La Prof. Kabudi, Zanzibar na Mtego wa Komba – III

Katika sehemu ya pili ya uchambuzi huu, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Othman Masoud, alianza kuvichambua vifungu vya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa kwa shangwe na kutetewa na wana-CCM wa Zanzibar mjini Dodoma. Kwenye sehemu hii, anaendelea kuvichambua vifungu hivyo. – Mhariri.

 Mfumo wa Serikali Mbili [Ibara ya 73]

Ibara ya 73 ya Katiba Inayopendekezwa imeweka bayana mfumo huo. Ibara ya 75 imeweka bayana zaidi kuwa Serikali ya Muungano itasimamia mambo yote ya Muungano kwa Jamhuri ya Muungano yote na mambo yasiyo ya Muungano kwa Tanzania Bara.  Mambo muhimu ya kuzingatia katika ibara hii ni kama yafuatayo:

 1. Ibara ya 112 inaeleza kuwa mamlaka ya kuamua juu ya sera zote ni ya Serikali ya Muungano;
 2. Ibara ya 114 inayohusu muundo wa Baraza la Mawaziri, ukiachia Rais wa Zanzibar hailazimishi kuwe na Waziri kutoka Zanzibar katika Baraza hilo;
 3. Katika uteuzi wa Waziri Mkuu chini ya ibara ya 110 haulazimishi kushauriana na Rais wa Zanzibar;
 4. Katika uteuzi wa mawaziri chini ya ibara ya 115, Rais wa Muungano anashauriana na Makamu wa Kwanza na Waziri Mkuu lakini Rais wa Zanzibar ambaye ni Makamu wa Pili hahusiki katika uteuzi;
 5. Hakuna ibara inayoweka utaratibu wa namna ya kuihusisha, kuishauri au kuishirikisha Zanzibar katika kufanya maamuzi yoyote yanayohusu masuala ya Muungano;
 6. Hakuna mfumo maalum wa kuunda Wizara za Muungano;
 7. Hakuna bajeti wala mapato yaliyoainishwa kwa mambo yasiyo ya Muungano wala hakuna mfumo wa matumizi unaopaswa kutenganisha baina ya mapato na matumizi ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano;
 8. Hakuna mfumo wa kikatiba unaoipa haki Zanzibar kupinga maamuzi ya kisera yatayofanywa na Serikali ya Muungano ambayo ni kinyume na maslahi ya Zanzibar;
 9. Hakuna mfumo wa kikatiba unaoibana Serikali ya Muungano kufanya maamuzi yoyote yale kwa faida ya upande mmoja hata bila kuishirikisha Zanzibar na bila ya ridhaa ya Zanzibar;

Matokeo ya jumla ya mapungufu hayo ni kuwa Serikali ya Muungano iliyoundwa bila ya kuishirikisha Zanzibar inao uwezo wa kufanya maamuzi ya kisera na ya kiutawala bila ya ridhaa ya Zanzibar. Serikali ya Muungano inaweza kutumia rasilimali za Muungano kwa faida ya upande mmoja bila ridhaa wala kuishirikisha Zanzibar. Chini ya mfumo wa Serikali mbili unaojengwa na Katiba Inayopendekezwa, Zanzibar haimo katika Muungano bali ni sawa na iliyomo katika mahusiano ya kimahamiya (Protectorate).

Uhalali wa Rais wa Muungano kwa Upande wa Zanzibar [Ibara ya 89(6)]

Ibara ya 89, Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kuwa mgombea wa Chama au mgombea binafsi.  Chini ya ibara ya 89(6), mgombea urais atatangazwa ameshinda iwapo atapata zaidi ya asilimia hamsini ya kura zilizopigwa. Chini ya Katiba Inayopendekezwa, mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ni makubwa ikiwemo yale ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na sehemu.

Masharti haya yanazua maswali muhimu yafuatayo:

 1. Kama Zanzibar ni mshirika sawa katika Muungano, kwa nini isiwe na sauti hata kidogo katika kumchagua mtu wanayemkabidhi mamlaka ya utaifa wao;
 2. Iwapo kama Rais wa Muungano na chama chake hawakupata kura hata moja Zanzibar, uhalali wake wa kutekeleza mamlaka makubwa ya kiutawala kwa watu ambao hawakukuchagua unatokana na nini?
 3. Iwapo Zanzibar – ambayo ni mshirika katika Muungano – haikubaliani na usimamizi wa Rais katika masuala yao yaliyopo chini ya Muungano, ina haki gani ya kikatiba au ya kisheria ya kumdhibiti Rais huyo ikiwemo tabia ya Rais huyo kuonyesha dhahiri kuikandamiza Zanzibar?

