Wawakilishi Zanzibar walilia fedha za mfuko wa jimbo

Mwakilishi wa jimbo la Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma amesema kitendo cha Serikali kutowapatia Wawakilishi wa Majimbo fedha za Jimbo kwa kipindi kirefu sasa ni njia moja wapo inayokwamisha upelekaji wa maendeleo katika Majimbo husika.

Mwakilishi huyo ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar wakati akichangia Ripoti ya kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi.

Amesema kuwa tokea kuchaguliwa kwao kushika nafasi hizo wamepokea fedha za Jimbo awamu moja nazo ni Shiling milioni 20, ila hadi sasa hakuna fedha nyengine ambazo wamezipata ili kuhudumia majimbo yao kama utaratibu wa fedha za jimbo ulivyo.

“Tunasikitika sana kuona wenzetu Wabunge wanapata fedha kila kipindi lakini sisi baada ya mara moja tu hakuna tena hadi leo hali hii inasikitisha sana na kurudisha nyuma maendeleo”alisema Juma.

Aidha ameongeza kuwa kitendo hicho kimeanza kuleta sitofahamu mbali mbali majimboni kutokana na baadhi ya wananchi kutoamini kama Wawakilishi wao bado hadi leo hawajapatiwa fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya majimbo yao.

Hivyo Hamza ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha kulipatia ufumbuzi wa haraka suala hilo kwa kuwapatia fedha hizo ili lengo la kuhudumia wananchi Majimboni kupitia fedha hizo liweze kutimia kwa wakati uliopangwa.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amesema kuwa pamoja na maoni na vilio vingi vya wajumbe wa Baraza hilo ila taarifa kamili juu ya michango ya wajumbe hao itatolewa mwezi wa tisa kama ulivyo utratibu wa Serikali.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.