HABARI

Viongozi 5 wa Uamsho ‘waachiliwa’

Viongozi watano wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar waliokuwa wametoweka kwenye mazingira ya kutatanisha zaidi ya wiki tatu sasa, wameachiliwa na kurejea majumbani kwao katika mazingira pia ya kutatanisha.

Mmoja wa viongozi hao, Amir Haji Khamis, akizungumza kwa hali ya huzuni na wasiwasi, ameiambia Zaima Media hivi leo kwamba hawawezi kuzungumzia zaidi ya kushukuru kwamba sasa yuko huru na kwamba waliomkamata hawakumuuliza kitu chochote.

“Itoshe tu kuwa tuko salama. Hatuwezi kusema lolote zaidi,” alisema kiongozi huyo ambaye alitoweka tangu mwanzoni mwa mwezi Februari 2018.

ANGALIA VIDIO: Viongozi wengine wa Uamsho watoweka, familia yawasaka, polisi wakanusha kuwashikilia

Jeshi la polisi lilikanusha tangu awali kuhusika na kuwakamata viongozi hao, ambao kwa mujibu wa mke wa Amir Haji waliwahi kuitwa na polisi kutakiwa awache kukusanya michango kwa ajili ya familia za viongozi wenzao walioko mahabusu Tanzania Bara kwa takribani mwaka wa nne sasa.

Akizungumza kwa njia ya simu na Zaima Media muda mfupi baada ya taarifa za kuachiliwa kwa viongozi hao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassar Nasser, alirejea kauli yake ya awali kwamba jeshi lake halikuhusika na ukamataji wao na hivyo halijui chochote kuhusu kuachiliwa kwao.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.