La Prof. Kabudi, Zanzibar na Mtego wa Komba – IV

Waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere (kushoto) na Abeid Karume.

Kwenye sehemu ya tatu ya uchambuzi huu wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud, mwandishi alimalizia kuchambua baadhi ya ibara za Katiba Inayopendekezwa vinavyoiangamiza kabisa Zanzibar, licha ya kupitishwa kwa mbwebwe kubwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutokea CCM upande wa Zanzibar, ambao wengine leo hii wanamkejeli Waziri wa Sheria na Katiba wa Tanzania, Prof. Palamagamba Kabudi, kwa kukitafsiri kile walichokipitisha kwa hiyari na ushawishi wao wenyewe kwenye Katiba Inayopendekezwa. Sasa endelea na sehemu hii ya mwisho.

Profesa Kabudi na Dhana Inayopotoshwa

Nimehisi ni wajibu kutanabahisha kwamba, pamoja na kwamba siungi mkono hata kidogo aliyoyasema Profesa Kabudi kwa vile si sahihi na hayaendani na wajibu wake wa kitaaluma na hata wa kimaadili na kiuongozi, lakini ni vyema kutafuta wapi tulipojikwaa na turekebishe.  Profesa Kabudi alianza kwa kuipotosha dhana nzima ya Muungano wa Tanzania pale alipoufananisha na Muungano wa India na Ethiopia.

Na Othman Masoud Othman

Kwanza nchi hizo sio za Muungano bali ni za mfumo wa Shirikisho la kugawana mamlaka [federal arrangement].  Pili, shirikisho la nchi hizo halikutokana na muungano wa dola huru (sovereign states).  Tatu, msingi mkuu wa kugawana madaraka baina ya Serikali ya Muungano (Shirikisho) na Serikali shiriki ni kile kiitwacho ugatuzi (devolution).

Kwa upande wa Muungano wa Tanzania, kwanza, umetokana na muungano wa dola huru, pili, dola hizo ziliungana kwa mkataba maalum wa kimataifa na tatu, msingi mkubwa wa kugawana madaraka baina ya Serikali ya Muungano na Serikali Shirika ya Zanzibar ni Mkataba wa Muungano, ambao uliweka mfumo wa kuhamisha madaraka (assignment of sovereign powers) kwa msingi kwamba, kwa yale madaraka yasiyohamishiwa katika Muungano, kila upande utakuwa na mamlaka kamili )exclusive powers).

Naamini kumbukumbu bado zipo jinsi nilivyofafanua katika kikao cha mawaziri wa pande mbili kule Dodoma juu ya upotoshwaji wa dhana ya Muungano katika Katiba Inayopendekezwa kwa kutaka kuingiza dhana ya devolution badala ya ile ya power assignment and exclusivity iliyoasisiwa na Mkataba wa Muungano, ambao unaeleza kwa ufasaha dhana hii.

Hata Mzee Rashid Kawawa alipokuwa akiwasilisha Mswada wa Sheria ya Kuridhia Muungano katika Bunge la Tanganyika, alitumia maneno fasaha sana katika dhana hii. Alisema wazi kuwa chini ya Mkataba wa Muungano, Zanzibar itatoa baadhi ya mambo yake na kuyaweka chini ya usimamizi wa pamoja wa Serikali ya Muungano. Kwa hivyo, chini ya msingi huo, Rais wa Muungano hawezi kuwa na residual power kwa mambo ambayo si ya Muungano kama Profesa Kabudi anavyotaka tuamini.

Pili, Profesa Kabudi anapokataa kwamba hakuna migongano katika katiba mbili, sijui anachukua wadhifa gani katika taaluma ya sheria. Maadili ya taaluma yanahitaji kuheshimu maamuzi ya mahkama za juu za nchi.  Mahkama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi mbili tofauti – ile ya Seif Sharif vs SMZ [1998] TLR 48 na ile ya Machano na wenzake 17 [SMZ vs ALI [2000]1 EA 216 – imeeleza bayana kwamba ipo migongano ya wazi na ya msingi katika katiba mbili na kushauri hatua zichukuliwe kuondoa migongano hiyo.

Tatu, migongano ya kikatiba haiwezi kuondolewa kwa kuisuluhisha kwa kupora madaraka upande mmoja na kuyapeleka upande mwengine. Dawa ya migongano ni kurekebisha katiba. Mifano ipo mingi. Katiba ya Switzerland ya 1874 ilibadilishwa mwaka 1999. Ajenda kubwa iliyopelekea kubadilishwa, pamoja na mambo mengine, ni kutokuwepo bayana jinsi Serikali za Kantoni zitavyoshiriki katika mambo ya nje hasa pale sera na maamuzi ya Serikali ya Muungano yanapoathiri maslahi ya Kantoni. Katiba mpya ya 1999 iliweka bayana na kwa lugha fasaha suala hilo kupitia ibara za 55 na 56.