Hicho ni kielelezo tosha kuwa Zanzibar haimo katika Muungano kama mshirika bali kama mahamiya.  Lakini pamoja na hayo, viongozi hao waliyakubali masharti hayo ya Katiba inayopendekezwa.

Mamlaka ya BUNGE [Ibara 134]

Ibara ya 134 ndio inayoimaliza kabisa Zanzibar.  Ibara hiyo inaeleza utaratibu wa namna 3:

 1. Kwanza, chini ya 134(1)(a)- aya hii inahusu utaratibu wa kupitisha Miswada ya inayohusu ama:
 • Sheria ya mambo yasiyo ya Muungano; au
 • Sheria ya Mambo ya Muungano yaliyomo katika Nyongeza ya Kwanza; au
 • Sheria ya Kubadili Katiba

Utaratibu utaotumika ni kwa kupitishwa Mswada huo ikiwa utaungwa mkono na Wabunge walio wengi.

 1. Pili ni ibara ya 134(1)(b) – aya hii inahusu utaratibu wa kupitisha sheria inayohusu ama:
 • Kubadili masharti ya Katiba [ni dhahiri kuwa sharti hili limejirudia kwani ni sawa na sharti la ibara ya 134(1)(a) iliyoelezwa hapo juu];
 • Kubadili masharti ya jambo lililotajwa katika Nyongeza ya Pili ya Katiba [ni mambo mawili 2- kubadili masharti ya Katiba ya Muungano yanayohusu Mambo ya Muungano na kuongeza au kupunguza jambo la Muungano]

Utaratibu ni utakaotumika ni kupitishwa iwapo Mswada huo utaungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wa kila upande.

 1. Tatu ni ibara ya 134(1)(c) – ibara hii inahusu utaratibu wa kupitisha sheria kwa mambo yaliyotajwa katika Nyongeza ya Tatu ambayo ni mambo matatu. Kwanza ni Muundo wa Jamhuri ya Muungano, pili, kuwepo au kutokuwepo Jamhuri ya Muungano na tatu ni kubadili masharti ya ibara ya 134. Utaratibu utaotumika ni wa kura ya maoni itayoungwa mkono na nusu ya wananchi wa kila upande.

Ibara hii ya Katiba Inayopendekezwa kwanza imerejea masharti ya ibara ya sasa ya 98 ya Katiba ya Muungano ambayo imekuwa ikipingwa na Zanzibar katika nyaraka, ripoti na maandiko yote.  Imekuwa ikipingwa kwa sababu kadhaa lakini muhimu ni kama zifuatazo:

 1. Inainyima kauli Zanzibar kama mshirika katika Muungano katika kuamua sheria za Mambo ya Muungano, ambazo kwanza zimependekezwa na Baraza la Mawaziri ambalo Zanzibar haina ushiriki, lakini sheria hizo ndio zinazoamua haki za kila upande katika Muungano;
 2. Inawafanya wabunge wa Zanzibar wasiwe na kazi yoyote katika Bunge la Muungano;
 • Inakamilisha dhana ya kuwa Zanzibar si mshirika katika Muungano bali imo kama mahamiya.

Mifano ya namna Zanzibar ilivyoathirika na mamlaka haya ya upande mmoja katika kutunga sheria za pamoja ipo mingi sana na ndio miongoni mwa mizizi ya fitna za Muungano. Miongoni mwa Sheria za Muungano zilizotungwa bila ya ridhaa ya Zanzibar au kwa kutozingatia maoni ya Zanzibar ni pamoja na Sheria ya Tanzania Revenue Authority ya 1996, Sheria ya Benki Kuu ya 1995, Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu na Sheria ya Money Laundering ambayo ilipelekea SMZ na SMT kutofautiana katika kikao cha SADC kilichofanyika Botswana na hatimaye kupelekea Zanzibar kutunga sheria yake ya Anti-Money Laundering.

Pamoja na Ibara hii kutumika vibaya dhidi ya Zanzibar huko nyuma, ibara hii sasa imekwenda mbali zaidi kwa kuutia kufuli mfumo huu wa ajabu na kandamizi wa Muungano kwa kuulinda kuwa hauwezi kubadilishwa mpaka kwa kura ya maoni. Sijui kama kuna namna mbaya ya kukosa uadilifu kuliko mtu aliyepewa dhamana kutetea maslahi ya nchi na watu wake, kuwafunga katika dhulma ya wazi kiasi hichi. Na bado viongozi wakakubali masharti hayo.

