Hoteli ya nyota tano na ukumbi wa kimataifa kujengwa Micheweni

Kampuni ya Kimataifa ya VAULT yenye Makao Makuu yake mjini Washington Marekani imeonesha nia ya kutaka kuweka Miradi ya Kiuchumi katika Ukanda wa maeneo huru ya Kiuchumi uliopo Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya VAULT Tawi la Tanzania Bwana Said Ali Said amesema Uongozi wa Kampuni hiyo umefikia uamuzi huo kutokana na maumbile mazuri ya Hifadhi ya Misitu pamoja na Fukwe za kuvutia watalii.

Bwana Said amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa VAULT iko tayari kuanza miradi yake wakati wowote kuanzia sasa iwapo itapata fursa hiyo ikilenga zaidi hapo baadae kujenga Hoteli yenye Hadhi ya nyota tano pamoja na  ukumbi wa kimataifa wa mikutano.

Aidha Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya VAULT amesema katika hatua za awali za miradi yao imepanga kutoa ajira zaidi ya wananchi 300 wazalendo wa maeneo ya ukanda wa Micheweni kwa lengo la kuwa karibu na wananchi hao.

Naye Mwakilishi wa kampuni hiyo kutoka Washington nchini Marekani Bwana Hirsi Dirir amesema taasisi za uwekezaji pamoja na zile za miradi ya kijamii nchini Marekani zimelenga kusaidia wananchi wenye kipato cha chini katika mataifa mbali mbali duniani.

Balozi Seif akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wawili wa Kampuni ya kimataifa ya VAULT uliofika Ofisini kwake Vuga kumueleza nia yao ya kutaka kuwekeza kwenye Ukanda wa maeneo huru ya kiuchumi Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali imefarajika na muelekeo wa uwekezaji huo katika ukanda wa Micheweni ambao ni jambo zuri kwa vile litasaidia kutoa ajira kwa vijana wa Zanzibar.

Balozi Seif ameushukuru na kuupongeza Uongozi wa Kampuni ya VAULT kwa uamuzi wake wa kutaka kuwekeza kwenye  ukanda wa Micheweni na kuushauri kuangalia uwezekano wa kuipa kipaumbele Miradi ya Uvuvi kwa vile visiwa vya Zanzibar vimezunguukwa na bahari sehemu zote.

 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.