Nape atema cheche juu ya demokrasia nchini

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amesema Tanzania inaweza kuwa Taifa la ovyo iwapo itashindwa kujifunza siasa za kuvumiliana hata kama yale yanayosemwa hayapendezi.

Nape ambaye amekuwa akiibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii kutokana na ujumbe mbalimbali anaotoa amesema ili Taifa liweze kutembea katika mstari ulionyooka, linapaswa kujenga utamaduni wa kuvumiliana.

Mwanasiasa huyo alisema hayo katika ibada ya kuaga mwili wa mmoja wa waasisi wa Chadema, Victor Kimesera aliyezikwa jana katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Kimesera alikuwa mwanasiasa wa aina yake na alivumilia mengi. Kwa maana hiyo, tunapaswa kujifunza siasa za kuvumiliana. Hata maneno tusiyoyapenda maana hii Tanzania bila kuvumiliana itakuwa nchi ya ovyo sana, lazima wakati mwingine tuvumilie hata tusikie maneno tusiyoyapenda,” alisema Nape.

Alisema amelazimika kufika Dar es Salaam akitokea Dodoma kwa ajili ya mazishi ya Kimesera kutokana na kuheshimu mchango wa kiongozi huyo.

Bila kutaja mwaka, Nape alisema alikutana kwa mara ya kwanza na Kimesera katika Klabu ya Gymkhana na tangu hapo aliendelea kushirikiana naye kwa mambo mbalimbali.

“Ndiye aliyenifundisha ustaarabu wa kucheza gofu na wakati mwingine tulitaniana mwishowe tunanunuliana kinywaji na yeye wakati wote alisisitiza sisi ni wamoja na tuishi kwa kuvumiliana. Atakumbukwa kwa hilo,” alisema.

Akimzungumzia Kimesera, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye alisema alikuwa mwanasiasa aliyepigania demokrasia ya kweli.

Sumaye amewataka Watanzania kuelewa kuwa bado wana safari ndefu ya kuifikia demokrasia ya kweli.

Alisema nchi bila kuwa na misingi inayozingatia demokrasia ya kweli inaweza kupotea njia, akisisitiza kuna haja ya kutambua matunda yaletwayo na demokrasia.

“Itakapofika wakati Watanzania watakapoona wamepata demokrasia ya kweli wataona wamechelewa lakini sasa wanaendelea kupitia katika mazingira magumu,” alisema.

Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Chadema alisema daima wataendelea kumkumbuka mwanasiasa huyo kutokana na ujasiri wake wa kupigania haki bila woga.

“Alifanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwingine alizunguka nchi nzima kuhubiri demokrasia. Tumepoteza mtu muhimu katika chama hata nasi jamii ya wafugaji tunamkumbuka namna alivyotupigania,” alisema.

Wanasiasa wengine waliohudhuria mazishi hayo ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita.

Kimesera alifariki dunia Machi 24 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na tatizo la saratani ya tumbo. Ameacha mjane, watoto watano na wajukuu 18.

About Zanzibar Daima 1613 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.