HABARI

Riwaya: Safari ya Kumuua Rais – 1

“Hali ya hewa unaiyonaje? , Talib alimuuliza Abdull, huku akimtazama usoni mkononi ameshika chupa ya maji akishushia kooni kukata ukali wa kiu.

“Huku kunaonekana ni joto kidogo”, alijibu , macho yake yakipishana na mandhari ya majani ya kijani yanayovutia , kupitia dirisha la kioo cha basi la abiria walillokuwa wanasafiri.

“Leo nimemkumbuka sana Fartuun”, kisha alisema Abdull,  huku  ikinamisha kichwa kuashiria kuna jambo analitafakari zaidi.

“Achana na hayo mawazo..ngoja tumalize kazi yetu kwanza…ikimaliza urudi kweli kwani anakusubiri ”.

Abdull ni kijana aliyekuwa mwanzoni mwa mwaka wake wa 27 tangu kuzaliwa akiwa na  urefu wa futi tano na nchi kadhaa, ngozi yake ikibeba  rangi ya mchanganyiko wa weupe na weusi, tabia yake ya upole na aibu kidogo vilimpendeza kila mmoja.

Talib ni kaka wa Abdull, yeye anakaribia  kutimiza miaka 30, ngozi yake ni nyeupe kidogo kuliko Abdull lakini Abdull ni mrefu kidogo kuliko kaka yake.

“Kazi ikimaliza inabidi tuende Dubai kidogo ili ukarudishe hali”, alisema Talib kumwambia Abdull huku akimbinya kwa utani katika paja lake na wote wakatabasamu.

Abdull alikuwa kakonda kidogo, ingawa awali alikuwa na mwili uliojaza vizur tu na kifua kipana.

Baada ya jua kuwaka sana, mwisho anga ikafunikwa na mawingu,  ni saaa kumi na moja na dakika kadhaa jioni, likiwa limebaki saa moja na nusu kabla ya basi lile kuingia katika jiji la Dar es Salamm.

Ni mwaka 2008 wote waili walikuwa wanatokea Dodoma ambako Talib alienda kumchukua ndugu yake huyo  katika hospitali ya wagonjwa wa akili, ni mwaka mzima umepita tangu Talib ampeleke Abdull huko.

Na Rashid Abdallah

Jioni ile waliingia katika jiji la Dar es Salaam, manyunyu ya hapa na pale yalikuwa yakiendelea kushuka, walichukua taxi hadi maeneo ya Posta,  foleni ilikuwa kubwa mno huko njiani, lakini walipofika posta walienda  katika hoteli moja maarufu jijini kwa ajili ya mapumziko.

Baada  ya kuoga nakupata chakula katika mgahawa wa hoteli, walirejea chumbani,  muda ukiwa unakaribia saa nne kasoro usiku. Talib alifungua mkoba wake huku Abdull akiwa amesimama katika dirisha la kioo la chumba kile, akiangalia mandhari  ya kuvutia ya bahari ya Hindi.

Ghafla Talib alimsogelea Abdull akiwa ameshika karatasi mkononi .

“Unaona hiki! Ndicho cheti chako..”

Kilikuwa ni cheti kinachomtambua Abdull kwamba ni mgonjwa wa akili rasmi.

Alikishika na kuanza kukisoma, huku Talib akiwa anarudi mkobani kwake.

“Inabidi hicho tukitunze kwa makini…ndio kila kitu katika issue hii”, alinena Talib.

“Sawa , hakuna shida kaka”

Baada ya dakika kadhaa wote walirudi kitandani na kupata usingizi  fofofo kutokana na machofu waliyokuwa nayo. Waliamshwa na miale membamba ya jua iliyokuwa inapiga dirishani kwao, kwani  usiku ule walisahau kulifunga dirisha.

Lakini jua  halikudumua kwa muda mrefu. Hali ya hewa ya Dar es Salaam ilikuwa ya mvua na baridi kwa siku mbili. Mitaa ilijaa maji, uchafu ukazaga.

Mchana ulipoingia walikuwa katika mitaa ya  Kariakoo wakiruka dimbwi hili na lile ya maji, wakiingi madukani ili kujitafutia mahitaji yao kabla ya safari ya kuelekea Zanzibar.

