Riwaya: Safari ya Kumuua Rais – 4

Tuliona sehemu iliyoisha Baada ya ndugu wawili kutoka Daadab na kuingia Mohadishu wakiwa na Ismail, wakaanza maisha ya uvuvi hapo, lakini ghafla mwenyeji wao akawaaga na kuondoka bila kusema anaenda wapi, lkn wao waliendelea vyema na uvuvi ambao uliwaingizia kipato kizuri,hadi Abdull akaanza chuo. Endelea…

Akiwa katika Chuo Kikuu cha Simad , Abudull alianza vyema chuo akajipatia marafiki wengi ambao walikuwa ni wanafunzi wenzake.

Idadi ya marafiki iliongezeka. Mmoja wa rafiki zake wakubwa alikuwa ni  Kassim ambaye aliishia karibu tu na Chuo.

Ulikuwa ni urafiki mkubwa mno,  hadi wakutembeleana katika familia zao, wakawa pia hawaachi kufanya mazoezi pamoja kila jioni.

Baba yake Kassim ni mwanajeshi mkubwa katika jeshi la Somalia, hapo ndipo Abdull alipofundishwa kushika silaha kwa mara ya kwanza.

Siku za Jumamosi na Jumapili Baba yake Kassim hutoka nje ya mji wa Mogadishu kwenda kuwinda ndege akiwa na Kassim na Abdull, tangu Abdull  anaogopa silaha hadi akaizoeya na kuwa mlenga shabaha mzuri sana.

Miezi ilikatika, biashara yao na kaka yake bado iliendelea kuwaendesha vizuri kimaisha na yeye akifanya vizuri pia masomoni.

Akafika mwaka wa pili Chuoni akichukua shahada ya Ualimu katika masomo ya Biology na Chemistry.

Kwa sababu ya kushiriki kazi za nguvu baharini na kuanza kupenda mazoezi tangu akutane na Kassim, akaanza kuwa na umbile la kuvutia sana, kifua kilichojaza na mwili mpana.

“Asalam aleykum”, ilikuwa ni salamu kutoka kwa binti mmoja aliyesima mbele ya Abdull. Ulikuwa ni wakati wa jioni, siku ile Abdull alienda kupumzika katika fukwe za Sekondo Lido, ilikuwa ni siku ya mwisho ya mapumziko ya katikati ya mwaka, kabla ya kurudi tena chuoni kwa muhula wa mwisho wa mwaka wa pili.

Licha ya kupumzika pia alikuwa anasubiri boti lao la uvuvi, kwani kundi la wavuvi wakiongozwa na Kaka yake, walienda asubuhi na kuahidi watarudi saa moja za jioni. Akiwa amevaa kaptula lilofunika magoti na fulani nyekundu, Abdull alikuwa ameketi katika jiwe dogo ufukweni pale.

“Waleykum salaam”, alitikia huku macho yake yakigongana na ya binti yule.

“Samahani lakini ni kama nakukumbuka ama nimewahi kukuona sehemu”, alisema binti yule  akitabasamu na kuzungusha kichwa chake huku na kule ishara ya aibu kidogo.

“Umeniona wapi?

“Simad University”.

“Sim..yap yawezekana kweli, nasoma pale, na wewe unasoma pale  pia?

“Ndio nasoma , nimewahi kukuona mara kadhaa..kuna siku nilikusalimia lakini hukuitikia..”.

“Oooh samahani…nadhani sikukusikia huenda mawazo mengi…”.

“Haina shida hata nami nilijipa matumaini kwamba hukunisikia..”

Baada ya kusalimiana hatimaye wakatambulishana majina yao, binti yule alimwambia Abdull kwamba yeye anaitwa Fartuun, alikuja ufukweni siku ile akiwa na marafiki zake.

Aliaga na kuondoka  nyuma akiacha anga yote imefunikwa na harufu nzuri ya manukato ambayo alikuwa amejipulizia.

“Mhh, hawa sio watu ..” ,Abdull alibaki anajisemea moyoni, baada ya dakika chache na yeye akaamua kuondoka eneo lile kwa hofu aliyokuwa nayo.

Alirudi nyumbani  , njia alimuandikia ujumbe mfupi wa simu Kaka yake, akimueleza kwamba watakapo karibia bandarini amjulishe.

Kumbe Abdull aliondoka ufukweni akiwa na hofu kwamba, yule binti aliyemtokezea hakuwa binaadamu, alipofika nyumbani kwao akabaki kumuuliza shemeji yake ambaye ndiye mke wa Talib, maswali magumu

“Kwanini unauliza hivyo sehemeji yangu?

