UTAMADUNI

Riwaya: Safari ya Kumuua Rais-6

Tulipoishia tuliona Abdull alivyoalikwa kwao Fartuun kisha binti huyo akaitambulisha familia yake kwamba huyo ndiye mchumba wake, baada ya siku kadhaa Talib anamshawishi Abdull waondoke wakalipize kisasi…Endelea….

“Sio ngumu,ni kushirikiana tu kila kitu kinawezekani..nitapanga mpango kamili ili tuingie katika utekelezaji..”, Talib alikuwa anasisitiza mpango wake kwa Abdull

Abdull alibaki na mawazo lukuki baada ya kuelezwa jambo la kulipiza kisasi na kaka yake, hamu ya kumwaga damu ya mtu kwa ajili ya kisasi alikuw nayo, hivyo haikumchukua dakika nyingi kukubaliana na wazo lile kwa asilimia zote.

Lakini uhusiano wake na Fartuun ndilo jambo pekee lililokuwa likimuumiza kichwa , alishaahidi kumuoa na kila mmoja kazama kwa mwengine kwa mapenzi ya dhati.

Kwa Talib hakuna jambo la kupoteza wala kumuumiza kichwa, miezi ilishakatika tangu aachane na yule mke wake wa Kisomali, wala hawakubahatika kupata mtoto yeyote.

Asubuhi yake Talib aliamka akiwa na mpango kabambe  jinsi gani watafanikisha lengo lao. Mpango alipouweka mezani na kuujadili yeye na ndugu yake,  wakakubaliana kwamba Abdull ndio awe mtendani mkuu, sababu moja kubwa ni uwezo wake mzuri wa kutumia silaha.

Siku chache baada ya Abdull kumaliza mitihani yake ya mwisho wa muhula na mwaka wake wa mwisho pia, changamoto ikawa jinsi ya kumuaga Fartuun, awali alifikiria  kuondoka bila ya kumwambia lolote.

Jioni ya siku ya pili ilikuwa ni ahadi ya Fartuun na Abdull kwamba watatoka nje ya Somalia na kwenda kutembea kidogo, ilikuwa ni safari ya kuelekea katika shamba la Familia ya Fartuun lililopo nje ya mji wa Mogadishu.

Fartuun alikuwa na usafiri binafsi ambapo ilikuwa ni gari ya Baba yake.

“Hii gari itakuwa yetu Baba yeye atatafuta nyengine”, Fartuun alinena huku akizungusha usukani barabarani kuelekea walikokusudia.

Abdull alijibu kwa sauti ya chini tena ya kuguna tu.

“Lakini leo hujachangamka, unaumwa au kuna mtu kakukera..?

“Hamna mbona niko poa”

Na Rashid Abdallah

Ingawa Abdull alikuwa anaficha kilicho moyoni mwake, lakini alielewa wazi ugumu wa lugha ya kumwambia Fartuun hadi aelewe kwamba yeye anataka kuondoka, fikra za mwambi-usimwambie ndizo zilizokuwa zinazunguka kichwani mwake.

“Abdull, Abdull unataka watoto wangapi wewe? Ilikuwa ni sauti ya Fartuun mara baada ya kutumia masaa kadhaa kisha wakafika sahambani kwao, Abdull alikuwa mbali kidogo akijaribu kutafuta namna ya kupata kamba ili kupanda na kuangusha madafu.

“Bora kumi na mbili…”

Ni jawabu iliyowafanya wote wacheke kwa sauti, huku Fartuun akitoka alipo na kumkimbilia Abdull alipo akiwa ameshika fimbo mkononi.

“Rudia ulichokisema, timu yako ya mpira…”, huku akiwa na fimbo  kamsimamia Abdull mbele yake, lakini wote wakitabasamu na kucheka.

