Maalim Seif awashukia Lipumba,Jaji Mutungi

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amesikitishwa na Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho  Profesa Ibrahim Lipumba kwa kuendeshwa kama kishada na kufanya kazi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Maalim Seif amesema  Lipumba kwa sasa siye yule Lipumba wa zamani wanayemjua, anashirikiana na makundi ya mungiki, akifanya kazi na CCM na msajili wa vyama vya kisiasa nchini Jaji Francis Mutungi kuihujumu CUF.

Ameyazungumza hayo leo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa ofisi ya wabunge wa CUF, Mogomeni jiji Dar es Salaam, wakati akieleza maazimio ya Kamati ya Utendaji ya Taifa ya chama hicho iliyokutana jana.

“Jaji Mutungi ni pacha wa Lipumba pia anafanya kazi zisizomuhusu, anachagua viongozi wa vyama na kuviendesha vyama atakavyo yeye, anachotakiwa  ni kukaa na vyama na kuvishauri lakini siyo hivyo afanyavyo yeye”, amesema Maalim Seif

Alipoulizwa kuhusu kauli ya Profesa Lipumba kwamba yeye ndiye anaihujumu CUF, Maalim amejibu kwamba Prof Lipumba sio msema kweli  akishangaa kuwa na elimu hadi akawa Profesa lakini muongo.

Maalim amewataka wafuasi wa chama hicho kuendelea kumpuuza Lipumba na wale wote wenye nia ya kukivuruga chama hicho , pia   waendelee kutunza amani na wasikubali kuchokozeka.

CUF imeingia katika mgorogoro tangu Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho Profesa  Lipumba kutangaza kufuta uamuzi wake wa kujiuzulu alioutoa tarehe 6 Agosti, 2015 na kutambuliwa  bado kuwa mwenyekiti  wa chama hicho na Jaji Mutungi,  upande wa kambi ya Maalim umegoma kumtambua kama mwenyekiti baada ya kujiuzulu kwake.

 

 

 

 

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.