MCHAMBUZI MAALUM, SIASA

JPM ameshinda walau kwa sasa

“LINI?”  Ni swali nililojiuliza, mara kwa mara, tangu Januari 8 mwaka jana kila nilipomsikia Edward Lowassa akitajwa.  Januari 8, 2018, ndiyo siku Lowassa alipopokewa rasmi Ikulu na Rais John Pombe Magufuli.

Baadaye Lowassa alisema alifurahishwa mno na mkutano wao, kwamba walizungumza mengi na alimpongeza Rais “kwa kazi nzuri anayofanya”.  Mkutano huo baina ya Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mmoja wa viongozi wa upinzani aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ulinifanya nijiulize tena hilo swali la “Lini?”

Swali hilo nilizidi kujiuliza Lowassa alipokutana tena na Rais na kuambiwa awatahadharishe wenzake waache kuibeza serikali kwani wasipofanya hivyo wataishia gerezani.

Kwa urefu swali lenyewe lilikuwa: “Lini Lowassa atarudi CCM?”

Katika uchaguzi mkuu wa 2015, Lowassa aligombea urais kupitia Chadema, akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), muungano wa vyama vya Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi.  Hivyo sivyo alivyokuwa amepanga.

Kwa muda wa zaidi miaka 20 alianza kuwa na ndoto ya kuingia Ikulu kwa tiketi ya CCM.  Mwaka 1995, alijaribu kutaka CCM kimteue awe mgombea wake wa urais lakini inasemekana kwamba Mwalimu Julius Nyerere alimtilia guu asifanikiwe. Na hakufanikiwa.

Badala yake, Benjamin Mkapa alikabidhiwa bendera ya CCM, akagombea urais na akashinda.

Ulipofika uchaguzi wa 2005, Lowassa alimuunga mkono Jakaya Kikwete kuugombea urais kwa kufahamu kwamba ifikapo 2015  zamu itakuwa yake na Kikwete atamuunga mkono yeye kuugombea urais.

Lakini 2015 Kikwete alimgeukia Lowassa akihakikisha kwamba hatoteuliwa na chama chao kuwa mgombea wa urais.  Kampeni kubwa na chafu ilifanywa ndani ya CCM ya kumpinga Lowassa. Kila aina ya tope alirushiwa. Shtuma kubwa dhidi yake ilikuwa ya ufisadi.

Baada ya kukataliwa na CCM Lowassa alihamia Chadema Julai 2015.  Chadema hakijampokea tu lakini kilimkubalia awe mgombea wake wa urais. Kwa upande wa Chadema huo ulikuwa uamuzi mzito uliokitikisa chama hicho pamoja na umoja wa wapinzani wa Ukawa.

Watu walianza kuuliza iwapo Chadema ilijiharibia jina au ilifanya uamuzi wa busara na sahihi wa kumkumbatia Lowassa kwa vile hali yake ya afya haikuwa nzuri na zaidi kwa shtuma za ufisadi zilizokuwa zikimuandama. 

Awali kulikuwa na tetesi kwamba Lowassa atahamia Chadema akiwa pamoja na wabunge wa CCM wasiopungua 50 waliokuwa wakimuunga mkono pamoja na wenyeviti 22 wa mikoa wa CCM.  Hakuna idadi hiyo ya wabunge au ya wenyeviti wa mikoa wa CCM waliomfuata Lowassa. 

Wengi wakiamini kwamba Chadema ilifanya kosa kubwa kumfanya awe mgombea wake wa urais aliyeungwa mkono na  Ukawa.

Akikirihishwa na uamuzi wa viongozi wenzake wa kumkubali Lowassa katibu mkuu wa Chadema, Dkt. Wilbrod Slaa, alijiuzulu kutoka chama hicho.  Kwa upande wa CUF, mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba naye pia alijiuzulu kwa sababu hizohizo za kumfanya Lowassa awe mgombea wa urais atayeungwa mkono na Ukawa.

Hata hivyo, kuna waliohisi kwamba uamuzi wa Chadema wa kumkubali Lowassa ulikuwa sahihi licha ya ugumu wake.  Juu ya tope alizopakwa, Lowassa bado alikuwa na haiba ya kisiasa ilivyowavutia wengi. Hayo yalithibitika Watanzania milioni sita walipompigia kura katika uchaguzi wa urais.

Mwaka 2015 Lowassa aliukata kwa papara uamuzi wake wa kutoka CCM. Alifanya nongwa na alijihamasisha kuwaonesha na kuwatia adabu viongozi wenzake wa CCM waliomdhalilisha. Alikuwa na lengo moja tu la kuunyakua urais.  Huo uchu wa urais ndio uliomfanya aamue kuchupa aangukie Chadema.

Huu uamuzi wake wa “kurudi kwao” ni tofauti na ule wa Julai 2015. Huu wa juzi ni uamuzi alioukata baada ya kutafakari kwa muda mrefu. Katika tafakuri zake hakuzingatia mustakbali wake wa kisiasa tu bali pia aliuzingatia mustakbali wake wa kimaisha.   

Kwa ufupi, aliangalia “maslahi”. Maslahi yake binafsi, ya familia yake na ya biashara zake.