“Nimesema wawili”

Ulikuwa ni wakati wa furaha kwa wote, utani na vicheko, lakini mara kwa mara Abdull alikuwa anazama katika dimbwi la mawazo ni jinsi gani ataondoka Somalia na kumuacha Fartuun. Abdull alijua wazi kabisa jinsi Fartuun alivyozama lisingekuwa jambo rahisi, ni binti ambaye leo-kesho anatamani kuwa mke.

Kuna wakati alikuwa anamueleza Abdull kwamba ameshachoka kuwa peke yake, hamu yake kubwa ni kuwa na mwenza ambaye wataishi pamoja hadi mwisho. Daima hakuacha kumsisitiza Abdull kwamba, hakuwahi kumpeda mtu kama anavyompenda yeye, hivyo hataki maumivu.

Kila alipokuwa akiyafikiria matukio ya nyuma na ahadi walizoahidiwa, moyo ulimuu Abdull, akajikuta machozi yanamtoka. Lakini hakutaka Fartuun aone machozi yake. Fartuun alikuwa ameenda upande mwengine wa shamba kwenda kuonana na mlinzi, akamuacha Abdull akitengeneza madafu ambayo walipanga kuyachukua.

Walikuwa pale tangu jua linachoma hadi likaanza kupoteza ukali wa mionzi yake, mawingu ya njano yakaanza kuchomoza kwa mbali.

“Halafu sijakwambia, Baba amemtafuta mwalimu wa kukufundisha gari”

“ah”

“Eti kulikuwa na Mwalimu mwanamke ndio walitaka kumleta, aah palichimbika mbona”

“Hilo wazo la mimi nifunzwe gari alilitoa nani?

“Aaah mmh sijui!”, ni jawabu aliyoitoa Fartuun huku akigeuza uso wake na kuangalia upande mwengine, mashavu yakitoa ishara ya mtu anayezuia kicheko.

Lakini mara tu Abdull alipoanza kucheka, naye akajikuta anacheka zaidi. Akimwambia Abdull kwamba maswali ya namna ile alishamkataza zamani lakini hataki kuyaaacha.

Baada ya dakika kadhaa wakakunja kila kilicho chao na kuanza safari ya kurudi Mogadishu mjini. Fartuun aliendelea kugundua mawazo mingi ambayo Abdull alionekana kuwa nayo kila safari ikisonga lakini aliamini ni machofu tu. Walipokaribia nyumbani kwao Abdull, alimuomba Fartuun amshushe tu njiani kwani kuna mtu alikuwa anaenda kuonana naye lakini haikuwa hivyo hakutaka Fartuun afike kwao, ingawa jambo hilo Fartuun alionekana kuligundua lakini alipotezea na kufanya kama alivyoombwa.

Usiku wa siku ule ulikuwa ni wa mawazo sana kwa Abdull, safari ya kuondoka ikiwa tayari na yeye moyoni hakutaka kumuacha mkono kaka yake. Aliamini udugu ni nzito zaidi kuliko upendo wa binti wa Kisomali.

Hatimaye akakubali ni lazima amuage, ndipo siku ilipofuata alimuita na wakakubaliana wakutane,  Fartuun akiwa haelewi anaitiwa nini. Walikwenda kukutana katika mgahawa wa Hoteli moja nje karibu na chuo walichosoma.

“Sorry kabla hujaanza lako, siku hizi nimeanza kuwa na tatizo la kusahau sahau maana nakufikiria sana wewe…familia inataka kuonana wewe na kaka yako ndani ya wiki ijayo..”

“Okaya, okay” , ilikuwa ni jawabu ya Abdull huku akijishika kichwa na kuiinama chini.

Alifikiria aanzaje wakati Fartuun ameshakuja na hadithi mpya ya kuhusu familia yake, lakini alimeza mate mazito na kutoa alilokusudia. Halikuwa jambo rahisi kwa Fartuun kumuelewa  baada ya  kumwambia kwamba anaondoka Somalia wala asingerudi tena, baya zaidi hakutaka kumuelewa anaenda Tanzania kufanya kwa jambo fulani muhimu.