Kwa Abdull ilikuwa ni mara yake ya pili  katika jiji la Dar es Salaam, mara ya mwanzo alikuja na marehemu Baba yake akiwa mdogo wa miaka sita au mitano tu.

Ndugu hawa wawili, walikaa hotelini  takribani siku tatu, wakitembea katika jiji la Dar es Salaam ingawa mvua zilikwamisha baadhi ya safari zao.  Siku ya nne ndipo walipoanza safari ya kuelekea katika kisiwa cha Unguja.

Jambo la kushangaza ni kwamba mara baada  ya Abdull kushuka katika taxi ambayo ndio iliwapeleka uwanjani wa ndege, hali yake ilibadilika akaanza kuonekana kama kijana asiyejitambua.

Kaka yake alimshika mkono kana kwamba anaelewa nini kinaendelea na kuanza kutembea naye kuelekea katika majengo ya uwanja wa ndege, hata yule dereva taxi alishangaa kidogo lakini akapotezea akiamini pengine kapata ugonjwa wa ghafla.

Walifika Zanzibar saa moja za jioni, walichukua taxi hadi Mji Mkongwe ambapo huko ndiko walikoandaa makaazi  yao.

Ni katika eneno la Vuga, Mji Mkogwe katika jengo la ghorofa lililo pembezoni mwa Barabara ya Vuga. Walikodi vyumba viwili na sebule, kukiwa na jiko na chooni pia.

Hadi wanafika nje ya mlango Abdull bado alionekana ni mtu ambaye kachizika kiakili, lakini mara tu baada ya kuingia ndani akarudi katika hali yake ya kawaida.

Talib alikuja Zanzibar wiki kadhaa nyuma kwa lengo la  kuandaa makazi yao, aliamua kukodi vyumba katika ghorofa ile kwa sababu barabara ile ingewarahisishia kwa kazi maalum iliyowaleta katika kisiwa cha Unguja.

Mara walipoingia tu Abdull alikimbilia dirishani kuchungulia, kisha akamtolea ishara ya dole gumba kaka yake, dalili za kwamba amewafiki uwamuzi wake wa kuchagua jengo na chumba kile.

Siku zilianza kukatika na maisha mapya ya Abdull ambaye aliishi kama mgonjwa wa akili huku Talib akiishi kama mtu wa watu katika jamii ya watu wa mji Mkongwe. Yote haya walikuwa wanayafanya kwa sababu ya kujua nini kimewaleta katika kisiwa cha Unguja.

Talib alijitahidi kutengeneza mtangamano mzuri na wa kweli na jamii ya watu wa pale, hili kwake lilikuwa ni jambo muhimu sana.

Talib alikuwa hakosekani katika shughuli za kijamii katika eneno la Vuga, michango kwa wenye shida, hadi jamii ikampenda na kupindukia kumpenda,  alikuwa ni kijana aliyependeza kwa tabia kwa kila aliyemjua.

Wazee wengi walikuwa wanamuweka kitako Talib na kumshawishi ili wamuoze binti zao, lakini mara zote alikuwa anatakaa kwa sababu hakutaka kumuingiza binti wa mtu katika matatizo,kwa sababu ya siri iliyojificha ya maisha yao.

“Unajua saivi nimeshakuwa rafiki mkubwa na sheha wa shehia hii”, Talib alikuwa anamueleza Abdull.  Zilikuwa ni nyakati za jioni ya saa tatu wakiwa wametandika busati wakipata chakula chao cha mwisho.

“Hahahaha! Wote waliangua kicheko, huku wakisukuma tonge moja moja vinywani mwao.

“Hodi” Ghafla walisikia sauti mlangoni kwao. Walishtuka kidogo na haraharaka Abdull akakimbilia chumbani na sahani yake akimuacha Talib akienda kusikiliza hodi hiyo.

Baada ya dakika kadhaa alirudi na Abdull akatoka ndani; alikuwa ni Mama mmoja jirani yao, aliyekuja kuwapa taarifa kwamba uniti za umeme zinakaribia kuisha.Talib alirudi akiwa tayari ameshampa pesa za kununulia hizo uniti.

