CCM Zanzibar hawana uhalali wa kumshambulia Kabudi

Waziri wa Sheria na Katiba wa Tanzania, Palamagambah Kabudi

Nikiwa Mzanzibari, Mwanasiasa Mstaafu nimeshangazwa mno na lawama anazotupiwa Prof. Kabudi kutoka kwa Viongozi Waandamizi wa CCM Zanzibar, wakiwemo Wawakilishi na hata Mawaziri kufuatia kauli aliyoitoa Bungeni hivi karibuni kutetea MFUMO wa KATIBA zetu mbili. Sitaki kujadili USAHIHI wa kauli yake, na pia niseme kuwa sikushangazwa na Wazanzibari wasio CCM waliopinga kauli ile ya Prof. Kabudi. Mshangao wangu upo kwa hawa CCM Zanzibar.

Prof. Kabudi alianzia kuwa Mwandishi wa Habari, baadae akasomea Sheria na hatimae akawa Mwalimu wa Sheria Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Kwa taaluma mbili hizi zinampa fursa ya kuujua vilivyo Muungano wa Tanzania na hisia za Watanzania wa pande zote mbili za Muungano kuhusu Muungano huu. Zaidi ya yote hivi karibuni alikuwa mmoja kati ya Wajumbe 32 wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (Tume ya Warioba) ambayo kuhusiana na suala la Muungano ilikubaliana na maoni ya Wananchi walio wengi kupendekeza Mfumo wa Serikali 3. Baada ya Tume ile kufikia ukomo wake, Prof Kabudi akishirikiana na waliokuwa Wajumbe wenzake, akina Mzee Warioba, Mzee Butiku, Prof Baregu, Mwanasheria Awadh, Mwanasheria Ali Saleh, Mjumbe Polepole, Mwanadiplomasia Mohd Yussuf na wengineo walifanya midahalo kadhaa kutoa elimu ya Katiba Mpya. Walitumia muda wao. Walifika hadi kuvamiwa na kushambuliwa pale Ubungo Plaza katikati ya Mdahalo. Nawakumbuka sana juhudi waliyochukua kutetea maoni ya Wananchi, walizunguka Nchi nzima. Prof. Kabudi akitetea Rasimu ya Warioba hadi kipovu kinamtoka.

Nakumbuka pia kuwa waliokuwa mstari wa mbele kuipinga Rasimu ile ya Serikali 3 walikuwa ni CCM Zanzibar. Waliipinga Rasimu ile tokea kwenye Mabaraza ya Katiba hadi kwenye Bunge la Katiba kule Dodoma.

Kule kwenye Bunge La Katiba Dodoma, CCM Zanzibar wakiongozwa na Balozi Seif Ali Iddi, Maalim Haroun, Mohd Aboud n.k walikuwa wanapigilia msumari kuwa TUBAKI KAMA TULIVYO na KATIBA ZETU MBILI na SERIKALI ZETU mbili kuelekea MOJA. Huku nje Prof. Kabudi na wenzake wanasisitiza kuwa MFUMO huu umeshindwa kutupa Muungano wenye kutoa hadhi na haki sawa kwa Washirika wa Muungano. Akina Haroun na Mohd Aboud wakali hawakamatiki !!! Wanataka tubaki kama tulivyo. Na CCM Zanzibar nayo imoto hadi kufikia wakati wa kumdhalilisha Spika Kificho hadharani kwa kumtaka akanushe Maoni ya Baraza La Wawakilishi yaliyotaka Serikali 3. Kificho akaukana Waraka aliousaini mwenyewe na ambao aliusoma mwenyewe mbele ya Tume ya Katiba herufi moja baada ya nyengine hadi akaumaliza. Idhilali ilyoje !!!

CCM Zanzibar walimsaliti na kumtosa hata Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Ndg Othman Masoud ambaye alisimama kidete kupigania maslahi ya Zanzibar kwa ujasiri usio kifani. Ilibidi atolewe katika Ukumbi wa Bunge chini ya ulinzi mkali kunusuru usalama wake. Wakafurahi kuwa wamemdhalilisha. Mungu si Athumani, leo wanadhalilika wao mbele ya kadamnasi ya watu kuyapinga yale yale waliyoyapigania.

Sasa leo alichofanya Kabudi ni kuyasema Bungeni yale ambayo CCM Zanzibar waliyapigania kule Dodoma kwa nguvu kubwa. Wao wakisema Katiba zetu hazina mgongano. Wakitetea Muungano wa Serikali 2. Walikubali Rais wa Zanzibar abaki kuwa Waziri tu katika Serikali ya JMT. Sasa leo nadhangazwa eti hawa hawa akina Maalim Haroun na Mohd Aboud kupingana na Kabudi. Alichofanya Kabudi ni kuungana na wao kuyasimamisha yale waliyoyapigania kule Dodoma. Si ajabu Yeye kaona afuate ule msemo maarufu kuwa “If you cant fight them, join them”

Mimi nitawaelewa Wazanzibari wengine wote wanaompinga Kabudi ; ila kwa CCM Zanzibar na hasa hasa hawa akina Haroun na Mohd Aboud na Balozi Seif Ali Iddi nikiwaangalia nachanganyikiwa. Wao walikuweko Dodoma, wakapigana vita vikubwa kuwa Zanzibar ibaki kama ilivyo ndani ya Muungano huu. Wakashinda na wakarudi na ushindi. Wakapongezana. Leo Kabudi kasema kipi ambacho ni kigeni kwao?

Naomba kwa Mwenyenzi Mungu atubainishie ugonjwa walionao Ndugu zetu hawa. Tuseme ni ule ugonjwa wa BT (Bora Tumbo) tu? Basi gonjwa hili ni janga kubwa.

Tanbihi: Makala hii imeandikwa na mtu aliyejitambulisha kama Mwanasiasa Mstaafu

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.