MCHAMBUZI MAALUM, SIASA

Maalim Seif, ‘The Terminator’

Kwa wale wapenzi wa filamu ya Hollywood, wataikumbuka filamu maarufu ya The Terminator, ambayo muhusika wake mkuu, Arnold Schwarzenegger, anapambana na maadui zake vya kutosha. Lakini bahati mbaya kutokana umadhubuti wake wa kimaumbile, anakumbana na sulubu za kutosha. Mara anajeruhiwa vibaya sana na kuna wakati anaaminika kuwa ameshakufa kabisa na maadui zake kuanza kufurahia ushindi. Muhusika anapokuwa katika hali ngumu kama hiyo, ndipo ghafla umuonapo ananyanyuka na nguvu kubwa ya ajabu ya kurejesha mapigo na hatimaye The Terminator anakuwa mshindi. Ujumbe mkubwa kwenye filamu hii ni kuwa The Terminator never dies, never defeated – yaani Terminator hafi wala hashindwi!

Ukitaka kuwa mkweli kwenye sanaa ya siasa tunayokwenda nayo nchini Tanzania kabla na hata baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, kama kuna mwanasiasa anayejitokeza kama mpambanaji asiyechoka, asiyevunjika moyo na anayejeruhiwa sana na maadui zake kiasi cha kwamba kuna wakati unadhani ndio ameshamalizika, lakini hapo ndipo anaponyanyuka na kuendeleza mapambano kwa nguvu kubwa na kila wakati anasamima akiwa mshindi, basi mwanasiasa huyu si mwengine ni Maalim Seif Sharif Hamad, The Terminator.

Akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akitokea kuwa waziri wa elimu na baadaye waziri kiongozi wa Zanzibar, Maalim Seif alifukuzwa nyadhifa zote hizo na baadaye kufukuzwa kabisa ndani ya chama mwaka 1988. Wakati anafukuzwa yeye na wenzake  saba, Mwalimu Julius Nyerere aliwaambia bora wakafanye upinzani wao nje ya Chama. Wakati huo hakukuwa na vyama vingi, hivyo hakukuwa na mbadala ama ufanye siasa ndani ya CCM au ustaafu siasa.

Maalim Seif alianzia hapo kupambana na maadui zake akiwa na kikundi kidogo cha watu hao saba aliofukuzwa nao aliweza kuwashughulisha watawala kiasi cha kumkamata na kumuweka ndani kwa miezi 36.

Wakati anatolewa ndani, vuguvugu la mfumo wa vyama vingi lilikuwa limeshaanza, akateuliwa uwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 1992. Chama kikiwa kichanga kikakumbana na mgogoro mkubwa uliomuhusisha wmenyekiti wake muasisi, James Mapalala, lakini Maalim Seif akaushinda mgogoro huo.

Katika hali isiyotarajiwa Uchaguzi wa mwanzo kabisa wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, Maalim Seif akiwa mgombea wa uraisi wa CUF, alimshinda Dk. Salmin Amour wa CCM na chama chake kupata viti vya uwakilishi 24 dhidi ya 26 vya CCM. Wakati huo, Maalim Seif akiwa na chama chenye umri wa chini ya miaka mitatu.

Hapana shaka, CCM haikuwa tayari kuona inashindwa na hivyo ikabadili matokeo na kumpa ushindi Dk. Salim Amour, mwenyewe akijuwa vyema kuwa alishindwa. Kwa matokeo hayo ya uchaguzi, maadui zake wakizidi kuongeza nguvu, maana kwa mara ya kwanza wakagundua kuwa kumbe hata baada ya vyote walivyomtendea, Maalim Seif hakuwa mtu wa kumdharau hata kidogo.

Ndipo wakaanzisha siasa za Unguja na Upemba, Uarabu na Uafrika, Uhizbu na Uafro na chama chake kunasibishwa na Uislamu.  Yote yalishitadi katika siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Yote yalimlenga yeye. Lakini yote hayo hayakusaidia chochote kumrejesha nyuma Maalim Seif.

Kinyume chake, aliyatumia kuzidi kujijenga na kukijenga chama chake na matokeo yake kikazidi kuenea kila kipembe sio tu ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba, bali Tanzania Bara pia.

Baada ya hapo, Maalim Seif kwa rikodi sahihi kabisa ambazo zinathibitishwa n ahata wana-CCM wenyewe, amekuwa akishinda kila uchaguzi unaoitishwa na anaoshiriki. Kielelezo cha juu kabisa cha ushindi wake ukawa ni uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wakati wapinzani wake wakiwa wameshatoka hadharani miezi michache kabla ya uchaguzi huo kwa bezo kubwa dhidi yake huku wakimwita “Bwege” kwa vile kulalamika kwake kuibiwa kila uchaguzi na pia wakinadi kuwa uchaguzi huo wa 2015 ndio ungelikuwa wa kuisambaratisha kabisa CUF kwa kipigo cha kura na ndio ungekuwa mwisho wa Maalim Seif mwenyewe, kiongozi huyu anayependwa kuliko yeyote na Wazanzibari akaibuka na nguvu ya ajabu, nguvu ya ushindi wa kishindo iliyopeleka taharuki kwa serikali zote mbili.

Pale Mapipa ya Ngozi, Kisiwa Nduwi, mpaka leo kuna taharuki na kulaumiana kusikokwisha. Waliotaka kumsambaratisha Maalim Seif, wameamua wenyewe kutangaza kustaafu siasa wakimuacha adui yao Maalim Seif, The Terminator, akitamba.

Naam, huyu kwa hakika ni Terminator. Na sasa hivi katika sehemu ya mwisho ya filamu yake na nimjuavyo mimi, Maalim Seif pamoja na machungu anayopitia hivi sasa yeye na wafuasi wake, atanyanyuka muda si mrefu.

Kama si leo ni kesho, akinyanyuka The Terminator najuwa umma ulio nyuma yake utanyanyuka naye kwa ari na nguvu ya ajabu, maadui zake waliojitepweka kwa kudhani wamemmaliza, wanapaswa wajiandae kupata kipigo wasichokitegemea kama ilivyowakuta 1995 na 2015. Maalim Seif kwenye siasa za Tanzania, hajawahi kuwa na mtu wa kumzuwia. Ni Terminator wa kwelikweli.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kwa jina moja la Mtumbatu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.