Mahakama ya Afrika Mashariki yaliondoa ombi la kesi ya Muungano

Majaji katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki mjini Arusha wameliondoa ombi la walalamikaji wa kesi inayopinga uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutaka, pamoja na mengine, kesi hiyo isikilizwe hiyo visiwani Zanzibar kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kwenye uwasilishwaji wake.

Akizungumza kwa njia ya simu na Zaima Media akiwa Arusha, mlalamikaji mkuu kwenye kesi hiyo, Rashid Salum Adi anayewakilisha wenzake 39,999, amesema baada ya kesi hiyo kuwasili mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na pingamizi za kila upande kusikilizwa na kujibiwa, imekubalika kuwa uwasilishwaji wa maombi yao ulikosa mambo ya msingi, ambayo yanahitajika kuwepo.

“Tumefika mahakamani lakini mahakama imekataa kuendelea kulisikiliza shauri letu kutokana na mapungufu yaliyotokea kwa wetu,” alisema Adi.

Licha ya kuondolewa kwa maombi yao kwa muda, kesi yenyewe ya msingi ambayo inahoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bado ipo pale pale na Adi aliiambia Zaima Media kwamba kufika kwao kwenye mahakama hiyo na kuwasilikiza wapinzani wao (upande wa serikali zote mbili) kumewasaidia “kuujuwa uzito na wepesi wao na woga wao pia.”

Kwa mujibu wa Adi, wanatazamia kurudi tena mahakamani hapo ndani ya kipindi cha wiki mbili kutoka sasa kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza.

“Tuna haki ndani ya wiki mbili kuliwasilisha tena mahakamani, na tunategemea kufanya hivyo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu,” alisema.

 

 

 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.