“Yaani leo siamini, jini amenijia uso kwa uso..nilikuwa nimekaa hapo kwenye fukwe za Lido..”.

“Sasa wewe umejuaje kama ni jini?

“Majini wanajuulikana shem…kwanza Masha-Allah anavutia… eti anasema amewahi kunisalimia pale chuoni lakini sikuitikia…

Anadai kwamba siku aliyosalimiwa na Fartuun yeye haikukumbuki kabisa, akisistiza hana tabia ya kudharau salamu za watu, pia hakumbuki kuiyona sura ile sehemu yoyote.

Abdull aliendelea kulalama huku kijasho kikimtoka, mkononi ameshika gilasi ya maji akilainisha koo lake taratibu.

“Usiwe na wasi wasi..”, mke wa Talib aliendelea kumtoa hofu

“..halafu alivyokuwa  ananukia mafuta mazuri balaa yaani jini..nimemshitukia tu..”

Ni maelezo yaliyofanya mke wa Talib kucheka na kutabasamu, akaendelea kumsisitiza apunguze hofu,  akimueleza kwamba katika ufukwe ule watu wengi hufika kwa ajili ya mapumziko.

Baada ya dakika chache Abdulll alipokea ujumbe mfupi kutoka kwa kaka yake, ulioeleza kakaribia kwao katika bandari ya Mogadishu. Shughuli zote za usiku ule za kumsaidia kaka yake, alizifanya akiwa na mawazo pomoni kichwani mwake.

Hata alipokuwa kitandani kuutafuta usingizi ili aamke siku nyengine, bado mawazo yalimsonga akiamini kwa udhati kwamba kakutana na jini la kike katika fukwe.

Akizikumbuka zile hadithi za utotoni kwake; majini wanapenda sehemu za bahari na fukwe,wanavutia sana,  pia hupenda kunukia. Ni mambo  yaliyozidi kuuchanganya ubongo wa hadi akachelewa kupata usingizi.

Hata baada ya chuo kufunguliwa, aliongeza wiki nzima ya kukaa nyumbani. Baada ya wiki kupita ndipo asubuhi ya Jumatatu baada ya jua kuchomoza,  akajitayarisha na kuelekea chuoni, huku akiwa na hamu iliyochanganyika na hofu moyoni mwake.

Baada ya dakika kadhaa alikuwa tayari ameshawasili chuoni, akiingia kupitia geti kuu, akizungusha kichwa chake upande huu na ule, kana kwamba kuna mtu anamtafuta,  hakuwa mwengine aliyekuwa akimtafuta isipokuwa ni sura ya Fartuun.

Lakini hakufanikiwa kumuona, akaingia darasani alipomaliza kipindi akaelekea katika mjengo mlo wa  chuo ili kupata kifungua kinywa, bado alikuwa akijitahid kuzungusha kichwa chake akitegemea atainasa sura ya binti yule.

Hadi mchana anaondoka chuoni hakumuona , moyo wake ukazidi mashaka, lakini akaamua kulipotezea suala lile kidogo kidogo.

“Vipi umemuona huko chuoni? , mke wa Talib  alimuuliza Abdul,baada ya kufika nyumbani.

“Hutoamini, sijamuona..lakini bora tuache ni kheri tuipotezee hii hadithi sitaki hata kaka ajue..”

Wiki ikakatika  Abdull akienda chuoni wala hamuoni Fartuun,binti aliyemwambia kwamba nayeye anasoma chuo kile. Zile safari za kwenda akipumzika ufukweni akazipunguza pia. Siku mbili za mwanzo wa wiki iliyofuata hakuenda chuo  kwa sababu mafua yalikuwa yanamsumbua , siku ya tatu ndipo alipoingia chuoni tena.

Asubuhi na mapema kabla hajaingia darasani akakutana na rafiki yake Kassim, aliyempa taarifa kwamba kuna binti alikuwa anamuulizia siku mbili ambazo hakuwepo chuoni.

“Anaitwa nani?, aliuliza Abdull

“anaitwa Fartuun..”

Ni jina lililoshitua moyo wake kwa mara nyengine , akabaki akitoa macho bila ya hata neno moja kumtoka kinywani mwake.

“Alitaka nimpe namba yako ya simu lakini nikamzungusha kwanza, si unajua mpaka unambie mwenyewe..”

“Vizuri kwa vile hukumpa..”

