Nassor Mazrui
HABARI

CUF yatoa kauli rasmi ziara ya Lipumba kisiwani Pemba

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Nassor Ahmed Mazrui, kimeikanusha vikali barua iliyotolewa na jeshi la polisi mkoa wa kusini Pemba, likidai kupokea barua ya CUF kuridhia kufanyika kwa kongamano kwenye ukumbi wa Makonyo, Chake Chake kisiwani Pemba hapo kesho (Jumamosi, 24 Februari 2018).

 

Hii hapa chini ndiyo taarifa rasmi ya CUF iliyotolewa na Mazrui:

“CUF – Chama cha Wananchi kimepokea taarifa ya ujio wa Ibrahim Lipumba kisiwani Pemba siku ya Jumamosi tarehe 24 Februari 2018, kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chake Chake Pemba kwa barua yake ya tarehe 23 Februari 2018 kwa Ofisi ya Wilaya ya CUF Chake Chake.

Makao Makuu ya CUF Zanzibar haijapeleka barua yoyote kuhusu ujio wa Lipumba kwa Jeshi la Polisi kama inavyodaiwa na barua hiyo ya Polisi.

CUF – Chama cha Wananchi kinatambua kuwa Lipumba sio kiongozi na wala sio mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa rasmi na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

Chama cha Wananchi – CUF kinaamini kuwa ziara hiyo ni uchokozi wa makusudi unaofanywa na kibaraka Lipumba akishirikiana na Jeshi la Polisi.  Ziara hii imekuja baada ya kufeli Jaribio la uvamizi wa Makao Makuu ya CUF Mtendeni ambalo lilikuwa na dhamira ovu sana kwa Chama.

Lengo la ziara hii ni kuwafanya wananchi, kama lilivyokuwa lile la uvamizi wa Makao Makuu Mtendeni, kututoa katika kupigania haki yao ya Ushindi Mkubwa iliyoporwa baada ya Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015.

Chama cha Wananchi-CUF  kinawataka wanachama, viongozi na wapenzi wa CUF waliopo Pemba kuwa watulivu kuendelea na shughuli zao za maisha za kawaida na kupuuza kabisa ujio huo wa Lipumba.

Kama tulivyoshinda uchokozi wa kuvamiwa Makao Makuu Mtendeni tukashinde tena kwa kutokukubali kutolewa katika mstari kupitia uchokozi huu anatumiwa kibaraka Lipumba kupitia ziara yake hii ya Pemba.”

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.