Aidha, Kanuni ya residual powers haiwezi kutumika kutengeneza mamlaka ambayo tokea asili yake anayedai mamlaka hayo hakupewa na Katiba au Sheria za nchi.  Kutokana na kanuni hii inayodhibiti matumizi ya residual powers katika mahusiano baina ya mamlaka za nchi, ndio maana haikutumika katika muungano wa Uingereza. Pamoja na Uingereza na Scotland kuwa na miungano miwili; ule wa kifalme wa 1603 (Union of Crowns) na ule wa mkataba wa 1707 (Articles of the Union), lakini Mfalme James Stuart baada ya kuwa mfalme wa nchi zote mbili, za Scotland na England, alishindwa kuziunganisha nchi hizo mbili kwa kutumia mamlaka yake kama mfalme, ingawa yeye mwenyewe alihisi ana mamlaka hayo kwa kanuni ya residual powers.

Katika kulitekeleza hilo alifikia hata kutengeneza bendera mpya ya Muungano (Union Jack), lakini wenzake walimtanabahisha kwamba hana mamlaka ya kutumia residual powers za ufalme kwa suala hilo chini ya mfumo wa kikatiba wa nchi hizo. Ndio maana muungano wao rasmi ilibidi usubiri kwa zaidi ya miaka mia moja na hatimaye ukaanzishwa kwa kupitia mkataba wa muungano wa 1707, ambao ndio unaoipa Scotland haki ya kupiga kura ya maoni kuamua kama wanataka bado kuendelea kuwemo katika muungano kila wanapoamua kufanya hivyo. Kama Muungano huo ungeanzishwa na Mfalme Stuart kwa residual powers, Waskochi leo wasingekuwa wanafaidi uhuru wa kuamua juu ya hatma yao. Ni vyema kwa Wazanzibari nao kutahadhari sana na hichi kirusi kipya cha Muungano cha residual powers kinachotaka kupandikizwa na Profesa Kabudi.

Siamini kwamba mwalimu wangu hayafahamu haya na zaidi ya haya niliyoeleza. Labda wale viongozi wetu wa Zanzibar waliotuingiza katika mtego wa komba ndio inawezekana wanapata shida kuyafahamu haya na hata wanapofahamishwa, kwa kuwa wazi uchu wa kipande cha ndizi kinawakosesha tafakuri.

Hitimisho

Malumbano hayajawahi kuisaidia nchi yetu kutatua kero yoyote. Malumbano juu ya Muungano yamekuwa yakiendelea tokea mara tu baada ya Muungano kuasisiwa. Mwisho wa malumbano hayo, ni Zanzibar ndiyo inayopoteza, ndiyo inayozidi kuumia. Hakuna marekebisho ya maana yaliyofanyika, kwa vile ni dhahiri kwamba Muungano uliasisiwa juu ya ajenda ya siri na umekuwa ukilindwa juu ajenda na itikadi ya siri.

Viongozi wa Zanzibar ndio wenye wajibu wa kusimamia maslahi ya Zanzibar katika mahusiano haya. Inapotokea baadhi yao kuangalia maslahi yao badala ya maslahi ya nchi, ndipo Zanzibar inapoangamia.

Laiti ingekuwa katika mtego huu anayeangamia ni yule aliyefuata kipande cha ndizi tu, tungesikitika kwa vile ni mwenzetu lakini tungeweka tanga, tukatawanyika tukaendelea na mengine. Lakini, kwa bahati mbaya, mtego huu wa komba ulioingizwa Zanzibar ni tofauti. Katika mtego huu, komba anakula ndizi yake akaondoka, lakini kinachoangamia ni nchi na vizazi; dahri na milele. Bila ya shaka huu ni mtego mbaya zaidi.

TANBIHI: Hii ndiyo sehemu ya nne na ya mwisho ya mfululizo wa makala za Mwanasheria Othman Masoud Othman akiichambua dhana ya mtego wa komba na maangamizi ya Zanzibar kwenye Muungano yanayofanikishwa na wale wale waliopewa dhamana ya kuilinda Zanzibar. Tafadhali changia maoni yako kupitia hapa ama kwenye mitandao yetu ya kijamii. – Mhariri

 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

3 Comments

 1. Ni Fasaha Ya Kuyaeleza Matatizo/Kero Na Gonganishi Za Kikatiba ,Lakini Hoja
  Zake Zimelenga Kuhoji Uhalali Wa Muungano Kiitikadi Badala Ya Kujadili Kero
  Husika .Kwa Mfano Usajili Wa Meli.

  Suala La Residual Power ,Ndugu Othman ,Amelipindisha Kinyume Na Aliyosema
  Prof. Kabudi …suala la residual power linaibuka panapotokea gonganishi za Kikatiba
  baina ya Katiba Za Zanzibar 1984 Ya 2010Na Ya Muungano Ya 1977 Au Articles of
  the Union Ya April 1964 Mama Wa Katiba Zote .

  Anaposema Agenda Ya Siri Hii Ni Dhana Pandikizi Ya Siasa/Itikadi Ya Chama Cha
  Upinzani CUF.

  • Usajili wa Meli halijawahi kuwa tatizo hapo kabla, kwa sababu kila upande una mamlaka yake ya kusajili vyombo vya majini na nchi kavu. Na hasa ukizingatia kuwa, usafiri wa majini na nchi kavu sio masuala ya muungano. Hivi karibun Zanzibar imeweza kupata international registry yake ya meli, sasa hapa ndio tatizo limezuka. Kwanin zanzibar ndio wawe na international registry na sio Tz bara? Cha msingi kama Tz bara nao wanahitaji registry yao, wafanye mchakato separate huenda wakafanikiwa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.