“Lakini kanambia  umfate, yeye anasoma madarasa yaliyo karibu na maabara …”

Abdull alibaki anaitika kwa roho ya unyonge taarifa alizokuwa anapewa na rafiki yake, nywele za mikononi zikaanza kumsimama kwa hofu na hamu ya kutaka kuonana naye, ili roho yake ijue moja.

Aliondoka na kuelekea sehemu ya mapumziko hata darasani hakuenda tena, akimuacha Kassim akielekea darasani kwa ajili ya kipindi. Hakukuwa na watu wengi wakati ule, aliamua kutoa moja ya kitabu na kuanza kusoma, ili kurusha mawazo.

Lakini kila mstari anaougusa, kulikuwa na swali linakuja kichwani mwake, akijiuliza kuhusu Fartuun. Hazikupita dakika nyingi ghafla  akamuona binti anakuja upande ambao alikuwa amekaa.

“Fartuun anasema umsubiri ..”, ndio ujumbe aliokuja kuuwacha binti yule baada ya salamu kisha akaondoka na kurudi alikotoka.

Ni ujumbe uliomuacha Abdull akiendelea kutafakari, na kuzama zaidi katika tafakuri hadi akahisi anapotea katika taswira ya mazingira yale.

Lakini baada ya robo saa, macho ya Abdull yaligongana na binti yule yule ambaye alimuona kule fukweni

Na Rashid Abdallah

akivuta hatua kuelekea alipo

“Abdull , hujambo?, aliuliza Fartuun kwa uchangamfu kabisa huku akitabasamu

“Sijambo,  na wewe mzima?

“Mzima, rafiki yako alinambia unaumwa , vipi hali yako..?

“Niko vizur, ni mafua tu”

“Hata taarifa ya kuumwa jamani hatupeyani?, aliuliza huku akimuangali Abdull usoni kwa jicho la kuibia ibia.

“ hakukuwa na namna ya kukufanya ujue..”

“Basi nipe namba yako..wakati mwengine usije kupata sababu..”,  huku akitoa simu yake kujiweka tayari

Hakukuwa na mazungumzo ya ziada baada ya hapo,  Fartuun aliaga akidai  wenzake wanamsubiri kwa ajili ya kufanya kazi ya kundi.

Fartuun ni binti anayevutia kwa rangi yake, mwili wake uliojazia kwa kiasi ulikuwa ni mvuto kwa wanaume wengi, hakuwa binti mwenyewe maringo ingawa familia yake ilikuwa inajiweza.

Abdull alirudi nyumbani,  roho yake ikiwa imemtulia kwa kiasi fulani, lakini hakutaka kulizungumzia suala lile kwa shemeji yake tena.

Siku zikasonga na urafiki wa karibu kati ya Fartuun na Abdull ukaanza, walikuwa ni marafiki wa karibu sana, huku mapenzi yakianza kuchipua katika mioyo ya wawili hawa.

Lakini hadi mwaka unamaliza kila mmoja anaingia mwaka wake wa mwisho chuoni, hakukuwa na cha zaidi kinachoendelea kati yao zaidi ya urafiki tu wa kawaida.

Kwa sababu ya wingi wa mapenzi ya Fartuun kwa Abdull, hata alipokuwa akiwaaga mashoga zake akimfata Abdull kwa ajili ya kwenda mjengo mlo  kupata chakula cha asubuhi au mchana pamoja , alikuwa akiwaambia kwamba anaenda kwa shemeji yao.

Walikuwa hawaachani mara kwa mara wakiwa chuoni hata wakati wa kurudi.

“Umewaambia mashoga zako waniite shemeji yao…?, kwa utani Abdull alimuuliza Fartuun ,  ilikuwa ni jioni moja wakiwa wameongozana wakirudi chuo.

“No! No! No!..hapana kabisa..”, alikataa huku akitabasamu na kuficha uso wake kwa mtandio

Jambo lililomfanya  Abdull naye atabasamu kisha wote wakaanza kucheka,  ingawa walicheka kwa pamoja lakini kila mmoja alikuwa na sababu yake ya kucheka.

“Unanitia aibu na wewe…maswali gani hayo!, alilalama Fartuun akiwa bado anaendelea kucheka.

Kipi kitaendelea kati ya Abdull na rafiki yake mpya (Fartuun)? Safari ya kumuua rais imegeuka na kuwa safari ya mapenzi? Ni kisa gani kilichowakimbiza Abdull na Talib kwao? Nini kitaendelea Unguja? Tukutane wiki ijayo….

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.