Wabunge CUF kwenda mahakamani kuhusu FIFA

Wabunge wanaowakilisha Chama cha Wananchi (CUF) bungeni wanasema kwamba watakwenda mahakamani kusaka majawabu juu ya masuala kadhaa ya michezo, likiwemo la “uhalali wa kikatiba wa Shirikisho la Soka la Tanzania Bara (TFF)” na “tafsiri wa Waziri wa Michezo wa Tanzania Bara kutumika kama ni Waziri wa Muungano ndani ya nchi na nje ya nchi.”  Zaidi soma taarifa ya wabunge hao kwa vyombo vya habari waliyoitoa hivi punde.

MKUTANO BAINA YA WABUNGE WA CUF NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UJIO WA RAIS WA FIFA TANZANIA ULIFANYIKA KATIKA OFISI ZA WABUNGE WA  CUF DAR ES SALAAM –  FEBRUARI 21, 2018 OFISI YA CHAMA MAGOMENI
Waheshimiwa Wana HabarI
Kama tujuavyo Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA atawasili nchini Tanzania kwa ajili ya mkutano maalum wa taasisi hiyo na jiji la Dar es salaam na nchi hii kupewa heshima ya kuwa mwenyeji.
Tunaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini hasa Shirikisho la Soka Tanzania TFF kwa kuaminiwa na taasisi hiyo muhimu na kubwa duniani nah ii ni heshima kubwa kwa nchi yetu ya Tanzania.
Tunataraji au pia ni matumaini yetu kuwa FIFA watafurahia maandalizi na hata huduma na ukarimu wa Watazania katika kuwa mwenyeji wa mkutano huu, kiasi cha kuishawishi FIFA na hata mashirikisho mengine ya michezo duniani yaweze kushawishika kuleta shughuli zake nchi sio tu kwa kuiongezea sifa nchi yetu lakini pia kukuza utalii na fursa za matangazo na biashara.
Waheshimiwa Wana Habari
Mtakumbuka mwaka jana Zanzibar ilipewa uanachama Namba 55 wa Shirikisho la Soka la Afrika CAF na wengi tukatumainia kuwa hio ilikuwa ni chachu na njia ya kuelekea kuukwaa uanachama wa FIFA, ambayo ndio kiu kubwa ya Wazanzibari.
Sisi Wabunge wa Wananchi tulifurahia sana tukio hilo na baadhi yetu tuliongoza kampeni kubwa tulioyofanya miongoni mwa viongozi wa mashirika mbali mbali ya soka Barani Afrika hasa kwa njia ya mtandao na baadhi kuzungumza nao. Walituelewa kama walivyoelewa juhudi za wenzetu wengine kama Chama cha Soka cha Zanzibar lakini hasa Shirikisho la Soka la Tanzania na Serikali zetu.
Ila ile ilikuwa kama kiini macho au ndoto vile. Ndani ya muda mdogo CAF hiyo hiyo ikafuta uanachama huo katika uamuzi ambao mpaka leo haukuwekwa wazi kueleweka na pia kukiwa hakuna njia ya kuhoji jambo hilo. Hiyo ikawa na maana pia safari ya FIFA ikazimika tena.
Zanzibar kama mjuavyo imejaribu mara kwenda moja kwa moja kujaribu uanachama FIFA ikiwa ni 2001, 2005 na 2010 lakini kisiki kikawa ni kile kile kimoja kwamba Zanzibar si nchi (State) na si mwanachama wa Umoja wa Mataifa na sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hivyo haina hadhi ya kuwa mwanachama. Hiyo ni pamoja na TFF kuwa upande wa Zanzibar. FIFA imekataa kulisikia hilo mpaka leo.
Sisi Watanzania tunajua kuwa suala la michezo si la Muungano na hivi tusemavyo kuna Waziri kila upande, kuna Baraza la Michezo kila upande, kuna vyama vya michezo kila upande pamoja na kuwepo TFF yenye mamlaka ya Tanzania Bara tu na ZFA yenye mamlaka ya Zanzibar tu.
Ila kwa sababu TFF kwa hila na mbinu, wakati ikijua kuwa mamlaka yake (mandate) ni ya Tanzania Bara kwa sababu ni shirikisho linalojumuisha vyama vya mikoa ya Bara tu, bado TFF imejibebesha jukumu visivyo halali kuiwakilisha Tanzania, yaani Tanzania Bara na Zanzibar, bila ya idhini wala uhalali wowote kutoka Zanzibar.
Ndio kwa maana hiyo FIFA hawatuelewi. Na zaidi hawatulewi kwa sababu TFF wamechukua na kulivaa jina TANZANIA ambalo ni letu sote, lakini linatumiwa na upande mmoja visivyo halali kikatiba na kwa mujibu wa Hati ya Muungano.
