MCHAMBUZI MAALUM

Hakuna mdharau ukweli aliyewahi kubakia salama

Ndugu zangu, nimeona tamko la Wizara ya Mambo ya Nje likieleza kuwa Balozi mbalimbali za Ulaya na Marekani ambazo hivi karibuni zimetoa kauli ya kukosoa mwenendo wa Serikali “hazijui hali halisi ya usalama wa nchi”. Kauli hii imenishangaza mno!

Nchi yetu imekuwa na tabia ya kijinga sana, kwamba serikali inaamini kuwa wao ndiyo wana hati miliki ya maono, mitizamo, halo halisi na mwelekeo wetu. Mtu yeyote anapotoa maoni na mtizamo wake juu ya nchi anaitwa “ametumwa”, “ana wivu”, “analeta chokochoko” “si mzalendo”, “ni mtu hatari” na mengineyo.

Katika historia ya dunia, wamiliki wa ukweli ni wananchi, wamiliki wa maono, mitizamo, mwelekeo na sisi ni nani – ni wananchi. Ndiyo maana mwananchi atakwambia “sina ajira”, mtawala atasema “huyo mvivu tu”, mwananchi atasema “sijavuna chochote shambani”, mtawala atajibu “serikali hailimi, usipovuna kufa kwa njaa”, mwananchi atasema “polisi wanatuua bila sababu”, mtawala atajibu “wanatimiza wajibu wao”.

Na Julius Mtatiro

Majibishano hayo kati ya mwananchi na mtawala yakupe picha halisi kuwa ukweli una mwenyewe, na mwenyewe ni mwananchi wa kawaida. Mtawala hawezi kuwa mkweli, dunia nzima! Watawala wakweli ni wale tu ambao nchi zao zina mifumo na vyombo huru ambavyo vinaweza kumwajibisha mtawala, vinaweza kufanya uchunguzi huru n.k.

Mauaji makubwa ambayo yanaendelea kutokea Tanzania, hali ya chuki na maneno ya kibabe kutoka kwa Rais na wasaidizi wake, mdororo na hali mbaya ya uchumi, mihimili ya dola (Bunge na Mahakama) kudhibitiwa na Rais, Vyombo vya habari huru kugeuzwa vituo vya propaganda za serikali au vichague kufungiwa…

Tume za Uchaguzi (ZEC na NEC) kugeuka kuwa matawi kindakindaki ya CCM, Jeshi letu la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa kugeuzwa kuwa vyombo vya kutumikia matakwa ya wanasiasa wa CCM na Serikali yake badala ya kuwa vyombo vya kulinda taifa zima na watu wake n.k. ndiyo hali halisi ya maisha ya Tanzania.

Hali halisi hii lazima isemwe na mabalozi wote, taasisi zote huru za kitaifa na kimataifa, viongozi wa dini zote, vyama vya siasa na kila mtanzania. Ukweli huu mkuu wa hali halisi ya maisha ya Tanzania hauwezi kubadilika kwa “tamko” la Wizara ya Mambo ya Nje, wala Tamko la Msemaji wa Serikali wala Tamko la magufuli.

Ukweli huu utasemwa kinyume chake na wamiliki halali wa ukweli (wananchi), ikiwa serikali itaamua kusimamia haki na matakwa ya ukweli unaomilikiwa na wananchi. Hakuna namna serikali itabadilisha hali hii kwa matamko bila vitendo.

Otherwise nawasihi watanzania, tuendelee kusema ukweli, tuieleze serikali ukweli, nawakumbusha kuwa hakuna serikali iliyoendelea kupuuza ukweli na ikabaki salama. Nawakumbusha tena kuwa malalamiko makubwa na manung’uniko ya sasa ni sehemu muhimu ya hatua za umma kujirejeshea haki na miliki zake.

Kwa kadri serikali inavyoendelea kudharau kelele hizi na ukweli huu, ndivyo inavyozidi kubaki na watu wachache wanaoiunga mkono (hasa Majeshi na wana CCM wenye vyeo).

Nyerere aliwahi kusema serikali zisisubiri wanaozipinga wawe wengi, maana wakati huo si majeshi wala vifaru huweza kuzuia mabadiliko ya lazima, baada ya serikali kutenda dhambi ya kudharau ukweli.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.