakiongozwa na Bw. Mtumwa Said Haji (Kesi No 2 ya 1995) walikwenda kufungua kesi Tanzania Bara kupinga jambo hili. Kesi yao ilipigwa na chini. Ulipofika wakati wa Mawaziri kula kiapo cha Utiifu na Uaminifu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kukawa na ukakasi kwa Rais wa Zanzibar (wakati huo Dk. Salmin Amour, almaaruf Komandoo) kwenda kula kiapo kwa “Rais mwenziwe”. Utaratibu ukabuniwa kuwa Rais wa Zanzibar ale kiapo cha uaminifu mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwenye Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, namkumbuka Mzee mmoja ambaye alilalamikia hadhi ya Rais wa Zanzibar kwa namna ya kipekee. Alisema huyu ni rais pekee ambaye naye siku ya uchaguzi hupanga foleni kuchagua rais pia, na ni rais pekee ambaye huunda serikali yake yeye akiwa rais, lakini hapo hapo akigeuka upande wa pili na yeye huwa waziri kama hawa mawaziri wake aliowateua. Alishangazwa na utatanishi huu. Lakini huo ndio ukweli tunaoendelea nao  hadi leo, bukheri wa khamsa ishiriin.

Pia leo tumekumbushwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye Mamlaka Makuu kwa Tanzania nzima na kuwa ni sahihi kwake kutoa maagizo kwa Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa vile Yeye ni Mkuu wa Nchi (Head of State) na Yeye ni Amiri Jeshi Mkuu (Commander In Chief).

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mtu huchaguliwa kuwa rais pale anapopata kura nyingi kushinda wagombea wenzake. Hakuna sharti kuwa apate kiwango fulani cha kura kutokea upande wa Zanzibar. Tanzania Bara kuna wapigakura zaidi ya Milioni 20. Zanzibar kuna wapigakura laki 5 tu. Mgombea anaweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kura za Tanzania Bara tu, hata kama KURA ZOTE ZA ZANZIBAR zimemkataa na hakuambulia hata kura moja.

Kwa hakika hasa, kinadharia, mgombea anaweza kushinda bila kura za Zanzibar na anaweza hata asiende kufanya kampeni Zanzibar na akanadi hadharani kuwa hataki kura yoyote kutoka Zanzibar. Ila kwa hali ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,mtu huyu mara tu ashikapo madaraka tumeambiwa anakuwa na uwezo kuamuru wale mawaziri waliochaguliwa na Wazanzibari ambao yeye hawakumchagua. Aliyechaguliwa na wenzetu ana mamlaka juu yetu.

1 thought on “Hii ndiyo hadhi ya Zanzibar kwa mujibu wa Prof. Kabudi”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.