Adi afafanua kile hasa kilichotokea kesi ya Muungano EACJ

Kiongozi wa Wazanzibari 40,000 waliofungua kesi ya kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenye Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Rashid Salum Adi, amefafanua kwa kina kile hasa kilichotokea jana kwenye mahakama hiyo mjini Arusha, wakati kesi yao ilipotajwa kwa mara ya kwanza kabisa kwa kutanguliza ombi la awali ambalo liliondolewa na majaji wa mahakama hiyo kutokana na mapungufu ya kisheria.

 

Soma taarifa yake rasmi kwa vyombo vya habari hapo chini:

TARIFA RASMI JUU YA MAAMUZI YALIYOTOLEWA NA MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI KUHUSU KESI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR.

Tarehe 09/03/2018

Jana tarehe 08/03/2018 Kesi namba 9/2016 ya madai ya Uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyofunguliwa na Wazanzibari wapatao 40,000 ilisikilizwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Afrika Mashariki – Arusha, mbele ya Jaji Monica Mugenyi, Fakihi Jundu na Charles Nyawello.

Kwa upande wa walalamikaji, Rashid Salum Ady aliongoza timu ya Wawakilishi wa Wazanzibari hao wapatao 40,000 ambapo kwa upande wa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar hawakuhudhuria Mahakamani hapo na badala yake walipeleka wawakilishi wao.

Katika kesi hiyo, Jana ilikua ni siku ya kusikilizwa kwa Shauri namba Saba (applications no.7) la kesi hiyo ambalo kimsingi, pamoja na mambo mengine Shauri hilo linaiomba Mahakama hiyo ya Afrika Mashariki kuhamishia vikao vyake nchini Zanzibar ili kuendelea kuisikiliza kesi hiyo Visiwani humo. Mahakama ya Afrika Mashariki inayo uwezo huwo na imekua ikisikiliza kesi zake katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki zikiwemo Kenya na Uganda ambazo baadhi Mahakama hiyo imefungua matawi yake.

Ady na wenzake wameiomba Mahakama hiyo kufanya hivyo ili Wazanzibari waliofungua kesi hiyo waweze kuisikiliza kesi yao pamoja na kuweza kuifatilia.

Pia, katika Shauri hilo Ady ameiomba Mahakama ya Afrika Mashariki iwapatie ulinzi kipindi chote cha usikilizwaji na ughairishwaji wa kesi hiyo na kuiomba Mahakama hiyo iweke zuio kwa Serikali ya Tanzania isiendelee kutumia fursa za Muungano, kwavile tayari kuna kesi Mahakamani inayohoji Uhalali wa Muungano husika.

Kwa mujibu wa Ady ni kwamba, kwasasa Serikali ya Tanzania inapaswa kuacha kujishughulisha na maswala yote yanayohusu Muungano mpaka pale kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Hata hivyo, baada ya kupitiwa kwa maombi hayo, kulionekana kasoro ndogo ndogo ambazo Mahakama hiyo iliwaamuru Walalamikaji kwenda kuziweka sawa kasoro hizo na kurudi tena baada ya wiki mbili kwa ajili ya kusikilizwa rasmi kwa Shauri hilo.

NB:
Jana ilikua ni siku ya kusikilizwa kwa Shauri namba 7 tu na sio kesi ya msingi. Kesi yenyewe haijaanza kusikilizwa Hadi yatakapomaliza kusikilizwa maombi ya awali ya pande zote mbili za Wazanzibari na Serikali.

Imetolewa Na:

Rashid Salum Ady,
(Kiongozi wa Wazanzibari waliofungua kesi EACJ).

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.