Abdull aligoma kumwabia Fartuun. Kichwani Fartuun aliamini ni usaliti ambao Abdull aliamua kuufanya kwa kisingizo cha jambo muhimu.

“Okay, sawa haina shida tutaenda wote”, Fartuun aliamini ni sentensi ambayo Abdull angeikubali, lakini alizidi kushangaa alipoambiwa kwamba hakuna uwezekano wa kwenda wote.

“Mimi naenda kuwaambia nini familia yangu, wakati kwa sasa tuko katika maandalizi ya ndoa?, alihoji  kwa hasira akiwa amesima.

Fartuun alirudi kukaa kwa upole na kuanza kumshawishi Abdull ili abadilishe uamuzi wake, alimueleza kwamba asingeweza kuishi Mogadishu bila yay eye kwa jinsi anavyompenda.

Alifika hatu ya kumuahidi kazi ikiwa anakwenda Tanzania kwa jambo hilo, Fartuun alisema kwamba Baba yake angemsaidia kupata kazi nzuri tu, lakini uamuzi wa kuondoa aufute au wafunge ndoa kisha waende wote.

Maneno hayo yote yalikuwa kana kwamba anagong’omelea msumari wa udongo katika jabali gumu, hayakumuingia Abdull wala hakuonekana kuwa  hata wazo la kubadili msimamo.

Abdull hakutaka kumchukua Fartuun kwa sababu ya mazingira ya mpango wao,ungechukua muda mwingi na wala hakuwa na uhakika wa kurudi salama kwa uzito wa lile ambalo walikusudia kwenda kulifanya, ingawa waliliratibu kwa ujuzi wa hali ya juu.

Hasira zilizidi kumpanda Fartuun,  akaamua kusimama kutoka katika kiti  kwa mara ya pili na kuanza kulalamika wa sauti ya nguvu alipoona hakuna linalomuingia Abdull, hadi watu wote katika mgahawa ule wakaanza kuwaangalia wao, ilikuwa ni kama sinema ya Kihindi.

Bado Abdull aliendelea kubaki juu ya kiti, akimsisitiza Fartuun naye arudi kukaa. Abdull aliendelea kumshawishi akae kitako bila ya mafanikio.

Fartuun aliendelea kumshawishi Abdull asiondoke, huku machozi yakiwa yamerowesha leso na mtandio aliokuwa amejifunika, kijasho pia kilikuwa kinamkatika. Kuna wakati akitumia sauti ya upole kumshawishi Abdull lakini wakati mwengine hasira zilimpanda na kunanza kufoka.

Baada ya kuona hakuna mafanikio  aliamua kuondoka kwa hasira na kuchukua usafiri kumfuata kaka wa Abdull. Abdull alishawahi kumuonesha Kaka yake ingawa , Talib hamjui Fartuun lakini Fartuun anamjua Talib.

Alipofika nyumbani alimkuta Talib akiwa anaagana na baadhi ya wageni waliokuja kwa ajili ya kuzungumza.

“Natumai wewe ni Talib..?, aliuliza Fartuun  akizunguka huku na kule kwa hasira alizokuwa nazo, aligeuka na kuwa kama nyati aliyetoroka mbugani.

“Naam nikusaidie nini binti..”

“Naomba uniachie Abdull wangu, kama kuna jambo wewe ndo umemtuma tafadhali nakuomba nenda mwenyewe..”

“Wewe ni nani kwa Abdull?

“Ni mchumba wake na hadi kwetu ameshafika,wanamtambua vizuri tu,..”

Zilikuwa ni habari mpya kwa Talib lakini aliamua kuzipokea vivyo hivyo, akajaribu kumtuliza Fartuun kwani hata mwili wake ulikuwa unatetemeka wakati anazungumza, na uso uliobadilika rangi,  hasira zilimjaa.