Mambo ya Muungano

Kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ikilalamika katika mambo ya Muungano kwa sababu zifuatazo:

 • Wingi wa mambo ya Muungano [kiasi cha 34 kwa sasa];
 • Kukosa ufafanuzi wa mambo ya Muungano;
 • Mambo ya Muungano kuikosesha Zanzibar nyenzo za kiuchumi

Mambo ya Muungano chini ya Katiba inayopendekezwa ni 21.  Mambo yote hayana ufanunuzi. Kwa mfano elimu ya juu.  Unaposema Elimu ya Juu maana yake ni nini.  Ni udhibiti tu au ni pamoja na mitaala, uanzishaji wa taasisi za elimu ya juu au ni pamoja na utoaji wa elimu ya juu.  Jambo jengine muhimu lililoingizwa katika Orodha ya mambo ya Muungano bila ya kuwa na hata ufafanuzi ni Mawasiliano.

Kwa hakika katika ulimwengu wa leo mtu anapoinyima nchi au hata uchumi wake haki ya kudhibiti Mawasiliano anakuwa wa ajabu kabisa.  Ripoti kadhaa za Benki ya Dunia zimeonyesha mchango wa Mawasiliano katika chumi za nchi na uchumi wa dunia kwa jumla.

Aidha, kutokana na maendeleo ya teknolojia na kuunganika kwa teknolojia [covergency of technology] mawasiliano ndio hatma ya nchi zote. Tulipofikia sasa kila kitu kinafanywa kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano, kuanzia miamala ya fedha, usafiri wa teksi na karibuni hata friji lako nyumbani litaweza kuagiza kile kilichopungua ndani ya friji. Unajiuliza hivi waliokubali Katiba Inayopendekezwa walikubali kwa uchu wa kipande cha ndizi tu au kwa sababu ya ugonjwa mbaya zaidi ya huo?

Kukosekana kwa ufafanuzi katika Katiba juu ya mambo ya Muungano ndiko kuliko ipelekea Zanzibar ikose haki zake katika Kampuni ya Simu ya Tanzania [TTCL] wakati ilipobinafsishwa pamoja na kwamba Serikali zote mbili zilikubaliana kwa maandishi katika Ripoti ya Muafaka wa Serikali Mbili kwamba haki ya Zanzibar ipatiwe ufumbuzi.

Jambo jengine ambalo limeingizwa katika Mambo ya Muungano bila ufafanuzi na linaiangamiza Zanzibar ni katika nyenzo za kiuchumi hasa kodi.

Kwa mfano, Kodi ya mapato ndiyo nyenzo kuu ya kuendesha uchumi wowote wa kisiwa ambacho hakina rasilimali. Kodi ya mapato ndiyo nyenzo ya kuvutia mitaji na ndio nyenzo kupata mapato hata katika rasilimali za nchi.

Jambo hilo limerejeshwa katika Orodha ya Muungano kupitia Katiba Inayopendekezwa bila ya ufafanuzi wa aina yoyote.  Maana yake Zanzibar ilipangiwa iendelee kubaki bila ya nyenzo hiyo muhimu ya uchumi milele.

Pamoja na kutokuwepo mabadiliko yoyote ya maana katika Mambo ya Muungano viongozi hao waliyakubali masharti hayo.

Kura ya Maoni Kubadili Muundo wa Muungano [ibara ya 134(1)(c) na Nyongeza ya Tatu

Katiba Inayopendekezwa imejenga misingi ya dhulma na kukosekana usawa na haki za washirika wa Muungano, jambo ambalo linawafanya watu wa upande mmoja wauchukie Muungano. Kwa upande wa pili, inawalazimisha dhulma hiyo iendelee mpaka pale anayedhulumu atapokubali kubadili dhulma hiyo kwa kupitia kura ya maoni

Hii ni dhulma kubwa dhidi ya Zanzibar. Haiingii akilini kwamba mtu ambaye ana kazi ya kuitetea Zanzibar akubali dhulma hiyo na kutaka kuirasimisha.

Itaendelea…

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

1 Trackback / Pingback

 1. La Prof. Kabudi, Zanzibar na Mtego wa Komba – IV – Zaima Media Network

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.