Mbowe aitwa tena polisi, atowa waraka mzito kwa taifa

Leo tarehe 22 Machi 2018, mimi na viongozi wenzangu waandamizi wa Chadema tumetakiwa tena kuripoti Polisi. Tunaokabiliwa na usumbufu huu ni pamoja na Mhe Vincent Mashinji (Katibu Mkuu), Mhe. John John Mnyika, Mbunge na Naibu Katibu Mkuu Bara, Mhe. Salum Mwalimu Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar; Mhe Halima J. Mdee, Mbunge na Mwenyekiti wa Bawacha, Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mhe. John W. Heche, Mbunge na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti (Mara, Simiyu na Shinyanga) na Mjumbe wa Kamati Kuu; Mhe. Esther N. Matiko, Mbunge na Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Mara na Mweka Hazina wa Bawacha Taifa.

Tuna taarifa pia ya kusudio la kumuunganisha Mhe. Peter Msigwa, Mbunge na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa (Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa) na Mjumbe wa Kamati Kuu katika shauri hili.

Historia ya wito:

Kwa muda wa wiki tano sasa, kufuatia sintofahamu kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro, tumekuwa tukisumbuliwa kuripoti Polisi kila wiki kwa mashtaka ambayo hayajawahi kuwekwa bayana.

Katika kampeni na chaguzi hizi, palijitokeza mambo mengi ya ukiukwaji wa Haki za binadamu, ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, matumizi mabaya yamadaraka ya kiserikali, udhalilishaji na unyanyapaa dhidi ya Vyama vya Upinzani, mauaji na mateso kwa viongozi wa vyama vya Upinzani na hata Wananchi wasio na hatia.

Wakati nenda rudi hii ikiendelea, tuna taarifa (asante teknolojia) kuwazinapangwa njama mahususi za kutubambikia viongozi wa Chadema kesi zaMauaji au Uhaini ili kuhalalisha azma ya Watawala kutuweka mahabusu kwamuda mrefu, wakidhani kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanikisha kufifisha na hata kuua kabisa uwepo wa Upinzani katika Taifa.

Jitihada hizo ni pamoja na kujaribu kuhusisha viongozi, wanachama nawapenzi wa chama chetu na tuhuma aidha za Kigaidi, Mauaji na hataUhujumu wa Uchumi.Mkakati huu Kitaifa unashinikizwa na Rais John Pombe Magufuli nakuratibiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Dk ModestusKipilimba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, Jeshi la Polisi,na Ofisi ya DPP.

“Viongozi” hawa, wasaidizi na washirika wao wamejazana matumaini hewakuwa vuguvugu la mabadiliko na uhitaji wa demokrasia ya kweli na vita dhidi ya udikteta katika taifa hili litazimwa kwa “kuwaficha, kuwapoteza na hata kuwaua” viongozi wa Chadema na wanaharakati wengine wanaoamini katika
uhalisia huu.

Naam, njama hizi zaweza kuua baadhi, kujeruhi baadhi na hata kupotezakadhaa! Lakini kamwe, hazitazima njozi za Watanzania wema kupigania haki na ustawi katika nchi yao.

Naamini kwa kuzima uongozi wa Chadema uliopo leo, siyo tu kutaruhusu kuchipua kwa kasi kwa uongozi mbadala, bali pia kutaamsha ari ya taifakuongeza juhudi katika harakati ili hatimaye kutokomeza udikteta na uongozi wa kiimla katika nchi yetu.

Taifa lina msiba! Wanasiasa, wanaharakati, wanahabari na hata wasanii wanateswa, wanafungwa, wanajeruhiwa na wengine kuuwawa!Wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje wanalia! Viongozi wa dini wanachanganyikiwa! Wakulima, wafugaji na wavuvi wako hoi! Hata watoto na wanafunzi nao ni tishio kwa watawala!

Taifa limejazwa hofu. Wengi hawasemi, lakini wanataabika rohoni. Wanaisubiri fursa iwavyo vyovyote vile. Nguvu, majeshi na silaha zao, magereza na mifumo kandamizi haziwezi kuwa suluhu ya uimla huu. Tuimarishwe badala ya kufifishwa.

Hatukimbii!! Tuko tayari kwa lolote, popote!

Shime Watanzania! Msitulilie! Lilieni watoto wenu na Taifa la kesho.

Na iwe vyovyote iwavyo! Damu, mateso, dhihaka dhidi ya maisha yetu iwe chachu ya dhati katika kutafuta Tanzania aliyoikusudia Mwenyezi Mungu yenye kusimamia haki, demokrasia, usawa, utu na ustawi kwa wote!!

Aluta Continua!!!

Freeman Aikaeli Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai kwa Taifa

 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.