Yalikuwa ni machozi ya damu, yakimtoka binti akililia upendo wake  kwa Abdull ambalo aliamini ndio unaenda kuzikwa kwa sababu asizozijua. Alijitahidi kusema na Talib ili amshawishi Abdull aifute safari yake, alisahau kwamba anazungumza na mratibu wa safari yenyewe.

Aliumia zaidi kwa kuwa hajui kipi kinamuondosha Abdull, akifikiria kwamba hakuwa kumsaliti, daima alijitahidi kumfanya kuwa na furaha kwani furaha ya Abdull ndiyo furaha yake pia.

Aliondoka pale, roho ikiwa imenyongeka mwili ulikosa nguvu kwa sababu ya maumivu aliyokuwa anayasikia moyoni. Aliamua kurudi katika ule mgahawa akiamini atamkuta Abdull lakini hakumkuta tena, hatimaye aliamua kurudi nyumbani kwao.

Ulikuwa ni usiku wa kujaza machozi katika lesso zake zote, alijaribu kumpigia simu Abdull lakini simu ilikuwa imezimwa. Akamtumia ujumbe akimwambia anatamani kuonana naye kwa mara ya mwisho,kwa sababu aliamini juhudi zake hazikuweza kufua dafu.

“Kmbe una mchumba hukunambia!!”, alisema Talib kumwambia mdogo wake wakati anaingia ndani usiku ule.

Lakini Abdull hakutaka kulizungumzia swala lile hasa kwa wakati ule, akamwambia Talib  watazungumza kesho kuhusu jambo hilo, bila ya kuchelewa akaingia chumbani kwake kwenda kupumzika.

“Usisahau safari ni kesho kutwa..”, yalikuwa ni maneno ya mwisho anamwambia Abdull ambaye tayari alishakuwa chumbani kwake.

Usingizi ulichelewa sana kumfikia , akiwaza hili na lile  bado akifikiria mbinu za kumtuliza Fartuun katika dakika za mwisho. Moyo wake pia ulimuuma kila anapoyakumbuka machozi yake.

Licha ya mawazo yote haya, bado moyo ulimwambia asirudi nyuma  kwani wanaloenda kulifanya ni muhimu zaidi kuliko mtoto wa Kisomali. Baada ya dakika chache akapata usingizi.

Fartuun hakuweza kulala usiku ule,hasa baada ya simu ya Abdull kuzimwa tangu aliporudi mgahawani na kumkosa. Alikuwa haamini ni kwa vipi mapenz ya dhati yanawenda kuyeyuka kwa sababu asizozitambua.

Ila ilipokuwa inakaribia saa kumi na moja za alfajiri ndipo alipopata usingizi.

Asubuhi  Abdull aliwasha simu yake na dakika chake tu ukaingia ujumbe mfupi kutoka kwa Fartuun akimuomba waonana kwa mara ya mwisho.

Alimjibu na kumtaka waonane katika fukwe za Sekondo Lido wakati wa jioni. Moyo wa Fartuun ilikuwa kama umemwagiwa tone la maji , alifarijika kupokea marejesho ya ujumbe alioutuma lakini  bado alikuwa anaumia moyoni.

Hata mama yake alianza kugundua mabaliko ya mtoto wake, usiku aliporudi hakutaka kula wala haikuwa kawaida yake, pia huchelewa kulala lakini aliingia kitandani mapema.

Asubuhi alimfuata kitandani kumuuliza ikiwa kuna tatizo lolote, lakini Fartuun aliamini bado ni mapema kueleza familia yake, kile kinachotokea kati yake na Abdull, hivyo alimwambia hajisikii tu vizuri lakini hakuna tatizo lolote.

Safari ya kumuua rais! Bado Fartuun ana nafasi ya kuizuiaya safari hii ya siri? Kukutana kwao kwa mara ya mwisho kutabalidisha lolote kwa Abdull?  Tukutane wiki ijayo…

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.