Kisha Waziri wa Katiba na Sheria – nasita kumwita wa Muungano maana na kule kwetu Zanzibar tunae wetu- anasema kuwa hakuna mgongano wowote wa baina ya Katiba ya Zanzibar na Tanzania  au usahihi ya Tanzania Bara.
Sitaki nikuchukue nikakuchosheni kwenye darasa la kikatiba lakini mkwamo huu unatokana na muundo wetu wa Muungano, ingawa kuna nchi kadhaa zenye utata zaidi wa utaifa wao na muundo wao lakini bado zimekuwa ni wanachama wa FIFA.
Ikiwa FIFA kwa mfano inasema kuwa kigezo ni kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) basi takwimu zinaonyesha kuwa nchi wanachama wa UN ni…ambapo zile wanachama wa FIFA ni…. Na kwa hivyo FIFA imechukua nchi kadhaa ambazo hazina sifa hiyo.
Iwapo Zanzibar ina kosa uanachama wa FIFA kwa sababu ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano na haina miguu yake wenyewe (legal standing) basi mbona zipo nchi nyingi tu ambazo si dola lakini ni wanachama wa Shirikisho hilo la dunia?
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Sisi Wabunge wa Wananchi tunathamini juhudi zinazochukuliwa kuipigania Zanzibar lakini kuna msemo wa Kiswahili unaelekeza ukibwebwa ujikaze na pia mwengine unaosema mshike mshike na mwenyewe uko nyuma.
Kwa sababu hiyo basi pamoja na mazungumzo ambayo yatafanywa kuendelea kuishawishi FIFA ielewe hali ya Zanzibar basi na sisi tumeona pia tupaze sauti zetu hasa kwa sababu viongozi wa FIFA wapo nchini lakini zaidi kwa sababu Rais wa Taasisi hiyo muhimu yupo nchini.
Isitafsirike kuwa tuna viza juhudi zinazofanywa ila ieleweke ni kuongezeana nguvu au kulitia mwega suala hili ambapo sisi tumeandika BARUA YA WAZI kwenda kwa Rais wa FIFA ambaye atakuwepo hapa nchini. Maana iwapo amefika nchini na hakupata ujumbe moja kwa moja kutoka na wanaochomwa na msumari wa kiatu, tutakuwa sisi wenyewe hatujafanya wajibu wetu.
Mbali ya barua hiyo kumueleza mifano mingi ya nchi zilizokubaliwa uanachama tutamwambia kwenye barua hiyo mambo yafuatayo:
1.    TFF haiwakilishi maslahi ya Zanzibar
2.    Mamlaka ya TFF hayajawahi wala hayafiki Zanzibar
3.    Muundao wa TFF ni kuwa ni vyama vya mikoa wakati ZFA ina mikoa yake
4.    TFF haijawahi kuwa na sera ya maendeleo inayoihusisha Zanzibar
5.    TFF inasimamia Kilimanjaro Stars na kuifanya ni timu ya Taifa Stars
6.    Hakuna kikao chochote cha kikatiba baina ya TFF na ZFA
Tutakuwa na mengine mengi lakini pia tutamwambia juu ya hatua ambazo Wabunge wananchi tutazichukua ili suala hili lipate fusa inayostahiki kusikilizwa kwa kufanya yafuatayo ambayo yana nia ya kuitisha mgogoro wa kikatiba ili kupata suluhu ya kweli na ya kudumu:
1.    Kwenda Mahakamani kutafuta uhalali wa kikatiba wa chombo cha TFF kufanya kazi ya Muungano na iizuie TFF kufanya kazi yoyote mpaka uamuzi wa Mahakama shauri hilo limalizwe
2.    Katika hilo pia tutaiomba Mahakama itupe muongozo juu ya kwa nini pasiwepo Chama cha Soka cha Tanzania Bara
3.    Kutafuta tafsiri wa Waziri wa Michezo wa Tanzania Bara kutumika kama ni Waziri wa Muungano ndani ya nchi na nje ya nchi
4.    Kutoa Hoja Binafsi Bungeni kuhusu mustakbali ya michezo chini ya utaratibu tata uliopo hivi sasa
Tunaamini bila ya kufika hatua hiyo hapatakuwa na suluhu kwa sababu hali hii imeendelea kwa muda mrefu na tumekuwa tukjificha kama mbuni kufanya kama kwamba sababu ya Zanzibar kukosa uanachama wa FIFA haitokani na Muungano na muundo wake.
Tunakushukuruni waandishi kwa kutusikiliza
Ally Saleh (MB)
Mnadhimu wa Kambi ya CUF Bungeni
About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.