Ni aibu kwa SMZ kutomtambua mshindi wa fasihi Ali Hilal

Yapata miaka miwili sasa tokea nipate kumjuwa Ndugu Ali Hilali Ali, nilishawishika kuomba urafiki kupitia mtandao wa ‘facebook’ kutokana na michango na elimu yake anayotoa kwa jamii kupitia ukuta wake huo, kutokana na uungwana wake mkubwa hakusita kukubali ombi langu na toka hapo tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara kupitia kuta zetu ingawa bado hatujabahatika kukutana uso kwa macho.

Kabla sijenda mbele zaidi ni nyema kwanza japo kwa kifupi historia fupi niliyo nayo juu ya kijana Ali Hilal, ili nikiingia katika kiini cha makala hii uone kwamba kile ninachokikusudia kukitetea kina uhalali wa mia kwa mia.

Jina lake kamili na sahihi ni Ali Hilal Ali, amezaliwa katika kijiji cha Kalani kilichopo katika wilaya ya Mkoani iliyopo katika Mkoa wa Kusini Pemba, Ndugu Ali Hilal kwa sasa anaishi Wete, wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba. Alianza safari yake ya elimu katika skuli ya Jadida Wete Pemba mnamo mwaka 1997 hadi 2003.

Alifaulu darasa maalum (Michepuo) na kujiunga na Elimu ya Sekondari mwaka 2003 katika Chuo cha Kiislam (CCK) kilichopo Kiuyu Wilaya ya Micheweni Pemba, ambapo alikuwa akisoma masomo yote ya sayansi na sanaa ( Science & Arts subjects), baadae mwaka 2008 – 2010 Ali Hilal aliendelea na masomo ya Kidato cha sita ndipo akaamua moja kwa moja kujikita katika masomo ya sanaa akachukua masomo ya Historia, Kiswahili na Kiingereza.

Ali baada ya kufaulu vizuri kidato cha sita ndipo mwaka 2010 hadi 2013 akajiunga na Chuo kikuu cha Usimamizi wa Fedha Tanzania (IFM) na amefaulu vyema shahada ya kwanza katika masomo ya Sayansi ya Hifadhi ya Jamii ‘Bachelor of Science in Social Protrction (BScSp).

Ali Hilla aliingia katika tasnia hii ya uandishi tangu mwaka 2011 akiwa Chuo Kikuu – IFM, alianza kuandika katika ukuta wake wa ‘facebook’ ndipo baada ya kuona kwamba kuna haja ya kuzikusanya kazi zake, ndipo akaamua kuziweka pamoja na kwa sasa ana riwaya zisizopungua 5 na katika hizo ni moja tu ndio ambayo ameshaichapisha.
Kwa utangulizi huo basi sina chembe ya shaka kwamba umepata picha halisi wewe msomaji wa makala hii, kwamba kijana Ali Hilal ni kijana halali wa visiwa vyetu vya Zanzibar.
Ali Hilal, kama walivyo wasanii wengine na yeye ni msanii, ambapo tofauti yao ni aina ya sanaa aliyojichagulia, wengine wamechagua sanaa ya muziki, maigizo na kadhalika, lakini yeye amechaguwa kuonyesha kipaji chake cha sanaa kwa kuingia katika uandishi wa riwaya na mashairi.

Licha ya kuwa nchi yetu imo katika Muungano wa Tanzania, lakini Zanzibar ina serikali yake ambayo inasimamia mambo yake yanayohusu Wazanzibari na Uzanzibari wao, na muungano huu ulipoundwa umeorodhesha mambo yanayohusu Muungano na yale yasiohusu muungano, na miongoni mwa mambo yasio ya muungano ni pamoja na sanaa, utamaduni na michezo.

Kinachonisikitisha na kunishangaza na kunisukuma hadi kuamua kuandika makala hii ni ule ukimya, ububu na uziwi wa Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa kimya katika jambo hili, jambo ambalo ni haki yake kikatiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar.

Ndugu Ali Hilal ameiwakilisha vyema nchi yetu katika mashindano hayo ya Kimataifa ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika ya mwaka 2017 yanayoandaliwa na Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani kwakushirikiana na Kampuni ya ALAF Ltd yaliyofanyika jana Januari15, 2018 mjini Newyork, na Ali Hilal Ali ameshinda tuzo katika kipengele cha uandishi wa Riwaya, kwa riwaya yake iliyobeba jina la ‘MMEZA MFUPA’.

Yapata muda wa mwezi mzima sasa, hadi leo hakuna taasisi yeyote ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, serikali ambayo ina Wizara nzima inayosimamia masuala ya Sanaa, hata zile taasisi nyengine ambazo zinahusika na sanaa na lugha ya kiswahili pia viko kimya kama kwamba Zanzibar haihusiki na Ali Hilali au Zanzibar haihusiki na kiswahili na sanaa.

Chakushangaza Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii Tanzania ambayo kimantiki na kiuhalisia wa kikatiba haihusiki na masuala ya Zanzibar kwa kuwa Habari, Utamaduni, sanaa na michezo si mambo ya Zanzibar, lakini imempongeza Ndugu Ali Hilali kwa kushinda tunzo hio ya ‘Mabati – Cornell’ kupitia waraka wake uliosainiwa na Waziri Dkt. Harrison Mwakiembe, sishangai Dkt. Mwakiembe kufanya hivyo kwa kuwa amefanya kwa kigezo cha uraia, kwa sababu kila Mzanzibari ni mtanzania ingawa si kila Mtanzania ni Mzanzibari.

Wakati Dkt. Mwakiembe akimpa Ali Hilal haki yake ya uraia kwa kumpongeza huku kwetu Zanzibar Wizara ya Habari, Utalii, utamaduni na Michezo, Idara ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (Suza), Baraza la Sanaa na hata Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wako kimya, kama kwamba Ali Hilal hakuiwakilisha Zanzibar katika mashindano.

Sasa hapa ndipo nnapojiuliza kwa kitendo cha SMZ na taasisi zake husika zimeshindwa kumtambua Ali Hilal aliyeiwakilisha vyema Zanzibar kwa kushinda tunzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika ya mwaka 2017, ni kweli ina nia ya kukikuza Kiswahili?

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ali Mohammed Ali.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

1 Comment

  1. Naam asanye sana mwandishi Ali Mohammed na HONGERA mwenetu Ali Hilal. Ama ksa SMZ wanazidi kutuaibisha kwa ukimya wao, nawaambia welewenu vingwele. Waandishi, wasanii nk wengi wa fani na vipaji, HAWANA HADHI YOYOTE mbele ya SMZ au baraza la wawakilishi. Lakini historia itawahukumu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.