UTAMADUNI

‘Kilio cha Usumbufu’: Diwani mpya yaingia sokoni rasmi

Kampuni ya uchapishaji ya mtandaoni, Zanzibar Daima Publishing House, imechapisha diwani mpya ya ushairi wa Kiswahili iitwayo ‘Kilio cha Usumbufu’ iliyoandikwa na mtaalamu wa lugha na fasihi na mwalimu wa siku nyingi, Maalim Ali Abdulla Ali.

Diwani hiyo, ambayo inaanza kuuzwa leo katika mtandao wa Amazon na washirika wake kote ulimwenguni, ina zaidi ya tungo zilizoandikwa kwa mitindo na miundo mbalimbali, ila zote zikifuata kanuni ya kimapokeo ya urari wa vina na mizani.

Akiandika kuhusu diwani hii na mwandishi huyu, bingwa wa Fasihi Andishi ya Kiswahili wa zama hizi, Profesa Said Ahmed Mohammed, ana haya ya kusema:

“Inahitaji sifa nyingi kwa mshairi kuweza kumteka msomaji namna hii! Kwanza, anahitaji kuwa na ukwasi wa lugha, na Ali Abdulla Ali anao wa kumiminika. Pili, ni jinsi mshairi anavyojua kuyatumia maneno yanavyostahiki mwahala mwake – katika miktadha ambayo msomaji angeungama kwamba yasingeliweza kutumika bora pahala pengine popote.”

Ali Abdulla Ali ni mzaliwa wa kisiwani Pemba na muda wote wa maisha yake ya kikazi amekuwa mwalimu aliyefundisha skuli kadhaa Unguja na Pemba, wakati huo huo akiandika kazi chungu nzima za Fasihi ya Kiswahili.

Miongoni mwa hadithi zake fupi kama vile: ‘Machupa’, ‘Mwanamke’ na ‘Mwenye Pupa’ ziliwahi kusikika katika kipindi cha ‘Karibuni’, cha Idhaa ya Kiswahili ya Deustche Welle nchini Ujerumani katika miaka ya 1980′.

Kazi zake za hivi karibuni ni pamoja na ‘Faidika na Methali, Nahau na Vitendawili’ (Phoenix Publishers) na tamthilia ya ‘King’ora cha Mwehu’ (Longhorn Publishers).

Aidha, Maalim Ali amechangia katika mikusanyo ya diwani kadhaa za hadithi fupi zikiwemo ‘Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine’ (Moran Publishers), ‘Homa ya Nyumbani na Hadithi Nyingine’ (Phoenix Publishers), ‘Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine’ (Longhorn Publishers) na nyinginezo.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.