Upinzani hautakufa

CCM Zanzibar

Kuna mkereketwa mmoja wa CCM ambaye pia nina mashaka tele na upeo wake katika kuyaelewa mambo, ameandika kwenye ukuta wake hivi: “Wacha vyama vya upinzani vife. CCM yenyewe peke yake ni zaidi ya vyama vingi.” Akamalizia na kuhoji, “Unabisha?”

Hili inawezekana pia linawakilisha mawazo ya wana-CCM wengi. Kwamba ni jambo walitamanilo kwa udi na uvumba kutokea. Lakini wajiulize, kabla ya mwaka 1992 si tulikuwa huko huko? Na wakiwepo CCM peke yao, ndani ya bunge, wakafanya marekebisho ya katiba kuruhusu vyama. Je, walidhani baada ya kuruhusu vyama, hivi vyama vitakosa wafuasi? Au, vitaendelea kuwa dhaifu siku zote? Kwa kuona bandiko lake haliwezi kuachwa bila ya kutolewa ufafanuzi wa kina, ili kuepusha upotoshaji, nikamjibu kama ifuatavyo:

Kufa/kuuwawa kwa vyama vya upinzani hakumaanishi kufa kwa upinzani. Upinzani utaendelea kuwepo kwa muda wote wa maisha ya mwanadamu katika dunia hii pindi watu hawaridhishwi na mienendo ya mambo na hii zaidi inatokana na sisi waja kuumbwa tukiwa hatufanani maoni.

Ingekuwa sote tuna maoni yaliyo sawa, hapo ungejiaminisha kuwa upinzani nao umekufa. Kazi kubwa ambayo CCM wanajipa ni kutaka sote tufanane, hii ni kinyume na maumbile. Tujikumbushe kwa mifano michache ndani ya Afrika mara baada ya nchi hizi kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.

Watawala waliofuatia walizikuta nchi hizi zina vyama, Zanzibar ikiwa ni mfano mzuri. Wakafuta vyama na kusimika utawala wa chama kimoja uliotamalaki katika kila sekta. Kwa maana, hata huduma ya kawaida ya kijamii au haki ya kiraia, mtu hakuweza kuidiriki iwapo si mwanachama wa chama hicho kilichowachwa na watawala.

Katika mazingira hayo, kila mtu akalazimishwa kuwa mwanachama wa chama hicho. Jee, wapinzani hawakuwepo? Jee, upinzani haukuwepo? Maswali hayo mawili usiyajibu wewe wala mimi. Lakini wacha kwa pamoja tuyasawiri yaliyojiri takriban miaka 30 baadaye.

Hapa Zanzibar, uchaguzi wa kwanza kufanyika baada ya kuruhusu mfumo wa vyama vingi ulitoa matokeo yaliyojaa utata na kutoaminika. Lakini kwa hili, hata tukichukuwa takwimu za matokeo ya urais yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi chini ya uenyekiti wa Marehemu Babu Zuberi Juma Mzee (Matoza) yalikuwa yanafungana, 50.2% ya Mgombea wa CCM na 49.8% ya Mgombea wa CUF.

Haya, kama kuwepo kwa CCM peke yake kulimaanisha kukosekana upinzani/wapinzani, ilikuwaje tukapata matokeo haya? Hali kama hii pia inadhihirika pale Misri, baada ya miaka mingi ya tawala zilizokataa upinzani wa Muslim Brotherhood tokea kwa Gamal Abdel Nasser, mpaka kufikia Hosni Mubarak, na matumizi ya mkono wa chuma dhidi ya raia wao wanyonge, siku uchaguzi wa kweli na wa wazi ulipofanyika, chama tawala kikapigwa na chini. Itoshe mifano hii miwili, najuwa ipo mingi sana.

Upinzani kamwe hauwezi kufa wala kuuwawa, utakachouwa ni urasmi wa upinzani. Na hilo ni hatari zaidi. Upinzani ulio rasmi ambao wewe unatamani kufa kama si kuuwawa, unatoa fursa rasmi ya watu kuelezea mawazo yao na kufanya shughuli kwa njia rasmi ambazo zinakubalika kisheria, hakuna kinachofichwa katika utaratibu huo. Upinzani usio rasmi utazaa usiri na njama.

TANBIHI: Makala ya Abu Ajmal katika ukurasa wa Facebook, https://www.facebook.com/almas.ali.71216/posts/2294407260599634 

About Zanzibar Daima 1700 Articles
Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho

Be the first to comment

Leave a Reply