Hodi ile iliwashitua sana kwani hawakuwahi kumleta mtu ndani mwao ,ni mwiko kuingi mtu katika nyumba yao, wala hawakuwahi kugongewa hodi na mtu yeyote, kila mmoja katika mtaaa ule alielewa kwamba ni mtu na mdogo wake ndio wanaishi mule,  ambapo mmoja ni mgonjwa wa akili, lakini hakuna aliyethubutu kuisogelea nyumba ile.

Maisha yaliendelea kusonga na umaarufu na ukarimu wa Talib uliongezeka sana, hakuwa anakoseakana katika maskani maarufu mji Mkongwe hasa ile ya  Jaw’s Corner, akienda huko kucheza bao na kuwanunulia kahawa wana maskani wenzake  baadhi ya siku.

Hadithi za siasa za CUF na CCM hazikuwa zinampita, hadi akawa msemaji pendwa zinapokuja hadithi hizo.

Pesa halikuwa jambo gumu kwa ndugu hawa wawili, ndio maana Talib hakutaka hata kufanya kazi,wapo wachache waliokuwa wakijiuliza vipi maisha yanawaendea vizuri lakini hawana kazi.

Lakini hakuna aliyewahi kuthubutu kumuuliza Talib swali hilo, kila mmoja aliamini sio swali muhimu kwasababu katika mji  kila mtu na  maisha yake, Ilimradi haonekani kuiba au kukaba.

Miezi ilikatika, Abdull akabaki kuwa  mgonjwa wa akili aliyezoeleka katika eneo lote la Vuga, tangu watoto wadogo wanamuogopa hadi wakamzoeya. Mingi ya mitaa na chochoro za  Mji Mkongwe alikuwa anaijua kwa upana na urefu wake, tangu siku za mwanzo akipotea hadi mwisho akawa mwenyeji.

Hakuacha kuokota okota vyakula, kusema peke yake na kupenda kukaa peke yake kama mkiwa. Bustani ya Forodhani  ni moja ya sehemu aliyoipenda sana, mara kwa mara huenda ili  kuvuta upepo safi wa bahari ya Hindi.

Abdull hakuona tabu kukaa kutwa nzima katika baraza za majumba mabovu ya Mji Mkongwe , kuvaa nguo chafu wakati mwengine, mara nyingi alikuwa anaonekana kukunakuna kichwa  na kukitikisa ingawa alikuwa mpole kwa kila mtu.

Zipo siku ambazo huzurura katika vichochoro hadi jua linazama, kisha hulala vibarazani , ima hufika asubuhi au hupata mtu wa kumchukua na kumrudisha Vuga anakoishi.

Hakuwahi kuyachoka maisha haya, ingawa alikuwa na akili zake timamu lakini aliamini ndio njia sahihi kupitia ili kukamilisha kiapo chao.

Siku moja jioni  Abdull alikuwa katika kingo za bustani ya Forodhani akibarizi na kuangalia mawimbi ya bahari yanavyokuja na kurudi, pembezoni kukiwa na watoto wanaruka na kuogelea.

Mandhari ile ya bahari, fukwe na vyombo vingi vya usafiri, yalizivuta fikra zake na kuzirudisha Mombasa  Kenya katika fukwe za nzuri za mji wa Nyali. Ni mji wa kitalii uliopo pembezoni mwa bahari ya Hindi.

Fikra zake zilirudi nyuma hadi  siku za mwanzo za mwezi wa pili mwaka 2001, pale  Abdull na Talib walipokimbia kwa jahazi kutoka katika kiswa cha Pemba na kukimbilia Mombasa, wakaingia katika jiji hilo la mwambao wa bahari ya Hindi kupitia mji huo wa Nyali.

Walikuwa na wakimbizi wengine wengi tu kutoka katika kisiwa cha Pemba lakini walipoingia Mombasa  kila mmoja akapotelea upande wake, Abdull na Talib wakiwa vijana wadogo wakabaki wakiwa.

Fartuun ni nani? Kwanini ndugu wawili wanaishi maisha ya kuigiza kisiwani Unguja? Kuna nini nyuma ya pazia la maisha ya ndugu hawa? Kipi kilichowakimbiza Pemba? Usikose wiki ijayo…                                   

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.