Alikwishaona kwamba mambo yake yanazidi kuwa magumu. Biashara zake zinakwamishwa,  mkwewe anasota gerezani na watawala bado wamekamia kuzidi kumtia adabu. Kwa vile alikuwa mpinzani wa kimaslahi, si wa dhati, hakuwa na hila ila asalimu amri.

Utawala wa mabavu ndivyo ulivyo. Hukubinya usiweze kufurukuta.  Hukubana koo usiweze kuvuta pumzi. Wanaojitolea kuupiga vita mfumo huo huwa tayari kujitolea kila walichonacho pamoja na roho zao. Lowassa hakuwa na moyo huo wala hana ujasiri huo.

Kurudi kwake CCM kumeizika kabisa ndoto yake ya kuwa Rais wa Tanzania. Bila ya shaka, miujiza hutokea na, kwa hali ya mambo ilivyo, ni muujiza tu utaoweza kumfikisha Lowassa anakokutamani. 

Nadhani kwa sasa baada ya kuzipiga hesabu zake za kisiasa Lowassa amekwishatanabahi kwamba hatoweza kamwe kuwa Rais wa nchi yake.

Pengine Lowassa angelikuwa Rais kwa tiketi ya Chadema, au hata ya CCM, angewapitisha Watanzania njia nyingine isiyojaa miiba na vigae.  Pasingekuwa na miiba ya kuwachoma na wasingekuwa wanakanyaga vigae. 

Kwa kurejea CCM, Lowassa ameufanyia fadhila kubwa upinzani, na hususan umoja wa Ukawa. Lile dosari lililojitokeza 2015 kwa wapinzani sasa hawanalo tena.  Kwa upande wa pili, viongozi kadhaa wa CCM waliokuwa wakitapika Lowassa alipoihama CCM sasa watalazimika wayale matapishi yao bila ya kuona haya.

Si hayo tu bali kuna uwezekano pia wa kuimarika makundi yenye kuhasimiana ndani ya CCM hasa katika kipindi hiki kinachoelekea uchaguzi mkuu wa 2020. Kwa sasa, Magufuli anaonekana mshindi kwa kuweza kuwarejesha wapinzani CCM wakiwa pamoja na kubwa lao, Lowassa.  

Kurejea kwao hata hivyo lazima kutaigharimu CCM. Sio vigogo wote wa chama hicho wenye kufurahishwa na jinsi “wasaliti” wa jana wanavyopokewa na chama chao na kutakaswa wakati waliwahi kutajwa kuwa mafisadi wakuwa waliokipaka tope chama chao na kutakiwa walivue gamba. 

Na wapo wenye kuudhika kwa ukali na ujeuri wa baadhi ya watendaji wakuu wa CCM. 

Kundi moja ni la wale waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa ambalo sasa linaelekea kuelemea upande wa Magufuli, ingawa kuna wasemao kwamba limeshinikizwa kufanya hivyo au limelazimika kufanya hivyo ili kulinda maslahi yao ya kibiashara.

Kwenye kundi hilo pia yumo Rostam Aziz aliyewahi kusema kwamba anajiengua kwenye siasa. Haikushangaza, hata hivyo, kuwa ni yeye aliyeandamana na Lowassa alipokwenda ofisi ndogo ya CCM “kurejea nyumbani”.

Kundi jengine linasemekana kuhusishwa na waziri wa zamani wa mambo ya nje Bernard Membe, ambaye amekaa kimya tangu 2015, pamoja na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Hili ni kundi lenye nguvu ndani ya CCM.

Kikwete alimaliza mihula yake ya utawala akiwa anahusika na matukio matatu makubwa nchini. 

Tukio la kwanza ni lile la kufifirishwa kwa mchakato wa kulipatia taifa katiba mpya, mchakato ambao uliligharimu taifa mamilioni ya fedha. Kuna wenye kuyaona matumizi hayo mabaya ya fedha za umma kuwa ni kosa la jinai na anastahiki ashtakiwe.

Tukio la pili ni la kumzuia Lowassa asiwe mgombea urais wa CCM  licha ya kwamba alikuwa na wafuasi wengi ndani ya chama hicho. Na tukio la tatu ni kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.  Mikono ya Kikwete inaonekana wazi katika matukio yote hayo matatu.

Kuhusu suala la uchaguzi uliofutwa wa Zanzibar walio karibu na Magufuli wanasema kwamba alikuwa tayari kufanya kazi na Maalim Seif Sharif Hamad, katibu mkuu wa CUF, lau angetangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Zanzibar, lakini alizuiwa na watu wa Kikwete.

Kama tetesi hizo zina ukweli basi Kikwete atapata taabu kutetewa pale historia hatimaye itapoamua kumhukumu.  Lazima iko siku ambapo vizazi vijavyo vitalazimika vikitathmini kipindi hiki cha historia ya Tanzania japokuwa viongozi wa sasa wanajaribu kuipotosha historia pale inapowagusa na kuugeuza uongo kuwa ukweli.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Rajab na kuchapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema. Mwandishi anapatikana kwa baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.